Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie katika hotuba hii ya Wizara ya Fedha. Mimi nitakuwa na michango miwili tu kama muda utaniruhusu nitazungumzia ufanisi uliopo katika Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa maana ya TRA na baadaye nitagusia haja ya kupanua wigo wa kodi na vilevile kuitaka Serikali au kuiomba Serikali iangalie tena nafasi yake katika utekelezaji wa blue print kwa madhumuni ya kuweza kuchagiza ufanyaji wa biashara katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, hakuna mtu ambaye anabisha kwamba Serikali inahitaji kukusanya mapato, hakuna mtu anayebisha katika hilo; na ili tuweze kufanikisha maisha bora ya Watanzania lazima Serikali iweze kufanikiwa na ndiyo kazi yetu sisi kuweza kuishauri Serikali iweze ikafanya vizuri na hata ukiangalia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri numbers ambazo amezionesha kutokana na performance ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali katika kipindi hadi kufikia Aprili inaonesha kwamba wamefanya vizuri. Kwa sababu ni average ya asilimia 90 na kwenda juu, hivyo kama ni Chuo Kikuu Mheshimiwa Mwigulu umefanya performance ya “A” ama A plus na hapa lazima nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa sababu Mheshimiwa Rais ndiyo captain wa timu hii ya kina Mwigulu. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri kwa sababu naamini hata uwekaji watu sahihi katika maeneo sahihi ya Wizara ya Fedha na TRA yameweza kutuletea mafanikio haya ambayo tunayazungumza leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mimi nilikuwa naangalia andiko la ActionAid ambalo andiko hili limetolewa mwaka 2021 wenyewe wameliita Sealing the Gaps. Walikuwa wanaangalia mfumo wetu wa kikodi na kimapato, wakaona kwamba kuna matundu ambayo yanasababisha nchi yetu tusiweze tukafikia ukusanyaji bora wa mapato na wenyewe wanakisia kwamba kuna shilingi trilioni 17.4 yawezekana zinaeleaelea na Serikali hazikusanyi ni fedha nyingi sana. Na wenyewe wanasema kuna changamoto za usimamiaji wa masuala ya kodi, wanasema kuna kodi ambazo hazilipwi na hazikusanywi, watu wachache kwa maana ya wigo ni mdogo mno wa watu ambao wanaotozwa kodi na kwa hali hii wanashabikia utanuzi wa wigo wa ulipaji wa kodi, haya ni maneno mazuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na ukiaangalia sisi tunayafahamu naamini hata Serikali inafahamu na kwa kuwa Serikali inafahamu, ni dhahiri kinachofanyika sasa kwa performance hii naweza nikasema tayari tumeanza kuona njia sahihi ya kuweza kwenda.

Mheshimiwa Spika, lakini ukiiangalia TRA hii hakika inafanya kazi nzuri ingawa ina challenges kubwa sana, ina changamoto nyingi, kwa mfano miaka mingi TRA imekuwa ikipiga kelele kuhusu kuongezewa idadi ya wafanyakazi. Na ni mpaka juzi walikuwa na watu 4,000 na ushee. Nashukuru Serikali kwamba wamewaongezea ajira ya watu 2,000 kama tulivyosikia katika hotuba hapa, lakini hitaji lao sasa hivi ni watu 8,000 na ushee maana yake kwamba bado kuna deficit, kuna upungufu wa watu 2,000.

