Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nashukuru kwakupata nafasi ya angalau kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati nikiwa ni msaidizi wake, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutubariki na kutupa nafasi ya kukutana tena na kuleta zawadi nyingine ya Mama kama ambavyo amekuwa akisema Mheshimiwa Mwijage kutoka katika Wizara ya Nishati kama ambavyo imeanza kutolewa tangu jana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwa sababu ya muda nitakimbia kimbia ili nimuachie Mheshimiwa Waziri nafasi pana zaidi ya kuweza kueleza mambo makubwa zaidi ya kisera ambayo yamechangiwa na Waheshimiwa Wabunge katika nyanja mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Moja, kwa kuendelea kuwa na imani na mimi na kunibakiza nitumie neno hil,o katika Wizara hii ya Nishati nikiendelea kumsaidia Mheshimiwa Waziri majukumu lakini na kumsaidia yeye pia, lakini cha muhimu zaidi mimi nimshukuru kwa sababu yeye ndiyo anayefanya kila kitu katika Wizara yetu ya Nishati nasi tunaleta ujumbe ambao anatupatia yeye. Haya mambo yote ambayo mmeyasema hapa sisi tunayofaraja kwamba Mheshimiwa Rais ametuamini na kuturuhusu tuje kuyasema kwenu na kupokea maoni yenu na tunawahakikishieni kwamba hatutawaangusha ninyi wala hatutamuangusha Mheshimiwa Rais katika utekelezaji wa yale yote ambayo tumekubaliana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya muda mimi niseme maeneo kama matano lakini kwa haraka haraka. Kwanza yametolewa maoni na maswali mengi ya msingi kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge katika maeneo mbalimbali, kwa niaba ya Serikali niseme mambo kadhaa ambayo yamesemwa yapo wazi kabisa na tunayachukua tunayafanyia kazi mengine yanahitaji mjadala mpana zaidi, tutauleta hapa ili uweze kufanyiwa kazi lakini kwa sababu ya muda sasa angalau nitaje machache ambayo moja kwa moja Serikali imeyachukua na tunaahidi kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la mafuta kwa haraka haraka nikuboresha miundombinu ya kupokea mafuta pale Bandari ya Dar es Salaam na bandari nyingine na kama tulivyosema na ambavyo mmesema nyie zipo gharama ambazo zinaongezeka katika bei zetu za mafuta kwasababu ya miundombinu yetu ya kupokea mafuta kutokuwa mizuri limesemwa na Waheshimiwa Wabunge wengi na tunalichukua na litaanza kufanyiwa kazi mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kujenga single receiving terminal, Mheshimiwa Waziri mara kadhaa ameeleza jitihada ambazo Wizara inazifanya jinsi ambavyo tumewatafuta wadau mbalimbali ili hilo jambo liweze kufanyika na itatusaidia sisi kuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuweza kufanya biashara ya mafuta katika hali ambayo inatuwezesha kuwa na ushindani mzuri. Wameshauri kwamba katika muda huu ambao tunajiandaa sasa tunakamilisha taratibu za kujenga single receiving terminal basi matenki yetu ambayo yapo pale tipper ambayo sisi tunayamiliki kwa sehemu kubwa basi yaweze kutumika kufanya kazi hiyo. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba hilo nalo limechukuliwa na tayari Serikali imeshaanza kulifanyia kazi na katika muda mfupi ujao mafuta yataanza kushushwa pale tipper.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wameshauri pia TBS iache kuwa inazunguka na sampuli za mafuta kutoka maeneo mbalimbali na kwenda kwenye maabara moja zitengenezwe maabara kila eneo ambapo mafuta yanashushwa na hilo limechukuliwa na katika muda mfupi litafanyiwa kazi na wanaotoka maeneo hayo ni mashahidi watakuja kuwaambieni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Waheshimiwa Wabunge wameshauri zitengenezwe kanuni za kuwezesha biashara ya mafuta katika vijiji vyetu kuwa rafiki zaidi. Niseme kwanza mwaka 2020 zilishatengenezwa kanuni za kuweka mazingira rafiki katika maeneo ya miji na vijiji kufanya biashara za mafuta lakini hiyo kama haitoshi Serikali tayari imeanza kupitia upya kanuni hizo ili kuona namna ambavyo inaweza ikashusha zaidi zile gharama za wale watu wanaweka katika vituo maeneo ya vijijini na katika muda mfupi tutaona matokeo yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pamoja na Waheshimiwa Wabunge wameshauri kwamba mfumo wetu wa BPS au mfumo mwingine wowote utakaotumika katika kuagiza mafuta uzingatie kuhakikisha kwamba mafuta yanayokuja ni safi ni