Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Aloyce Andrew Kwezi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba nichukue nafasi hii kwanza kukushukuru kunipatia nafasi ili niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara yetu ya Maliasili na Utalii. Lakini awali ya yote nianze kwa kuwapongeza sana Wizara hii kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea nayo. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Wakurugenzi wote wa taasisi zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naanza kwa kuwashukuru kwa sababu Kaliua ni miongoni mwa maeneo ambayo yamepakana na Hifadhi kubwa mbili, kwanza tuna Ugara National Park, lakini pia tunayo Kigosi, lakini tuna TFS na tuna TAWA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ile timu ya Mawaziri nane ilipita katika Wilaya yetu ya Kaliua na tumenufaika kwa sababu sehemu kubwa ya changamoto imeweza kutupunguzia. Wilaya yetu takribani vijiji 26 vilikuwa kwenye hifadhi, lakini kwa kazi nzuri iliyofanywa na timu hiyo, sasa wananchi wale wako huru na tunajipanga kwenda kwenye matumizi bora ya ardhi katika vijiji vyetu. (Makofi)

Mimi nina machache ambayo ningeweza kuyashauri, kwanza kwenye Hifadhi ya Ugara; Hifadhi ya Ugara ni Hifadhi mpya, lakini hifadhi hiyo mpya mimi nimekwenda kutembea na timu mbalimbali ya uongozi wetu wote wa wilaya tumekuta hifadhi ile ni nzuri sana na inavivutio vizuri sana. Mimi nilikuwa napenda niishauri Wizara kuwekeza nguvu nyingi kwenye ukarabati wa miundombinu na miundombinu ambayo tunaomba kwa Hifadhi ya Ugara ni barabara nzuri ifike Ugara National Park, lakini miundombinu ya mawasiliano, miundombinu ya internet na miundombinu ya hoteli na camps mbalimbali. Nalisema hili sio kwa maana ya Ugara peke yake, lakini ukienda Kigosi miundombinu ya kuingia Kigosi ni shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado ukienda Katavi miundombinu ya kuingia Katavi ni shida, ukienda Biharamulo pale Burigi Chato hiyo yote miundombinu ni shida. Lakini ukiangalia ukanda wote ambao nimeutaja unaweza ukafanya vizuri kama inavyofanya vizuri ukanda wa Kaskazini, lakini tunaendelea kuangalia tukiwekeza fedha nyingi ukanda ule wote umepakana na nchi mbalimbali, Uganda jirani zetu, Congo jirani zetu, Burundi jirani zetu. Sasa nchi hizi zote zingeweza kutuletea tija kwa sababu vivutio tulivyonavyo huko ni vizuri na tukivihamasisha vizuri tukavitangaza vizuri nina uhakika ule ukanda wote utafunguka vizuri sana. Kwa sababu unakuta kutoka Burundi mpaka unaingia Hifadhi kilometa 30, sasa kwa nini hatujatangaza kwa kiwango ambacho ni kizuri na kiwango kikubwa zaidi? Nilikuwa nashauri miundombinu ile kwenye hifadhi zote ambazo nimetaja iboreshwe na twende kwa kasi zaidi kama Mheshimiwa Rais anavyotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine nilikuwa naliomba ni kwenye marekebisho ya mipaka, ni kweli tumepita, vijiji viko huru, lakini baadhi ya maeneo bado urekebishaji wa mipaka bado migogoro haijaisha. Kwa mfano, Igagala Namba Nne hicho ni kijiji, Ugansa bado, Usinge bado, Luganjo Mtoni bado, Kombe bado; nilikuwa naomba maeneo haya wayape kipaumbele, ili kuhakikisha sasa wananchi tunaishi kwa furaha kwa amani tukiendelea kulinda hifadhi zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Tabora ni miongoni mwa mikoa ambayo inazalisha asali na uzalishaji mkubwa umepakana na hizo hifadhi. Sasa nilikuwa nawashauri kwanza naomba tupewe muda kwa sababu kuna eneo ambalo limeongezeka la TFS likaenda Ugara sisi kule kuna mizinga. Tunaomba tupatiwe angalau miezi miwili wale wananchi wavune na waweze kutoa mizinga yao, hilo ndilo ombi ambalo ningependa mliangalie kwa ukanda mzima wa Urambo, ukanda mzima wa Kaliua na ukanda mzima wa kuelekea njia ya Ushetu pote humo ni wafugaji wa nyuki. (Makofi)

Ushauri wangu mwingine ni kuhusiana na utalii wa ndani; Mheshimiwa Rais ametusaidia kwenye Royal Tour kwa maana ya kutusaidia kufungua huko, lakini tunapopata janga sisi wa ndani tunakwama kwa sababu miradi mikubwa inategemea wafadhili. Ni kwa nini sisi tusijenge utamaduni wa kuhamasisha utalii wa ndani tukajengeka kifikra kuwa tayari kutembelea hifadhi zetu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nashauri utalii wa ndani tuupe hamasa kubwa sana na mimi niwaombe Wizara watoe nguvu pale Kaliua ile hifadhi ukifika kule kwa kweli, kuna kivutio kikubwa, nilimuona Mr. Shelutete alikuja kama mara mbili, lakini nilipokuja kuangalia sikuamini, ile ni Kaliua kweli? Kwa sababu, ilikuwa ni vivutio vizuri kweli kweli, sasa sasahivi wananchi wamehamasika, lakini miundombinu bado nis shida. Niombe zaidi tuweke hiyo miundombinu ili tuweze kufikika kwa hali ambayo ni nzuri na hali ambayo itatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nilikuwa nashauri pia kuhusiana na askari wa maliasili. Natambua kabisa na wenyewe wanapata changamoto wapo askari wanauawa kabisa, lakini nilichokuwa nashauri mimi hebu tuwape mafunzo askari wetu namna gani bora ya kukabiliana na wale ambao hasa zile vurugu za kawaida za mipakani kwa sababu nguvu ikitumika kubwa malalamiko yanakuwa ni makubwa sana. Nashauri tuboreshe mahusiano zaidi kwa maana ya kuwapa mafunzo ambayo sio lazima watumie silaha peke yake, lakini hata kuelimisha kwa maana ya kutujengea mahusiano mazuri na hifadhi zetu zitakuwa ni endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja, nimalizie; Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja Kaliua, Kaliua tulikamata magogo pale tukauza shilingi bilioni moja na nusu, Waziri Mkuu aliahidi kile kijijiā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30, malizia sentensi.

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, Kijiji cha Wachawaseme wapewe zahanati yao. Mkurugenzi wangu ameshaleta ile bill ya zahanati pale, mpaka leo tumepata shilingi bilioni moja na nusu, zahanati karibu shilingi milioni 70 bado hamjatuletea.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)