Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nichangie Wizara hii muhimu kwa uchumi wa Taifa letu, Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuipongeza Serikali angalau ilitoa ahadi ya tarehe mosi leo mwezi wa Sita wananchi wetu watapata ahueni ya kupungua kwa bei ya mafuta, sasa Serikali imechukua gape lile, wananchi wameona kidogo imepungua ingawa haijapungua sana, lakini angalau Serikali imeonesha njia na nina imani tunapoenda tutaendelea kupunguza zaidi kupitia Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hapa nitachangia mambo machache sana kwa upole sana ili Mheshimiwa Waziri kwa sababu ni bajeti yake ya kwanza na ametuandikia hapa jarida limetupa vipaumbele na hivi vipaumbele nina imani kavitoa katika Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi, naamini kama akivisimamia kama alivyoandika mwaka kesho hapa bajeti yake haitokuwa na maswali mengi lakini kama havitakwenda kama alivyoandika basi na yeye kidogo awe amejipanga mwakani atumie nguvu kuipitisha bajeti yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza wiki iliyopita alituletea watalaam wetu hapa wa wilaya na mikoa na wakandarasi wote. Tulipita kwenye mabanda kama mlivyokuwa mmeelekeza tuliwakuta mameneja wetu wa wilaya na mikoa na wakandarasi na nikushukuru kwa sababu kwa sisi wengine jimbo letu ni mbali sana na kufika Makao Makuu ya Wilaya, Meneja wangu Grace nilimkuta hapa na nikaongea nae na wakandarasi nikaongea nao, wakanipa ushikiriano mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo siku ile mlivyotuletea hapa nilijikuta tuna maswali mengi. Wakati tupo site hawajaja hapa tulikuwa tunajua kuna changamoto ya upandaji wa bei ya vifaa vya ujenzi, lakini hapa tena tukaja kukuta mkandarasi mwenyewe na aliyempa ajira yule yaani REA hawaelewani, lakini niliweza kusaidiwa na Mheshimiwa Naibu Waziri ndugu yangu Mheshimiwa Byabato, alimwita mkandarasi na REA wenyewe wakaitwa kuzibaini zile changamoto baina yao za kimkataba, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri alitoa maelekezo pale wakakae kikao, alisema jioni wakae kikao, lakini mpaka leo kikao hakijafanyika na mgomo upo palepale, mkandarasi ameshindwa kuelewa kwa sababu REA anampa maelekezo ambayo yapo nje ya mkataba wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe hata ile niliyokuwa nawaambia wananchi tusubiri wanasema wana- bargain bei za vifaa kumbe nilikuwa nawadanganya kumbe ni tatizo la mkandarasi na REA hawajaelewana ndiyo maana kazi imesimama jimboni kwangu. Hata hivyo, nikumbushe mwaka jana 2021 Mheshimiwa Naibu Waziri alifika jimboni kwangu waliahidi Kijiji cha Izumba watawasha umeme baada ya mwezi mmoja, lakini sasa hivi mwaka mmoja na miezi miwili hawajawasha umeme. Nilivyokuja kufuatilia kwa mkandarasi, kuja kumhoji hicho, akaniahidi mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi Julai, maeneo ya Songambele, Izumba yatakuwa yamewaka umeme, lakini kwa mgogoro huu kama tusipoutatua mapema mpaka muda huo umeme utakuwa haujawaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri kwa kuwa alituletea wataalam wenyewe, yale maswali yote yaliyoibuka, akae na wataalam wake, wakusanye maoni yote ya Wabunge ambayo tuliyaongea pale wakayafanyie kazi kuliko sasa, walituambia saa kumi watakaa kikao, leo tunaenda siku ya tano au ya sita hawajakaa kikao. Sasa ndiyo Waziri ajue ana watu gani ambao anafanya nao kazi kwa sababu yeye ameingia mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kampuni inaitwa JV POMY walimpa kazi ya kuunganisha umeme, amechukua hela za wananchi wangu, ameondoka LUKU hataki kuwaletea, wakimpigia simu sababu ni nyingi. Niombe kwa sababu zipo LUKU zaidi ya 120, tutoe kauli nini kilicho nyuma ya pazia juu ya mkandarasi huyu je, ni uzembe wake au kuna tatizo gani ambalo limemkumba? Kama kuna tatizo, basi wananchi wapewe taarifa kuliko sasa hela zao zimekaa kule halafu hawajui lini wataunganishiwa umeme. Nimwombe Mheshimiwa Waziri atusaidie hili hii Kampuni ya JV POMY ndio ilitusababishia hata hasara kwa ndugu yangu jirani yangu Mheshimiwa Kakunda, eneo la Makibo umeme umechelewa sana kwa sababu ya uzembe tu na ucheleweshaji mdogomdogo ulionao hii kampuni. Nimwombe Waziri aipitie vizuri, ikiwezekana wampunguzie kazi sehemu nyingine kwanza kumwezesha kumaliza kazi za mwanzo ili kuondoa kelele na lawama kwa Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nichangie, nilishamlilia Mheshimiwa Waziri na nikamwambia hatujapinga maelekezo ya Serikali kupandisha gharama za umeme, tumemuunga mkono, lakini tunacholia maelekezo ambayo aliyoyaleta walisema vijiji vitaendelea kuwa Sh.27,000 lakini maeneo ya miji itakuwa Sh.320,000 na kwingineko, lakini kwangu kuna vijiji vimeingizwa kwenye Sh.320,000 havina sifa ya kuingizwa huko kikiwemo Kijiji cha Goweko, Kijiji cha Igalula, Kijiji cha Kigwa na Nsololo Tambukareli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atoe kauli moja, wananchi wana hamu ya kuunganishiwa umeme na wao kama wangewaletea wakati ule wangeunganisha mapema, tatizo Serikali yetu ilikuwa inaleta kidogo kidogo, sasa wakati Serikali imefungua kupeleka umeme kwenye vitongoji, leo wanawapandishia bei wanaenda kumuunganishia nani, lakini tunakumbuka bei haikuwa hiyo ilikuwa Sh.170,000 basi wangerudisha hata ile Sh.170,000 kuliko sasa hivi imepanda, ukinunua nguzo moja unalipa mpaka zaidi ya 1,700,000 mpaka 2,000,000, kwa Mtanzania gani na uchumi gani? Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri aweze kutusaidia jambo hilo ili tuweze kulitatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Igalula lina vijiji 46 havina umeme, lakini juzi Mheshimiwa Waziri alitoa takwimu tatizo ambalo saa hivi wanaenda kulitatua kusafirisha umeme kwa umbali mrefu, ninavyoona kuna umeme nautoa Igunga unakuja jimboni kwangu kwenye Kata ya Loya, umeme ule umekuwa na changamoto sana, unakuja mdogo, wananchi hawafanyi kazi, mashine moja ikiwaka mashine zingine zote haziwaki na wananchi hawapati huduma nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe katika utekelezaji wa miradi, tulikuwa tunaomba muweze kujenga Kituo cha Kupozea Umeme hasa katika Kata ya Kigwa, itatusaidia sana kwa sababu vile vijiji 46 kama umeme kweli tukiuchukulia katika Kata ya Kigwa kama walivyo-plan sasa hivi, basi katika vile vijiji vyote kutakuwa kuna tatizo kubwa la umeme kwa sababu umeme unasafiri zaidi ya kilometa 200, kilometa 300 na huko ulipotoka zaidi ya kilometa 800 au 900 sasa unauongozea 200, huku kwenyewe bado unatusumbua unakatikakatika, unapoenda kuuongezea tena 200 zaidi, utaendelea kuwa na matatizo badala ya kwenda kutatua tatizo ndiyo tunaenda kuongeza kelele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wafanye tathimini waweze kuongeza Vituo vya Kupozea Umeme, pale Kigwa tutampa eneo nadhani tuna maeneo makubwa ili waweze kujenga kituo chao cha kupozea umeme na baadaye twende tukausambaze katika maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine linaloendelea sasa hivi, tumekuwa na plan za muda mfupi, sasa hivi wakandarasi wapo site, tunapitisha nguzo za miti kwenye majaluba, anajua kabisa hili ni jaluba, lakini saa hizi watalaam wa REA wapo, TANESCO wapo, mkandarasi yupo, umeme unapitishwa kwenye jaluba, baadaye masika inakuja nguzo zinakuwa kwenye maji zinaanguka, halafu baadaye wanasema tunaomba fedha za maintenance, kwa nini wasitengeneze mapema nguzo za zege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri waangalie maeneo yote ambayo yana matatizo ya kujaa maji, basi tuanze kugundua mapema wakandarasi wapo kule kama hawayajui hayo maeneo, Viongozi wa Vijiji wapo, Viongozi wa Dini wapo, wawashirikishe watawaambia hapa maji yanajaa wakati gani, hapa maji hayajai. Kama ile route imelazimika ipite palepale, waweke nguzo za zege ili kuweza kusaidia wananchi wetu. Kwa hiyo, kwa mwaka huu yangu ni hayo machache kwa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kama ushauri, niipongeze Serikali wanaendelea na harakati nzuri za ujenzi wa bomba la mafuta, lakini tulishauri bei ya mafuta inaongezeka hasa Mikoa ya Kagera, Kigoma kule kwa sababu bei ya Dare es Salaam unakuta shilingi 3,100 lakini Kigoma ukienda shilingi 3,600 au shilingi 3,700, lakini wakija kuuliza kwa nini tunatofautiana na Dar es Salaam kitu ambacho kinachosababisha ni kwa sababu kule ni mbali depot zipo Dar es Salaam, tunaongeza cost za transport.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri tulishauri kwenye Kamati, lakini tuendelee kushauri kama sisi wawakilishi wa wananchi, katika Mradi wa Bomba la Mafuta kwa kuwa tumeliunganisha kutoka Uganda mpaka Tanga, palepale tujenge bomba letu lingine tena ambalo litarudisha mafuta mengine ambayo yatasaidia Mikoa hiyo ya Kanda ya Ziwa. Leo meli ikipaki Tanga tuweze kufungua mafuta Tanga tukaweka depot pale Nzega au Bukene, yakaweza kuja magari ya Mwanza yakawa yanachukua pale, magari ya Kigoma yakawa yanachukua pale tutasaidia sana kupunguza bei, lakini vile vile tutasaidia kupunguza mlundikano wa magari kwenda Dar es Salaam. Kwa hiyo, tukiweka vituo vyetu vya Serikali na bomba likawa la Serikali, gharama itakuwa ni cheap ingawa tutaweka tozo kidogo. Kwa sasa hivi kwenda Mwanza ni zaidi ya Sh.150 hadi Sh.170, lakini ukiweka pale kutoka Mwanza kuja Bukene wakachukua mafuta pale watachukua kwa Sh.50 ile nyingine itakuwa cost ambayo tumemsaidia mwananchi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kauli kwa kusema naunga mkono hoja kwa sababu mabanda yalikuja, majibu mengi niliyapata. Ahsante sana. (Makofi)