salama na uhakika wa kupatikana kwa mafuta hayo. Nasi tunawahakikishieni Waheshimiwa Wabunge kwamba wakati wote ambapo tunatafuta njia nzuri zaidi ya pamoja ya kuwezesha gharama za mafuta kushuka lakini tunahakikisha tunazingatia uhakika wa upatikanaji wa mafuta katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine uliotolewa ni kuweka mazingira mazuri ya kuhakikisha wale wanaoleta mafuta wanaochezea chezea taratibu zetu hizi wakaleta katika compartment yao unakuta mtu ana Meli na compartment tatu, compartment moja ina mafuta machafu nyingine mbili zinakubalika tuwashughulikie sawasawa ili kuepusha kutuchezea chezea na kututania mara kwa mara. Nami kwa niaba ya Serikali niwaahidi tutaendelea kushughulika nao kwelikweli ili waendelee kupata adabu na kutotuchezea chezea kwa sababu sisi ni hub ya wengine wanaotutazama kutoka huko nyuma yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeshauriwa kuhakikisha kwamba tunafanyia kazi chanzo cha umeme cha cha jotoardhi (geotherm) kwa kuhakikisha kwamba sheria ile tunairekebisha ili iweze sasa kukidhi matakwa ya kuwa chini ya Wizara ya Nishati na kuiwezesha pia Wizara yenyewe kuwa ndiyo msimamizi sasa mkubwa wa TPDC na kuipa kipaumbele TPDC kwa ajili ya kuweza kuleta mabadiliko katika eneo la nishati ya joto ardhi kama wenzetu Wakenya walivyofanya. Tuwahakikishieni kwamba hilo tumelichukua na kwenye bajeti hii pesa imetengwa zaidi ya Bilioni Ishirini kwa kuendelea kuiwezesha TPDC kufanya kazi zake katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni maeneo ambayo kwa uchache kabisa yapo mengi sana nimeona niyagusie na mengine Mheshimiwa Waziri atakuja kuyamalizia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa ufupi niende kwenye maeneo mengine mawili. Eneo ambalo kila Mheshimiwa kila aliposimama ameligusia eneo la umeme vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafurahi kwanza kwa Mheshimiwa Rais kuendelea kui-support sekta ya nishati kwa kupeleka umeme vijijini bila kupepesa macho bila kupepesa kope, katika hili Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amepambana kwelikweli. Ni uwazi usiopingika kwamba kwa sehemu kubwa sana umeme vijijini siyo biashara umeme vijijini ni huduma kwa sehemu kubwa sana. Kwa sababu umeme ule unaounganishwa tunazifahamu familia zetu za vijijini, kwa sehemu kubwa mtu anaweka umeme wa Shilingi 9,150 unit 75 anakaa nazo miezi mitatu, miezi sita siyo biashara. Pamoja na hilo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza pelekeni umeme kwenye vijiji, pelekeni umeme kwenye vitongoji na gharama ibakie kuwa Shilingi 27,000. Katika hili Wizara ya Nishati tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, Trilioni Moja na Bilioni Mia Mbili na Hamsini zipo zinaendelea kupelekwa katika maeneo yetu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba miradi ya REA inakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwenye eneo jingine tulisaini mikataba mingi kwa ajili ya kupeleka umeme vijijini, mikataba ile mingi ilikuwa inadondokea Desemba mwaka 2022, mingine ilikuwa ina overlap Desemba, 22 kwa sababu mkataba unamiezi 18. Sasa tuwahakikishieni kwamba wale ambao walitakiwa kukamilisha mikataba mwezi Desemba ambao walianza mapema, tutapambana nao na kuhakikisha kwamba kipindi hicho kikifika mikataba inakamilika. Wale ambao mikataba yao ilikuwa ina-overlap basi tutakubali kuhakikisha kwamba muda ule wa mkataba unafikiwa lakini endapo kutatokea kuongezeka kwa muda wa kukamilisha mkataba yapo mambo kadhaa ambayo yatasababisha kuongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo yapo mawili chanya na mengine ni hasi, jambo la kwanza sisi wenyewe Waheshimiwa Wabunge tunapenda maeneo tunayopeleka umeme yaongezeke, sasa unapoongeza scope ya kazi siyo rahisi kumbana mtu afanye kazi katika muda uleule mliokuwa mmekubaliana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo jingine ni kuongeza wigo sasa si kazi ya awali lakini Mheshimiwa Waziri tayari ameshatoa ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kuongeza kilometa mbili kwenye maeneo yetu ya vijiji sasa inapoongezwa kilometa mbili si rahisi sasa ukamilishe ndani ya uleule muda uliokuwepo wa awali. Changamoto hasi ambazo tumezipata cha kwanza ni kupanda kwa gharama za vifaa, ni uwazi usiopingika gharama zimepanda