Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Mwanaidi Ali Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama hapa mbele ya Bunge lako Tukufu kuchangia hoja za Wabunge ambazo wamezitoa leo tarehe 30/05/2022. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nimshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini, kuniteuwa kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, ili kumsaidia kazi katika Wizara hii. Pia, nimshukuru Mheshimiwa Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana vizuri na kutusaidia katika Wizara yetu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee nimshukuru Mheshimiwa Dorothy Gwajima, Waziri wangu ambaye ananielekeza vizuri na kunisimamia katika kuelekeza maelekezo yote katika kuendesha Wizara hii. Bila kumsahau Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuendeleza ili kuhakikisha kwamba Serikali yetu inakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niipongeze Kamati ya Kudumu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa michango yao na ushauri na maoni katika kuboresha na utendaji wa majukumu ya Wizara. Niishukuru Kamati tunajitahidi kuzingatia maoni na ushauri katika kutekeleza majukumu ya Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana wewe pamoja na Naibu wako kwa umahiri wenu wa kuliongoza Bunge hili. Pia nisikose kuwashukuru Wenyeviti ambao wanasaidia kuliongoza Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nikishukuru chama changu cha CCM kwa kunipa heshima kuwa Mbunge na hii leo nipo hapa kama Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Pia nishukuru UWT kuanzia ngazi ya shina hadi mkoa, mkoa hadi Taifa, bila kuwasahau akinamama wa Mkoa wa Kusini ambao wameniheshimisha leo kuwapo hapa Bungeni na Taifa likaniamini kuniwezesha kuongea hapa katika Bunge hili tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba nitamke kuwa kuunga mkono hoja hii iliyowasilishwa kwa asilimia mia moja

Mheshimiwa Spika, naomba sasa kujibu hoja za Wabunge; kwanza tumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mimi katika hoja hizi za Wabunge nitajikita katika sehemu nne; wamachinga, malezi na makuzi ya watoto, wazee na wafanyakazi wa ustawi wa jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara yetu ina sera kama tano, Sera ya Maendeleo ya Jamii ya mwaka 1996, Sera ya Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2000, Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 na Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2001 na Sera ya Taifa ya Wazee.

Mheshimiwa Spika, tunakuja katika wamachinga; kwanza tumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuona umuhimu wa watu hawa ili kuendesha biashara zao ndogo ndogo katika Taifa hili. Napenda nimpongeze kwa upendo mkubwa aliokuwa nao katika Taifa hili, Mheshimiwa Rais ameunda Wizara hii kuhakikisha kwamba anataka kurejesha mila na desturi za Watanzania ili kuwe na utamaduni ambao tunautokea. Hivi sasa mila na desturi zote ambazo zina mmomonyoko mkubwa kwa hiyo, ameona umuhimu wa kuunda Wizara hii ili kuhakikisha kwamba yale yote ambayo tulikuwa tunapewa na wazee wetu waliotangulia basi tunayaleta na kuyafanyia kazi kuhakikisha nchi yetu hii inakuwa salama salmini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa wamachinga, Waheshimiwa wamechangia masuala mbalimbali kuwa maeneo Rafiki ili wafanye biashara zao bila kubughudhiwa.

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushurikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Halmashauri na viongozi wa SHIUMA tunaendelea kutenga na kuboresha miundombinu ya maeneo waliyotolewa kwa ajili ya shughuli za wamachinga. Pia tumshukuru Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa shilingi milioni kumi-kumi kwa kila Mkoa kuhakikisha kazi zao zinakwenda vizuri, ili kutimiza malengo yao waliyokuwanayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, wamachinga tunao vizuri na tunaendelea kusikiliza changamoto zao kuhakikisha kwamba taratibu zote za kiofisi zinakamilika ili waweze kuwa na taasisi ambayo itakuwa mfano katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu huduma za wazee; napenda kulithibitishia Bunge lako tukufu kuwa Serikali imeheshimu na inatambua kuwa wazee ni hazina kubwa ya rasilimali katika umuhimu na ustawi wa jamii wa maendeleo ya Taifa. Aidha, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 imeweka misingi ya kibinadamu kuwaheshimu na kuwathamini wazee. Katika kuhakikisha kuwa wazee wanapata haki zao na huduma za msingi, Wizara imefanya mapitio ya Sera ya Wazee ya mwaka 2003 na kuandaa mikakati ya utekelezaji wa kuwezesha utungaji wa sheria hiyo kuhusu pensheni ya wazee, mafao kwa watumishi wastaafu kulipwa kwa mujibu wa sheria ya kuanzishwa na mfuko husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha kulingana na mgawanyo wa majukumu suala hili lilitolewa ufafanuzi na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana na Watu Wenye Ulemavu. Aidha, Serikali inatambua umuhimu wa kuanzisha mpango wa pensheni katika jamii kwa wazee wote.

