Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Dr. Josephat Mathias Gwajima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru sana kwa kunipa muda ili nichangie na mimi hii hoja ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Kwanza nikushukuru wewe, lakini pia nimshukuru dada yangu Balozi Liberata Lutageruka Mulamula kwa namna alivyo-present hoja yake vizuri kwa ufupi na kwa namna ya kueleweka.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitajikita hasa kwenye suala la uraia pacha; nimeona suala la uraia pacha limeongelewa na watu wengi sana na limekuwa suala la muda mrefu sana. Kwanza nataka nioneshe kwamba uraia pacha duniani siyo issue ngeni, nazitaja kwa ufupi nchi ambazo zinaruhusu uraia pacha; ya kwanza ni Marekani yenyewe, Pakistan, Nigeria, Brazil, Bangladesh, Russia, Mexico, Egypt, Uturuki, Ujerumani, United Kingdom, Ufaransa naweza kuzitaja ni zaidi ya nchi 70 na kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kuna zingine zimeenda mbali zaidi kama Finland pamoja na Ufaransa wenyewe wameruhusu mpaka multiple maana yake mtu anakuwa na uraia zaidi ya tatu au nne. Sasa siyo issue ngeni duniani kwa sababu zaidi ya nchi 70 na kitu zinakubali suala la uraia pacha. Pamoja na presentation nzuri ya dada yangu Balozi Mulamula, lakini nimekuwa disappointed sana kwa jinsi ambavyo kwenye hotuba yake hakutaja kabisa kwa habari ya uraia pacha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Bunge lililopita tulilizungumza sana kwamba kwa ajili ya kuwasaidia ndugu zetu walio ughaibuni ni muhimu sana ku-consider uraia pacha, lakini kwenye hotuba yake hakuzungumzia kabisa kabisa. Kwa hiyo, nataka nimtangulizie dada yangu Balozi Mulamula nisipopata maelezo mazuri kwenye majumuisho yake ninalo kusudio la kukamata shilingi kwenye mshahara wake, nikipata maelekezo mazuri of course nita-withdraw.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo nimeona amelikumbuka kwenye hotuba yake ukurasa wa 83 amekubali kwamba kuna remittances kwa maana ya walio ughaibuni diaspora wame-transfer fedha kuja Tanzania mwaka 2020 almost dola milioni 400 na amesema mwaka 2021 wame-transfer fedha dola milioni 569.3; hizi pesa zimetoka ughaibuni au diaspora kuja hapa Tanzania zikiletwa na ndugu zetu walio ughaibuni. (Makofi)

Pia kwenye hotuba yake hiyo hiyo ukurasa wa 83 amesema kwamba hawa ndugu zetu wa diaspora pia wamenunua nyumba National Housing zenye thamani ya bilioni 2.3 na ameongeza pia wame-invest kwenye Hamidu City Park kule Kigamboni. Kwa hiyo, ametambua kabisa mchango wa watu wa diaspora na fedha au remittances ambazo zimetoka ughaibuni kuja hapa Tanzania, lakini namshangaa kwa nini sasa hajaona umuhimu wa kuwaza uraia pacha kwa hawa mabwana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria yetu ya Uraia Sura Na. 357 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 inatambua uraia wa aina tatu; uraia aina ya kwanza ni uraia wa kuzaliwa, uraia wa kurithi na uraia tajinisi. Sasa uraia wa kurithi ni ule ambao mzazi mmoja ni raia wa Tanzania akizaa mtoto anapewa uraia; uraia tajinisi ni uraia wa kuomba basically mtu anaomba uraia sawa sawa na criteria ya nchi yetu anapewa uraia na uraia wa kuzaliwa ni zawadi ambayo mtu anayoipata kutoka kwa Mungu, hakuna mtu anaweza kuzaliwa nchi mbili kwa mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapozungumza mimi kwa habari ya uraia pacha nilikuwa nakuomba sana Mheshimiwa Mulamula pamoja na wenzako wale Watanzania waliokwenda ughaibuni kutafuta Maisha, mtu amekwenda kusoma, amezaliwa Tannzaia ni Mndendeule, ni Mdigo, ni Mgogo, ni Mpare, ni Mnyaturu akaenda kubangaiza maisha kule na kwenye harakati ya kubangaiza maisha kuna baadhi ya nchi zinauwezo wa kutambua brain za watu wetu, anafanya vizuri Ph.D wanaangalia dissertation yake wanamuona mtu ubongo wake unafaa kutumikia nchi zao, wanawapa uraia, wanabaki kule siyo kwa sababu wanawapenda ili kusudi ile bongo yao itumike kwa ajili ya kuendeleza nchi zao. (Makofi)

