Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na uzima. Nishukuru pia kwa kupata nafasi ya kuchangia kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zake za makusudi kabisa kuwa na utashi wa kupunguza ukali ya bei ya mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa January Makamba - Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Wakili Msomi Byabato - Naibu Waziri wa Nishati pamoja na watalaam wote wakiongozwa na Katibu Mkuu kwa kazi nzuri mnayoifanya ili kuhakikisha wananchi wanapata umeme. Chapa kazi msigeuke nyuma mkawa mlima wa chumvi, songa mbele na Mungu atawasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirejee kwenye hotuba ya bajeti iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri na kuchangia kwenye vipengele vifuatavyo; kwanza katika hotuba yake ya bajeti Mheshimiwa Waziri ameeleza kuwa gesi asilia sasa itapelekwa nchini Uganda. Niishauri Serikali ihakikishe mikoa ambayo gesi hii inapitia wapate huduma hii ya gesi asilia majumbani kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida yake kwanza itafanya wananchi kujiona ni sehemu ya mradi na kuwa walinzi wa bomba hilo lisihujumiwe na itapunguza gharama za matumizi ya umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu migodi kuunganishwa kwenye gridi ya umeme ya Taifa, migodi hii inatumia umeme mwingi hivyo ni chanzo cha mapato kwa TANESCO. Pia exemption kwenye mafuta Serikali inapoteza fedha nyingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu matumizi ya gesi asilia kwenye magari na Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini ya Wizara kutumia gesi asilia, niombe na kushauri litolewe tamko kwa magari yote ya Serikali na Taasisi zote magari yake yatumie gesi ili kubana matumizi ya Serikali kwa kipindi hiki ambacho mafuta yamepanda bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tungehamasisha matumizi ya gesi asilia kwa wananchi wote, lakini hapa kikwazo ni gharama ya ubadilishaji wa mfumo wa gari kwenda kwenye gesi. Kiasi cha shilingi milioni mbili ni kikubwa mno. Ushauri wangu uangaliwe uwezekano wa kupunguza gharama lakini pia viwekwe vituo vya kutosha vya ubadilishaji mifuko ya magari, kwa kuanzia kila Wilaya ili huduma ipatikane kirahisi wananchi waweze kutumia gesi kwenye magari yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipongeze Shirika letu la TANESCO kwa jinsi linavyobadilika kwa haraka sana. Kwa mimi niliyefanyakazi Wizara ya Nishati ukilinganisha miaka hiyo ya 1990 na sasa ni vitu viwili tofauti kabisa kazi imefanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha Shirika kuanzisha Nikonekt App ambayo itarahisisha huduma za kufungiwa umeme kwa Dar es Salaam, Pwani na sasa imezinduliwa Kanda ya Kati na Kanda ya Kaskazini. Hii itaondoa ukiritimba na wateja kupoteza muda ambao ungetumika kufanya shughuli zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa watumishi; watumishi wengi wanafanya kazi kwa mikataba kwa muda mrefu na kwa weledi na uadilifu. Shida na changamoto iliyopo wanapotangaza kazi, hawa hawapewi kipaumbele, wanaajiriwa wapya, matokeo yake na mikataba yao inavunjwa, wanakuwa mitaani, baada ya muda wanafuatwa tena wafanye kama vibarua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili tunapoteza watumishi wenye uzoefu na waliolitumikia shirika kwa uaminifu. Pia tunavunja sheria ya kibarua ambaye hutakiwa kufanya kazi kwa muda wa miezi mitatu. Nikuombe Mheshimiwa Waziri wasaidie hawa watumishi waliolitumikia shirika kwa muda mrefu, wale wenye sifa wapewe ajira za kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.