Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ubungo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Nataka nichangie pointi tatu tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nataka nitumie nafasi hii kuwapongeza sana, pale Jimbo la Ubungo kama unavyojua, tumejaliwa, tuna kila aina ya talent pale. Nataka nitumie nafasi hii niwapongeze vijana wetu, tuna timu pale za mpira wa miguu 25, karibu timu tatu kwa kila Kata, wanacheza na zimesajiliwa na TFF. Tunazo timu tisa za netiboli, wanacheza, pia pale tuna champions, wanamichezo wa ngumi, kila Kata, wako wengi. Tunao champions ambao wameshakuwa na majina Kitaifa, nataka niwapongeze sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza champion Selemani Kidunda wa kutoka Jeshi Camp kutoka Kata ya Mburahati. Champion Mfaume Mfaume wote mnamfahamu hapa, si mumpigie makofi, kutoka Kata ya Mabibo. Tunaye Champion Baiza Mazola kutoka Kata ya Mabibo. Champion Nasib Ramadhan kutoka Kata ya Mabibo. Champion Iddi Pialali wote tunamfahamu huyu kutoka Kata ya Manzese. Tunaye Champion Pengo kutoka Kata ya Manzese. Hawa ni vijana ambao wanatupa furaha sana kwa sababu Wizara hii moja ya jukumu lake ni kuleta furaha katika nchi na hawa vijana wanatupa furaha sana Dar-es-Salaam na katika kata yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze wanamuziki wakubwa, wazito katika Jimbo la Ubungo, nikianza na Dulla Makabila, anafanya vizuri sana. Shoko Mwamba anafanya vizuri sana. Madee Ali, kijana yule, Ney wa Mitego, Tundaman, Segu Segumbo, Dogo Dulla, Amigo, Bayo Fundi Ubungo na Mariam wote kutoka Ubungo. Wanaleta furaha katika Mkoa wa Dar-es-Salaam.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Wewe uliomba ruhusa kwenda hospitali, nenda hospitali. Hakuna taarifa, endelea. (Kicheko)
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Hoja yangu ya pili.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ester kaa chini wewe ni mgonjwa. Sasa usije ukazungumza vitu hapa. (Kicheko)
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni ombi. Nataka nichukue nafasi hii, Mheshimiwa Ester ugua pole, nataka nitumie nafasi hii nilete ombi. Pale Jimbo la Ubungo na hususan Kata ya Manzese na Sinza tuna uwanja wa kihistoria, uwanja unaoitwa TP. Huu ni uwanja ambao upo mpakani mwa Kata ya Manzese na Kata ya Sinza, Mtaa wa Chakula Bora upande wa Manzese na Mtaa wa Sinza E upande wa Sinza, ni uwanja muhimu sana na umuhimu wake pia ni wa kihistoria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla Yanga haijaanza mwaka 1935, mwaka 1920 mpaka 1926 ilikuwa inaitwa Young Boys na ilianzia Manzese kabla ya kwenda Kariakoo, walikuwa wanachezea uwanja huu wa TP. Baada ya kwenda Kariakoo ndio wakaanza kuitwa Young Africans na badaye mwaka 36 baada ya mambo kuwa mabaya walikuwa wanashindwa sana ndio wale jamaa wakajitoa wakaondolewa wakaenda wakaanzisha Simba. Kwa hiyo, Simba basically ni timu ambayo inatokana na Yanga, walikuwa ni waasi baada ya kufukuzwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndio maana maana haka kahistoria watu hawakaelewi, lakini ilianzia Manzese, ikaenda Kariakoo, 1935 ikawa ni Young Africans, 1936 wakaenguliwa baadhi wakaanzisha Simba, wakabaki Yanga kupigania uhuru, kwa hiyo, hili ni jambo la msingi. Sasa ule uwanja wa TP ni muhimu na tunahitaji kwa kweli kwa ajili ya…
NAIBU SPIKA: Sasa Mheshimiwa Kitila Mkumbo, Kiti kikikuomba ushahidi wa haya mambo unayo?
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ndio ninao, nitaleta. (Makofi/Kicheko)
NAIBU SPIKA: Haya, endelea.
