Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafinga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, naomba kuwapongeza kwa hotuba ya bajeti ambayo itafungua fursa zaidi. Hata hivyo nina ushauri na hoja kadhaa ambazo nisipopata majibu ya kuridhisha nitashika shilingi kwa nia njema ya kupata ufafanuzi.
Mheshimiwa Spika, kwanza ni Mradi wa REGROW; mradi huu ulizinduliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tarehe 12 Desemba, 2018 wakati huo akiwa Makamu wa Rais. Hata hivyo kumekuwa na kusuasua sana katika kutekeleza mradi huu ambao ni mkopo wa Benki ya Dunia wa kiasi cha dola milioni 150 za Kimarekani.
Mheshimiwa Spika, matarajio ya mradi huu pamoja na mambo mengine ni kuboresha mazingira ya shughuli za utalii ikiwa ni pamoja na ku-upgrade existing roads, airstrips lakini pia kujenga kituo kikubwa cha habari kwa maana ya information centre pale Kihesa, Kilolo. Aidha, mradi huu unatarajiwa kuboresha ushiriki wa wananchi wanaozunguka hifadhi ama kwa mafunzo ya uhifadhi au kwa kupata ajira ndani ya sekta.
Mheshimiwa Spika, mradi huu ambao narudia kusema kuwa utekelezaji wake ni wa mwendo wa kinyonga ungeweza kunufaisha kaya zaidi ya 20,000 na wakulima wanaozunguka Hifadhi ya Ruaha.
Mheshimiwa Spika, mradi huu kwa mujibu wa maelezo ulipaswa kwa mtiririko uwe umeanza na kukamilika mwaka 2024 ambapo ilipaswa mpaka kufikia mwaka huu wa 2022 kiasi cha fedha dola milioni 111 ziwe zimeshatumika kutekeleza hayo niliyoyataja hapo juu. Kwa mtiririko ilipaswa baada ya uzinduzi by 2020 kiasi cha dola milioni 41 kilipaswa kiwe kimetumika; by 2021 kiasi cha dola milioni 76 kiwe kimetumika; by 2022 kama nilivyosema kiasi cha dola milioni 111 kilipaswa kiwe kimetumika; by 2023 kiasi cha dola milioni 141 kilipaswa kiwe kimetumika; na by 2024 kiasi chote cha dola milioni 150 kiwe kimetumika, na hapa tuelewane hoja sio tu kutumika bali kutumika katika shughuli zilizopangwa kwa lengo la kuboresha mazingira ya utalii na ushiriki wa wananchi katika uhifadhi.
Mheshimiwa Spika, Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anafanya jitihada kubwa kufungua milango kwa kushiriki mikutano ya Kimataifa ikiwemo Royal Tour ambako anaitangaza nchi na utalii wetu, kwa kufanya hivi watalii watakuja, je, kama tumekuwa na mwendo wa kinyonga kutekeleza mradi wa REGROW hatuoni kuwa tunajikwamisha na kumkwamisha Mheshimiwa Rais?
Mheshimiwa Spika, pili, fedha hizi sio grant, ni mkopo ambao inafaa matunda yake yaanze kuonekana, lakini sasa tunajivuta, mara ilikuwa sijui GN kutoka ardhi ili kufidia na eneo, sijui muda wa mradi tumeongeza, for whose interest. Kwa hiyo, kama mtu ninayejali utalii kama sehemu ya kuongeza mapato ya Taifa na wananchi, jambo hili sio sahihi, ndio maana pasipo majibu ya kutekelezeka nitashika shilingi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu misitu; tunashukuru sana sekta imetulia sana, nawapongeza sana TFS kwa ushirikiano na pia kwa kupokea mawazo ya wadau. Nawashukuru pia kwa CSR, wanatupa support kubwa sana watu wa Mafinga na Mufindi, nawashukuru mno.
Mheshimiwa Spika, nina ushauri katika mambo mawili; kwanza ni kuhusu tozo; ninashauri baadhi ya tozo sasa umefika wakati tuziondoe, kwa mfano LMDA, tayari sasa maeneo mengi yamepandwa miti, tozo hii ambayo ililenga kuirudisha shambani kupanda miti, ni wakati sasa tukaiondoa sambamba na kuangalia suala la bei na tozo nyingine ili kusisimua biashara.