Kwa hiyo, sisi kila mwaka na kila wakati tunakuwa tunawapoteza watu hawa kwa kuweka restrictions kwamba hatuwahitaji kuwa raia hawahitaji kuwa raia wa nchi zetu.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji Mheshimiwa Askofu Gwajima amesema vizuri kuhusu raia wa kurithi, hao raia wa kurithi wakikutana wakaoana huyu raia wa kurithi na huyu raia wa kurithi, wakizaa watoto wanakuwa ni watoto ambao hawana nchi yaani stateless individuals. Kwa hiyo its even worth na naungana mkono na hoja yako.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gwajima.

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea hoja ya Mheshimiwa Salome.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna hiyo tunakosa mambo ya muhimu sana, kwa mfano Taifa la Israel mwaka 1948 baada ya Wayahudi kuwa wamerudi kutoka kwenye nchi walizokuwa wametawanyika kila Myahudi alirudi na skills za nchi aliyokuwa, matokeo yake Taifa hilo limeendelea sana kiteknolojia kwa sababu kila mtu alikokuwa alirudi na maarifa au skill alizokuwa nazo. Kwa kuwapa watu wetu uraia pacha tunapata faida kadha wa kadha mojawapo ni skill transfer, mtu anakuwa kwenye ile nchi aliyokuwa amekaa ame-acquire skills fulani, anaporudi nchini kama raia wa Tanzania tunaweza ku-tap hiyo skill na kuitumia kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo tunapata tunapata freight capital, kuna baadhi ya Watanzania wamekaa kwenye nchi za kigeni wamefanya vizuri sana kiuchumi. Mimi nilikuwa kule North Caroline nikamkuta Mtanzania mmoja Mnyaturu wa kwetu kule Singida anamiliki University kubwa kama ile University of Dar es Salaam, ni Mtanzania; nilikuwa kule Canada wakati fulani nilikuta Watanzania watatu ni sehemu ya Baraza la Mawaziri katika Serikali ya Canada. (Makofi)

Sasa watu kama hawa tukiruhusu uraia pacha tunaweza ku-tap skills na ku-transfer capital kutoka kwao na tukapata hatua ya nchi yetu kuipeleka mbele zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini faida nyingine kwa kuwanyima uraia pacha tumewatenga na familia zao, ni masikitiko sana unapofika kwenye ubalozi zetu mahala pengine unawakuta wamejipanga kuomba visa ukimsemesha anaongea kindendeule, mwanamke ni Mndendeule, mwanaume ni Mndendeule, watoto Wandendeule wanaomba visa kuja kwenye nchi yao Tanzania, it doesn’t make any sense....

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Gwajima, kengele ya pili hiyo.

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie tu kidogo, kwa hiyo kwa sababu hiyo, nilikuwa naomba kama itakupendeza tujitahidi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ni human resource; nchi yetu ina natural resources nyingi sana, lakini natural resources ili uzigeuze ziwe hospitali uzigeuze ziwe shule inahitaji human resource ya watu hawa...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gwajima mengine unaruhusiwa kuleta kwa maandishi.

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja, lakini nisipojibiwa vizuri nitaondoa shilingi, ahsante sana. (Makofi)