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nitaleta na paper zipo zimeandikwa, nitaleta. Ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aniangalie katika jambo hili. Kwa historia hii naomba anipe nguvu uwanja wa TP tuutengeneze, iweze kufanyika michezo. Sisi pale ni maarufu kwa suala la Ndondo Cup analifahamu, atatusaidia sana kwa Ndondo Cup.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho, kama nilivyosema awali, sisi maisha kisaikolojia, maisha ni nini? Ni mchakato wa kutafuta furaha, ndio maana ya maisha. Kwa hiyo, jambo lolote ambalo linaleta furaha ni muhimu likaungwa mkono. Sasa juzi nilikutana na, pia suala la furaha Mheshimiwa Waziri ni kazi yake, moja ya kazi ya msingi ya Wizara hii ni furaha. Nimeona hata kwenye speech yake ameiweka vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nimekaa na Daktari mmoja anafanya kazi katika moja ya hospitali za Serikali Dar-es-Salaam, yeye anakaa Kata ya Makuburi, amekuja kunilalamikia anasema karibu kila siku mara tatu kwa wiki anakamatwa. Kwa sababu gani? Yeye anafanya kazi mortuary, usiku anaondoka asubuhi. Kabla hajaenda nyumbani, ananiambia, yeye hunywa bia sita asubuhi, lakini kila akienda kunywa bia sita pale karibu na nyumbani kwake kwenye baa anakamatwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikakutana pia na wafanyabiashara, nilikuwa na kikao nao Dar-es-Salaam. Wakaniambia kwamba, Dar-es-Salaam moja ya lalamiko lao ni kwamba, hawaruhusiwi kufungua baa asubuhi na mwisho saa sita, kwa hiyo, inamaanisha kwamba, nikasema tatizo ni nini? Nikagundua kuna sheria ya The Intoxicating Liquors 1968, kile Kifungu cha 14, kimepangia watu muda wa kufurahi kwamba, hakuna kufurahi mpaka saa 6.00 mchana na mwisho wa kufurahi saa 6.00 usiku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wewe unafahamu majiji yote duniani hufanya kazi saa 24. Hii habari kwamba, watu asubuhi wasifungue biashara, wasifungue baa, wasifurahi mpaka saa 6.00 mchana ni sheria ya kizamani na hii sheria ilitungwa 1968 mwaka mmoja baada ya Azimio la Arusha ili watu na wakati huo nchi ilikuwa ni nchi ya wakulima na wafanyakazi, ilikuwa wanatakiwa wakalime mashambani, wakafanye kazi maofisini. Sasa huko tulishaondoka, hii ni nchi ya wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara, wanamichezo, wanaburudani, wote kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hili, hii sheria inazuia furaha ya nchi. Aiangalie tuibadilishe ili watu wawe na uhuru wa kufurahi wakati wowote maadam wanazingatia sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi...
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa. Mheshimiwa Gwajima.
TAARIFA
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilipenda kumpa Taarifa tu rafiki yangu Mheshimiwa Profesa Kitila kwamba, furaha haiko aina moja, ziko aina nyingi sana za furaha. Kama hawawezi wakaipata furaha inayotokana na kunywa pombe, basi wapate furaha inayotokana na vitu vingine. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kitila.
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu nimtaarifu Mheshimiwa Askofu kwamba, kabla hajaziponya hizo roho, lazima tuponye miili ili apate roho. Kwa hiyo na kwa sababu hiyo, naomba kwa heshima na taadhima nisipokee Taarifa yake. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, so, namalizia kwamba, on a serious note na hii baadaye Wizara ya Fedha itamhusu kwenye bajeti yake, Dar-es-Salaam Jiji la biashara, hawawezi kupanga muda wa kufanya biashara. Dar-es-Salaam watu watafanya kazi 24 Hours, mtu anafanya kazi usiku ana haki ya kwenda kufanya burudani asubuhi. Hii tuiangalie sheria hii ibadilishwe ili tufanye biashara 24 Hours tukusanye kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nichukue nafasi hii kabisa kwa dhati nimpongeze sana Mheshimiwa Mchengerwa. Nampongeza kwa jambo moja tu, hii Wizara ameipa hadhi sana, ameipa heshima, yaani ni Waziri ambaye yuko very proud kuwa Waziri wa Michezo, this is very good. Ameifanya kwamba, kumbe kila mtu anaweza akatamani kuwa Waziri wa Michezo, nampongeza kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia. (Makofi)