Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye hotuba hii ya Nishati. Kwanza kabisa nami niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyoweza kufanya kazi iliyo bora na iliyotukuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa sababu ametupunguzia maswali mengi na ametufanya tuelewe vitu vingi kwa wakati mmoja. Kile kitendo alichokifanya cha yeye kuwaleta wataalam hapa, pamoja na Mameneja wa Wilaya zote, maana yake ni kwamba pale ametupunguzia muda wa kwenda kuwafikia hawa watu wote, lakini pia naamini wazi kuwa imepunguza maswali mengi na hata vilevile michango haitakuwa mingi sana kutokana na jambo lile alilolifanya. Kwa hiyo, ni pongezi kubwa kwake na natamani hata Wizara nyingine zingefanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja niende kwenye mchango wangu, kwenye Jimbo langu ama Wilaya ya Tunduru. Wilaya ya Tunduru tunapokea msongo wa umeme wa kilovoti 33 kutokea Songea Mjini na umeme ule unasafiri kwa kilomita 260. Kama unasafiri kwa kilomita 260 maana yake ni kwamba huku njiani kote umeme huo unatumika na tunautumia kwa Wilaya mbili, kwa maana ya Wilaya ya Namtumbo na Wilaya ya Tunduru. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inapotokea hitilafu Namtumbo maana yake ni kwamba Namtumbo wanakosa umeme na sisi Tunduru tunakosa umeme pia vilevile. Kwa hiyo, jambo hili limepelekea umeme wa Tunduru kukatikakatika mara nyingi sana na tunapata adha kubwa mno. Ulifikia wakati kwa siku umeme unakatika mara 12 mpaka mara 17. Wakati mwingine unaweza ukakatika siku nzima umeme usipatikane. Wakati mwingine tunalala na giza usiku kucha. Lakini ukiuliza ni kwamba unakuta hitilafu imetokea Namtumbo, kwa hiyo, mpaka wenzetu wa Namtumbo washughulikie hitilafu hiyo ya umeme ndipo na sisi Tunduru tuweze kupata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya adha hiyo kubwa, tarehe 4 Septemba mwaka jana niliweza kuuliza swali la msingi hapa ambalo Wizara kama inaweza kutujengea substation ya kilowati 132 pale Tunduru. Kwa bahati nzuri Mheshimiwa Naibu Waziri wa Wizara hii aliweza kujibu kwamba watatuletea ama watatujengea mradi huo wa kilowati 132 pale Tunduru na alisema ataingiza kwenye mpango huu ili sasa Tunduru tuweze kupata hiyo substation na tuondokane na tatizo hili la kukatikakatika kwa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa nimepitia mpango huu mara mbili, mara tatu, sijaona kabisa hilo jambo kama limeingizwa kwenye huu mpango. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa, anipe commitment ama aseme na wananchi wangu wa Tunduru kule wasikie kama ni kweli huu mradi upo ama haupo, kwa sababu tuliambiwa utaingizwa kwenye huu mradi lakini sijaona kama umeingizwa kwenye huu mradi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa aniambie ni kweli huu mradi utatekelezwa kwa kipindi hiki? Kama utatekelezwa je, ni lini utaanza huu mradi? Naomba pia utakapotekelezwa huu mradi ama utakapoanza kujengwa huu mradi, niombe sana utakapokuwa unatoka Songea kuja pale Tunduru Mjini, basi zijengwe njia tatu za usambazaji. Njia ya kwanza irudi Hulia, njia ya pili iende Nanyumbu Masasi na njia ya tatu itumike palepale Tunduru Mjini. Hapo Waziri atakuwa ametusaidia sana na tatizo hili litaenda kwisha kabisa na Mheshimiwa Waziri tutampongeza mno na tutamwombea aendelee kudumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kutokana na ukubwa wa Wilaya ya Tunduru ilivyo, tunahitaji angalau tupate sub office nne ambazo hizi zinaweza kufanya kazi kwa urahisi, kuwafikia wadau wa umeme kwa urahisi kutokana na eneo lenyewe namna lilivyokuwa kubwa. Kwa hiyo, sub office hizi zipatikane nne ambazo zitakuwa na ikama za kiofisi zilizokamilika. Sub office moja ijengwe Milonde, ya pili iwe Nakapanya sub office na ya tatu iwe Nalasi sub office na ya nne iwe Lukumbule sub office. Kwa kufanya hivyo maana yake ni kwamba tutakwenda kusaidia kwa haraka matatizo haya ya umeme kwisha katika Wilaya ya Tunduru kutokana na kwamba jiografia ya Tunduru ni kubwa mno. Kwa kutumia ofisi moja tu na wana gari moja tu, kukitokea changamoto tatu kwa siku moja maana yake ni kwamba wanawafikia wananchi kwa ugumu mno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne, nataka nishauri kwamba hizi transfoma zinazojengwa kwenye vijiji lazima tuziangalie kwa umakini ama tuangalie namna ya kufanya, kwa sababu zile transfoma zinazidiwa haraka sana na wateja wa umeme kwa sababu zina KVA 50. Kwa hiyo, kama zina KVA 50 maana yake ni kwamba kama zina wateja wengi inazidiwa kwa haraka na kunatokea tatizo tena la kukatika kwa umeme. Kwa hiyo, nashauri badala ya kufunga transfoma za KV 50 basi zifungwe transfoma za KV 100 na kama siyo hivyo basi kwenye kijiji kimoja zifungwe transfoma mbili, tatu na kuendelea kulingana na ukubwa wa kijiji chenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)