Pili, Kituo cha Panda Miti Kibiashara chini ya ufadhili wa Serikali ya Finland; sisi Halmashauri ya Mafinga Mji kwa kushirikiana na Seikali tunaomba tufanye jitihada za pamoja ili baada ya phase ya sasa kumalizika, Finland watusaidie kwa phase nyingine zaidi ili kuendana na muda wa uvunaji wa miti toka mradi ulipoanza. Hii itasaidia kufanya tathmini ya uhakika na kupima matokeo ya mradi umekuwa na msaada kwa kiasi gani katika Taifa na jamii. Hata hivyo ili jambo hili lifanikiwe ni muhimu sana sote kwa pamoja tukashirikiana kushawishi GRL kutuachia lile eneo na baadae mradi ukiwa umemalizika kwa ukamilifu kituo kirithiwe na Halmashauri ya Mafinga Mji.
Mheshimiwa Spika, CSR kwa makampuni; jambo hili ni la hiyari lakini makampuni makubwa yaliyowekeza katika maeneo yetu yanao wajibu wa kutoa CSR, kwa sababu sisi tumewapa maeneo lakini moto ukitokea wananchi wanashiriki kuuzima, ikiwa TFS kupitia Shamba la Sao Hill wanatoa CSR, why not haya makampuni? Ushauri, naomba tuwe na forum nao na ikibidi watoe taarifa zao za CSR.
Mheshimiwa Spika, mimi ndio champion wa kushauri na kusukuma ajenda ya kwamba kama tunataka kujenga uchumi wa viwanda tuzuie kusafirisha veneer, na mimi ndiye pia nilishauri kuwa kwa kuwa kiwanda sio kama kwenda kununua nyanya sokoni ambapo utazikuta tu, basi tuwape muda, hata hivyo imethibitika kuwa muda huo ni mfupi na ndio maana kama mshika au mtoa hoja ninashauri, pafanyike extension hata ya miaka miwili ili watu hawa wajipange.
Mheshimiwa Spika, ni mjinga tu ndiye ambaye huwa habadilishi mawazo, jambo hili limeathiri pia mapato ya mtu mmoja mmoja, lakini pia own source kwa Halmashauri zetu ikiwemo Mafinga Mjini. Ni kwa muktadha huo nashauri kuwa tufaye extension pasipo masharti na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri pamoja na ugeni wake katika Wizara nilimueleza kwa kina jambo hili.
Mheshimiwa Spika, nasema kwamba ushauri huu wa kufanya extension ya ban uwe huru pasipo masharti kwa sababu kwa msisitizo kabisa wapo watu walitumia mwanya huu kujineemesha jambo ambalo sio sawa.
Mheshimiwa Spika, tunachosisitiza mara zote ni welfare ya wafanyakazi katika viwanda na pia ulipaji wa kodi na tozo za Serikali.
Mheshimiwa Spika, kuhusu utomvu maarufu kama gundi, imethibitika kuwa hakuna athari hasa kwa miti iliyokaribia kuvunwa, ushari wangu makampuni yanayovuna ambayo hayazidi mawili, moja linavuna katika shamba la Serikali na moja katika mashamba ya GRL, wapewe miti ya kutosha ili kusudi wananchi wapate ajira, Halmashauri ipate cess na Serikali iongeze mapato. Suala hili lina faida sana hasa katika ulinzi shirikishi dhidi ya majanga ya moto. Kazi ya kuvuna gundi ilikuwa inaajiri zaidi ya watu 1000 na wengi wao wanawake, na ni kazi ambayo mtu anaweza kufanya sanbamba na kazi zingine, kwa mfano mtu akitoka shamba anajiongezea kipato kwa kwenda kuvuna gundi, analipwa kulingana na kiwango alichovuna, mimi kama mtu niliyekulia kwenye misitu, nawapa ushauri ambao ni genuine sana ambao tija yake ni kubwa kwa ustawi wa misitu na jamii zetu.
Mheshimiwa Spika, bei elekezi ya vigogo; katika vikao tulivyokaa tumejadili sana suala la bei elekezi ya vigogo kwa Wachina, ninashauri tufikie mwisho, nakambuka Kamati ya Profesa Felister ilikuwa tayari na ripoti ya nini kifanyike ili kuwa na win win situation, kwa hiyo pamoja na kuwa biashara ni huria lakini lazima tuwe na mechanism za kuona kuwa wananchi wetu wananufaika.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.