Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shaurimoyo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kuweza kupata nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Awali ya yote napenda nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, lakini vilevile napenda nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi. Nawapa pongezi hizo kwa kuweza kushirikana kwa pamoja kuipaisha nchi yetu ya Tanzania katika anga ya kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumza suala hili la namna Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anavyofanya kazi kwa ajili ya kuipaisha nchi yetu katika anga ya kimataifa na hapa nataka nizungumzie kuhusu hii Royal Tour pamoja na Dubai Expo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Watanzania wenzetu wachache wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii katika kubeza hili suala la filamu hii ya Royal Tour, lakini nafiriki wangekuwa wanaijua faida yake nafikiri wangetulia kwa sababu na wao siku yoyote kama si leo kesho itawagusa katika mzunguko wa uchumi wetu wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, filamu hii la Royal Tour inaweza ikaongeza idadi kubwa ya wageni ambao wataingia nchini hususani watalii, lakini vilevile tunategemea kupata wawekezaji wengi kutoka mataifa mbalimbali kuja kuwekeza katika nchi yetu ya Tanzania na wanapokuwa wengi maana yake malipo ya viza yatakuwa mengi maana yake tutapata pato kubwa, lakini hoteli zetu zitajaa na zitachukua watalii kwa madaraja yote daraja la juu daraja la chini na madaraja ya kati, lakini vilevile italeta ongezeko kubwa la fedha za kigeni na hii itasababisha kuwa uchumi wetu wa Tanzania kuwa upo juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ukurasa 182 Ilani yetu imeelezea namna fursa ambazo zinatakiwa zifanywe na viongozi wetu kuweza kuhangaika na kuweza kuwatafutia maisha mazuri wananchi wote wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, historia inatuambia muasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitumia nafasi yake ya Urais muda mwingi kwa ajili ya kuweka mahusiano mazuri ya Tanzania na mataifa mbalimbali duniani, kwa hivyo haya ambayo anayafanya Rais wa sasa wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan sio mambo mageni yeye amejielekeza zaidi sasa hivi katika diplomasia ya uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nilikuwa napenda niwapongeze Mabalozi wetu hususani Balozi Mavura ambaye anaiwakilisha Tanzania katika nchi ya South Korea, amekuwa na jitihada kubwa katika kuunganisha Watanzania ili kuweza kupata fursa mbalimbali ambazo zipo South Korea. Lakini vilevile nimpongeze Balozi Kairuki ambaye analiwakilisha Taifa letu katika nchi ya China naye amekuwa mstari wa mbele katika kuhangaika na kuweza kuleta fursa mbalimbali katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Balozi Mahmoud Thabit Kombo ambaye anaiwakilisha nchi yetu katika nchi ya Italy, naye amekuwa anafanya jitihada kubwa katika kuunganisha Watanzania na hivi karibuni kulikuwa kuna tamasha kubwa kule nchini Italy ambalo linaitwa Macfrut lilifanyika katika mji wa Rimini, Italy tamasha hili liliwapeleka wadau wengi wa kilimo wa nchi yetu ya Tanzania na banda la maonesho ambalo lilitumiwa na Watanzania lilikuwa ni kivutio kikubwa kwa bidhaa mbalimbali ambazo zilioneshwa pale. Hivi sasa tunajionea wazi kwa Taifa letu linaanza kuwabeba wakulima wa kawaida wa Tanzania na kuwapeleka katika soko la kimataifa huko ughaibuni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hili suala sio suala la kubeza kwa hiyo tunaomba tumuunge mkono Rais wetu pamoja na Mawaziri wote ambao wanafanya kazi kwa niaba yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kiasi cha miaka minne iliyopita nchi yetu ya Tanzania iliingia mkataba na nchi ya Qatar na mkataba huu ulionesha wazi kuwa namna ya kuweza kupata ajira kwa Watanzania vijana pamoja na Watanzania ambao wana kada mbalimbali za kitaalam. Sasa hivi ni mwaka wanne lakini inaonekana bado jitihada za kuchukua fursa hizo na kuzifanyia kazi bado zimezorota, kwa hiyo nilikuwa namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa, malizia, sekunde 10.
MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Waziri akatapokuja hapa basi angalau aje kutueleza kuhusu mkataba huu wa Tanzania na nchi ya Qatar.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)