Sasa kutokana na upungufu huo na ukiongezea ukweli kwamba mifumo ambayo ingeweza ku-support masuala mazima ya administration ya kodi hakika TRA wangeweza kufanya vizuri zaidi. Nataka niwape mfano mmoja mdogo tu, katika Bunge lako hili niliwahi kusimama na kuzungumza kuhusu kuongeza au kuweka Maafisa Kodi kwenye kila kata na nikatoa mfano, kama tuna Maafisa Ugani, kama kuna Maafisa wa Ustawi wa Jamii kwa nini tusiwe na Maafisa Kodi kwenye kila Kata. Nashukuru na naipongeza TRA walisikia ushauri ule na hata kwenye Kamati yetu tukatoa tena ushauri ule. Walichofanya ni nini, walikusanya vijana 250 kule Dar es Salaam wakawapeleka katika maeneo ya Kinondoni, Ilala, Tegeta na Temeke ili kwenda kuangalia ufanyaji wa biashara na kuweza kuangalia kama kila anayefanya biashara anatambuliwa na amesajiliwa kwa maana ya mlipa kodi.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwezi mmoja ama miezi miwili waligundua wafanyabiashara 27,463 hawakuwemo katika mfumo wa kodi. Sasa hiyo maana yake ni kwamba katika kipindi kirefu kuna watu ambao wanafanya biashara, lakini hawalipi kodi stahiki. Hivyo mimi niwapongeze TRA na niipongeze Serikali kwamba kumbe mnaweza mkatusikiliza Wabunge na mkayachukua yale ambayo tunawashauri na mkafanyia kazi, hongereni sana kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nisemee kuhusu mifumo, yawezekana tukawa na watu mahiri, skilled katika maeneo mengi TRA, lakini bila ya kuwa na mifumo imara hawawezi wakafanikiwa. Hebu angalia kwa mwezi Machi ambapo mfumo wa e-filing wa VAT Returns zile za kulipia VAT walianzisha mfumo wao mwezi wa tatu na ukiongeza idadi ya wafanyakazi ambao wamewapata performance imekuwa ni nzuri sana. Performance yao ukiiangalia kwa mwezi Machi kodi za ndani zilifikia asilimia 111.5 hongereni sana TRA kwa kazi hiyo. (Makofi)

Lakini vilevile ukiangalia upande wa VAT mwezi Aprili walifikia asilimia 103.8 performance yao kuzidi malengo na ukiangaliza namba zote wame exceed malengo waliyojiwekea. Maana yake ni kwamba endapo watakuwa na mifumo sahihi kama ilivyo hii ya VAT ni dhahiri kabisa Serikali inaweza ikafanya vizuri na hapa nataka niikumbushe Serikali kuna mfumo mmoja unaitwa IDRAS nilikuwa nateta na mwananchi mwenzangu pale bigwa Mheshimiwa Mwigulu kwamba IDRAS ni mfumo ambao utaisaidia sana Serikali katika kupata fedha kupitia kodi za ndani.

Mheshimiwa Spika, hiyo ni kengele ya kwangu hiyo?

SPIKA: Hapana.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Sawa ahsante.

Mheshimiwa Spika, IDRAS ndiyo mwarobaini kwa sababu IDRAS itasimamia vizuri sana mifumo ya kodi za ndani kama ilivyo katika VAT kiasi kwamba mfumo huu ukiwa mahiri utaweza kuzungumza na mifumo mingine. Serikali imeonesha utayari wenu, sasa huu mfumo tunajua ni ghali na ilikuwepo na juhudi kuupata tangu Serikali ya Awamu ya Tano, lakini ile tender ika-fail. Sasa msitafute wafadhili, Mheshimiwa Waziri msitafute wafadhili, Serikali igharamie yenyewe mfumo huu, huu mfumo ndiyo utatuondolea matatizo. Angalia mfumo huu unaweza ukajumuishwa na miamala ya simu, mfumo huu unaweza ukajumuishwa na Forodha...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30 malizia sentensi.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, mifumo ya Forodha na mifumo mingine yote ya NSSF. Kiasi kwamba hata component ya pay as you earn mtaipata ya kutosha kuliko ilivyo hivi sasa.

Mheshimiwa Spika, hivyo ningeiomba Serikali inapokuja kumalizia na kutoa hitimisho itueleze inajipanga vipi kuhakikisha kodi za ndani zinapata mfumo mahiri ili kuweza kutusaidia kukusanya fedha za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja hii. Ahsante sana. (Makofi)