Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Makunduchi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwa mzima na kunijalia kuchangia katika Wizara hii na mimi najielekeza katika mpira wa miguu.
Mheshimiwa Naibu Spika, TFF ni Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania ambalo limejipa madaraka ya kuongoza mpira Tanzania kama ilivyo katika Katiba yake Ibara ya Kwanza. Lakini katika Ibara ya 12 imeorodhesha wanachama wake, la kusikitisha Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar halijaorodheshwa katika orodha hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, akija Naibu Waziri nataka anielezee kwa nini TFF inavunja Katiba yake na Baraza la Michezo halichukui hatua yoyote. Kwa nini hadi leo Chama cha Mpira wa Miguu Wanawake hawajafanya uchaguzi? Wakati Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake ni mwanachama halali kama alivyoorodheshwa katika Katiba Ibara ya 12. Hapa nisipopata maelezo ya kuridhisha nakusudia kuchukua shilingi ya Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo mwezi wa Machi, 2017 Chama cha Mpira wa Miguu cha Zanzibar kilipata uanachama wa CAF, lakini mwezi Julai, 2017 kiliondoshewa uanachama wake baada ya kukosa sifa za kuwa mwanachama wa FIFA. Mnamo mwezi Machi, 2021 CAF ilifanya mabadiliko yake ya Katiba Ibara ya 4(1) na Ibara ya 4(4); kwa mantiki hiyo Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar haliwezi tena kuwa mwanachama wa CAF. Sasa naomba niishauri Wizara ikae na Baraza la Michezo (BMT) na Baraza la Michezo la Zanzibar (BMZ)... (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
T A A R I F A
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba nimpe taarifa mzungumzaji, wakati umefika sasa kurejeshwa kwa Ligi Kuu ya Muungano ili tupate wawakilishi halali wa vilabu Tanzania. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ravia, taarifa umeipokea?
MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa naipokea na ninaiunga mkono kwa asilimia zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naishauri Wizara ikae na Baraza la Michezo (BMT) na Baraza la Michezo la Zanzibar (BMZ); washauriane namna ya kubadilisha Katiba ya TFF na Katiba ya ZFF ili ziendane na uhalisia uliokuwepo kwenye Katiba ya CAF na Katiba ya FIFA ikiwezekana waangalie Katiba ya TOC. Iwapo hili halikufanyika Mwenyezi Mungu akitujaalia mwakani nitalizungumza tena na kuwaomba Wizara waruhusu kuwaeleza CAF na FIFA kwamba TFF na ZFF hawashirikiani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa leo nimepunguza naunga mkono hoja. (Makofi)