lakini tunahakikisha kwamba jambo hili tunalifanyia kazi lakini pia tumebadilisha kutoka kwenye goods kuja kwenye works. Nisema kidogo hapa huko nyuma tulikuwa tunafanya mikataba ya upelekaji wa umeme vijijini kwa kutumia taratibu zinazoitwa goods ambapo mnampa Mkandarasi fedha ya kununua vifaa vyote asilimia karibia 80 ya mkataba ananunua vifaa anavitunza halafu ile asilimia 20 anaanza kufanyia kazi. Tuliona mtu anaponunua vifaa akapata faida yake anaingia mitini, sasa tukabadilisha utaratibu twende na works kwamba tutakulipa fedha kidogo advance payment asilimia 20 utanunua vifaa kidogo na pesa ya mobilization halafu sasa ukifanyakazi tukaja tukakagua tunakulipa. Sasa kwenye hiyo habari yakuja kukukagua tukakulipa ili ukanunue vifaa vingine tumekutana na habari ya kupanda kwa bei lakini tunahakikisha kwamba tunashughulika nalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya nini katika eneo hili, hatua za utekelezaji tumeshazisema mara kadhaa, jambo la kwanza ambalo tumelifanya. Tumewaleta Wakandarasi wote chini ya usimamizi wa Mheshimiwa Waziri January Makamba hapa Bungeni, wamekaa hapa siku tatu, Waheshimiwa Wabunge wameenda wamewaona, wamewahoji wamejua shida iko wapi na tunatatua vipi katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo tumelifanya ni kuongeza usimamizi. Mheshimiwa Waziri ameshasema, tunao wasimamizi ngazi ya Kanda, tunao wasimamizi ngazi za Mikoa lakini sasa wanakuja wasimamizi ngazi za Jimbo, waje wasimamizi wa miradi yetu ya REA kwenye Majimbo yetu. Ukiamka unaamka naye ukilala unalala naye na hiyo ni zawadi nyingine ya Mama ambayo Mheshimiwa Waziri ametuambia, nia ni kuhakikisha kwamba tunafikia sehemu ambapo mradi hautakwama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la tatu na la mwisho katika eneo hili; tumekaa na wakandarasi, tumejadiliana nao, tumekubaliana kwamba jambo hili sasa liishe, waendelee na kazi wakati sisi tunaendelea na mchakato wa kurekebisha mikataba yao na kuwawekea katika mazingira mazuri. Tunaahidi kwamba mikataba hii itakamilika, tutaisimamia vizuri kabisa na itakuwa ni ya tija kwa Watanzania wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vitongoji tayari zawadi nyingine ya Mama imeshasemwa, tuko katika taratibu za kutafuta shilingi trilioni 6.5 kwa ajili ya kuhakikisha vitongoji vile vyote zaidi ya 30,000 vinapelekewa umeme kwa pamoja katika muda mfupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda niende kwenye eneo lingine la mwisho la TANESCO; kila Mbunge aliyesimama amezungumzia kukatika kwa umeme. Wanasema mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Katika eneo hili hali siyo mbaya kama ilivyokuwa siku chache zilizopita, tulisimama Bungeni, tukakiri tatizo na upungufu lakini tukawaambieni njia za kuchukua na mimi nilikuwa mmojawapo niliyeahidi kwamba TANESCO hatuajiri mtu kwa ajili ya kukatakata umeme na kweli inaonekana wazi kwamba umeme haukatwi bila sababu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini umeme unakatika? Iko miundombinu ambayo ni chakavu inatuletea shida; kuna mambo ya asili yanatokea, radi, mvua, tingatinga na mambo kama hayo; kuna miundombinu kuzidiwa na umeme, transfoma tuliifunga, tulikuwa tuna watu 25 watu wameongezeka wamekuwa 50/70 hatujaibadilisha, tunakuwa na tatizo. Tumefanya nini katika eneo hili? Mheshimiwa Rais ametupa zawadi nyingine ya shilingi bilioni 500 ambayo itakuja kumaliza changamoto zote hizi katika maeneo yetu, zitapelekwa kujenga vituo vya kupoza umeme, zitapelekwa kujenga njia za kupeleka umeme, zitapelekwa kubadilisha transfoma na kuwekwa kubwa, zitapelekwa kutengeneza miundombinu mipya, tunakoelekea habari ya kukatikakatika kwa umeme itakuwa ni historia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachomshukuru Mwenyezi Mungu wakati mabadiliko haya mazuri yanakuja na zawadi za Mama zinakuja, niko hapa tayari kutumika kuendelea kuhakikisha kwamba watanzania wanapata kile walichokistahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda ninaomba niishie hapo, nashukuru sana ushirikiano ambao Waheshimiwa Wabunge wanatupatia na mimi binafsi niwaahidi nitaendelea kutumika na baada ya Bunge hili mtatuona sana majimboni tukiwa tunahakikisha tunafuatilia yale tuliyoyaahidi na kuyafanyia kazi kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)