Mheshimiwa Spika, pendekezo na mpango huu umeandaliwa na kuwasilishwa katika vikao vya maamuzi ambavyo vimetoa maelekezo ya masuala ya kufanyiwa kazi ili kuweka mifano mizuri na endelevu pale mipango itakapokamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu wazee na makazi yao; Wizara inaendelea kutoa huduma na matunzo ya makazi 17 ya wazee yanayowezeshwa, mfano Nunge, Kibirizi, Njoro, Kolandoto, Ngeha, Bakumbi, Ipuli, Fungafunga, Mazangwe na Nandanga na mikoa mbalimbali ambayo inapewa huduma hizi za wazee. Hadi kufikia Machi, 2019 wahudumu katika makazi hayo ni 510 ambapo wana ndugu kuwatunza katika jamii hii. Huduma zinazotolewa katika makazi hayo ni pamoja na chakula, malazi na huduma za matibabu.

Mheshimiwa Spika, vilevile wazee wanaendelea kupewa huduma mbalimbali, Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya Awamu ya Sita inatoa fedha kila mwezi shilingi milioni 76.247 kwa ajili ya chakula. Vilevile inatoa fedha shilingi milioni 76.247 kwa ajili ya kuendeleza makazi kila mwezi. Vilevile Wizara inatoa vifaa tiba kwa ajili ya kupewa matatizo ya afya yanayowasumbua wazee hao.

Mheshimiwa Spika, wazee wanarudishwa kutoka nje ya makazi ili wasitumike vibaya. Kwa hivyo, Serikali yetu inawaenzi wazee na inawathamini kwa kila hali na mali ambazo wanahitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako tukufu niwaombe Waheshimiwa Wabunge wote wazee wanahitaji malezi, na sisi sote tumelelewa na wazee hawa na ndio maana leo tuko hapa na tunasimama imara kuwatetea wazee wetu hawa, kwa hivyo, wazee wanapokuwa washakuwa na hali ambayo hawajiwezi basi tuwaelimishe wananchi wetu katika majimbo yetu huko ili waweze kuwaenzi wazee wetu hawa kuhakikisha kwamba, nao wanafaidika na nchi yao, sio kuwapotezea na kuchukuliwa na Serikali. Pale tunapowachukua katika Serikali haina budi tu inabidi tuwalee wazee hawa kwa hivyo, tuwasaidieni wazee wetu, wazee ni tunu, wazee ni kila kitu katika maisha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu Maafisa wa Maendeleo ya Jamii...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muuda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Dakika moja, malizia Mheshimiwa.

NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, Wabunge wengi wamechangia kuhusu maafisa hawa. Naamini Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, tutahakikisha kwamba tunawaajiri na kuwapa malezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, muda ni mdogo, michango yote mingine ataelezea Mheshimiwa Waziri kutokana na nafasi yake. Mimi nashukuru sana, niwashukuru Wabunge wote ambao wamechangia Wizara yetu hii. Ni imani yetu kwamba tutafanya kazi kwa uadilifu na michango yote ambayo mliyotupa tutaitekeleza kuhakikisha Wizara yetu hii inakuwa kama Mheshimiwa Rais alivyoitathmini.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo yote naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, kazi iendelee. (Makofi)