Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RIZIKI S. LULIDA. Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru sana na nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyetujalia kuwa na afya njema na kuwepo hapa. Ninamshukuru Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kuitangaza Tanzania duniani na Royal Tour imetua ndani ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru Waziri, Mheshimiwa Mchengerwa, na Naibu wake Mheshimiwa Pauline Gekul kwa kazi kubwa wanayoifanya, Katibu Mkuu Ndugu Hassan Abbas na Naibu wake Ndugu Saidi Yakubu Majembe, vilevile niwashukuru BMT ikiongozwa na Ndugu Singo, anajua kabisa humu ndani anae Mama yake anaitwa Double Riziki, yeye ni Single mimi ni Double. Ninamshukuru Ndugu Neema Msita nae vilevile yuko BMT anafanya kazi nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie kuwa hii Wizara ni Wizara nyeti ambayo ikiwekeza vizuri italeta ajira kubwa sana kwa vijana. Ninaipongeza timu yangu ya Tembo Warriors, hii timu ni ya vijana shupavu, wenye ulemavu, ambao walipambana mpaka sasa hivi na wamesaidiwa na Serikali katika uwekezaji wao mpaka sasa hivi Tembo Warriors wanakwenda katika World Cup. Ninamshukuru Waziri Mkuu, Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, akishirikiana na Mheshimiwa Rais walikuja kuwachangia uwanjani Shilingi Milioni 150. Ilileta chachu na hamasa kubwa kwa hawa vijana na ushindi wao sasa hivi tunaona unawapeleka katika World Cup. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawapongeza Serengeti Girls. Haya yote ni makundi maalum, mkiyaacha makundi maalum mngefanya makosa makubwa sana, kumbe makundi maalum yana uwezo mkubwa sana katika michezo. Leo nchi inapata faraja, inapata heshima kwa ajili ya makundi maalum ya walemavu na wanawake. Tujiulize, wanaume wako wapi, mimi naweka question mark, mtajitambua wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, klabu zote sasa hivi Tanzania ziwashirikishe makundi maalum ikiwemo klabu kubwa kama Simba Sports Club, nasema tena, kama Simba Sports Club. Wawe na kundi maalum la walemavu na wanawake, na timu kama ile ya Yanga Sports Club, nao vilevile wawaweke wanawake na watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli ninaposema ni ajira nataka niseme ni ajira kweli. Tembo Warriors sasa hivi nina vijana wanne wamepata u-professional player, wameajiriwa huko Uturuki. Tayari tumefanya wapate ajira na wajitegemee wenyewe, ninataka kuwataja kwa majina na tuwapongeze. Ndugu Khalfani Kihanga, ni kijana mlemavu kutoka Tabora lakini sasa hivi yuko Uturuki. Ndugu Ramadhani Chomelo, huyu kijana anatoka Kisarawe sasa hivi ni mchezaji Uturuki. Ndugu Frank Ngairo, anatoka Iringa, sasa hivi ni mchezaji Uturuki, Ndugu Shadrack Hebron kutoka Mbeya. Jamani kazi ya vijana ni kubwa sana kuwasaidia hawa, tukiwekeza zaidi hapa ina maana tutawatoa vijana wengi watakwenda katika professional soccer, watakuwa wanajitegemea wenyewe, hawategemei tena kusaidiwa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ilichukuliwa watu wenye ulemavu ni watu wa kusaidiwa, Hapana! Watu wenye ulemavu wanajiweza wenyewe. Twendeni pamoja tuka-invest kwa watu wenye ulemavu ili waweze kujitegemea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu sanaa; kwanza niwapongeze wasanii, katika sanaa vijana wameonesha kazi kubwa sana, sasa hivi wanaitangaza Tanzania duniani katika Royal Tour. Maana yake katika kutangaza utalii, unatangaza katika maeneo mbalimbali, utalii katika utamaduni, michezo, mila na culture mbalimbali yote yanaingia katika Royal Tour na Royal Tour nyumbani kwake ndiyo hapa michezo na utamaduni.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka niwataje vijana ambao sasa hivi unaona wanawika na kuitangaza Tanzania duniani. Namba moja ni Diamond Platinumz; Harmonize (Konde Boy); Ali Kiba, Zuchu, Ray Vanny na wasanii wengine ambao wanaendelea kuonesha nchi katika maendeleo makubwa. Hawa watoto wanaonesha usanii na wameajiri watu na kuajiri watu ina maana na wao wenyewe wanajitegemea katika kuipatia mapato makubwa nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, matumaini yangu ni kuwa tusimamame na hawa watu na haya makundi ili tuweze kuitengeneza Tanzania yenye kujitegemea kwa kupitia usanii pamoja na michezo inawezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Royal Tour; mimi nakwenda kuitangaza nikiwa mmoja kati ya mabalozi wa utalii. Katika mabalozi wa utalii tunataka kuunganisha michezo na utaliii. Maana yake ni nini? Tunataka kuanzisha ndani ya mbuga zetu za wanyama waje wacheze mpira ndani ya Serengeti. Maana yangu ni kuwa ndani ya Serengeti na Ngorongoro kuna viwanja vya mpira, tukalete timu kubwa ziingie pale. Zitakapoingia pale baadae tutakuwa tunajiuza wenyewe na soko letu liko pale, kuwa leo timu ya Arsenal wanashindana na Manchester ndani ya Serengeti. Hapo tutakuwa tumemuunga mkono na hii itakuwa na shughuli ambayo ni very sustainable na itatuingizia mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapato yale tutakubaliana kabisa, fungu maalum litakwenda kwa ajili ya makundi maalum ili baadaye wasihangaike na mambo ya kutafuta chakula, mavazi, hata nguo za kuvaa iwe ishu, kuombaomba. Hakuna kuombaomba, wenyewe hawa wanajiweza, tukiwatengenezea mfumo mzuri watakuwa wanaweza kujipatia mapato yao bila kutegemea kuombaomba na sehemu nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, sina mengi sana ya kuongea, kwa siku ya leo ninaomba na kuwaunga mkono kwa asilimia kubwa sana kuwasimamia hawa vijana. Vijana wanakwenda katika mapambano makubwa ya World Cup na tusibweteke sasa hivi ndiyo kipindi cha kusimama nao. Nashukuru Tembo Warriors wanaondoka kwenda Poland, wamepata nafasi maalum kwenda kujiimarisha kwa muda wa siku kumi. Ninaomba tufanye kila njia tuwasaidie hawa watoto katika kwenda kwao huko wasipate taabu ya chakula au ya matumizi, na Wabunge tuna jambo letu, tunasema hapa tunanyamaza lakini Wabunge kwa pamoja tumeungana kuwapenda watu wenye ulemavu na wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeze vilevile Mheshimiwa Keisha, amekuwa ni mentor wangu, nae ameanzisha timu ya watu wenye ualbino nao wanakwenda Kenya. Kutokana na mfumo huu, tukienda katika mazingira hayo Tanzania yenye maendeleo ya michezo na utalii na kuingiza kipato katika sanaa ya vijana inawezekana. Nawashukuru sana na ahsante sana. (Makofi)