Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye Wizara yetu hii muhimu kabisa.

Mheshimiwa Spika, kwanza, nitumie nafasi hii kuwapongeza sana kwa usimamizi mzuri wa kamisaa wetu Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Naibu Waziri wake, Mheshimiwa Hassan Chande, lakini niwapongeze sana watendaji wakiongozwa na wakuu wetu watatu hawa; Emmanuel Tutuba - Katibu Mkuu wa Wizara hii, pamoja na Naibu Makatibu Wakuu wawili; kaka yangu Lawrence Mafuru na dada Jenifa Omolo, wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ziada nimshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli kazi anayoendelea kufanya ni lazima tuseme, anafanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri ameeleza vizuri juu ya eneo la usimamizi wa sera za kiuchumi, uchumi jumla na akatuambia ni ukweli mambo makubwa ambayo yametusaidia sana ukuaji wa uchumi wa nchi yetu kuendelea kubaki kwenye asilimia 4.9 ukilinganisha na asilimia 4.8 kwa mwaka 2020.

Mheshimiwa Spika, kubwa sana ni kuwezesha shughuli mbalimbali baada ya UVIKO-19 kurejesha ile hali nzuri ambayo tulidhurika katika muda ule ambao watu mnakumbuka tulivyoingia kwenye UVIKO-19. Lakini ziada ya hapo pia kuwezesha upatikanaji wa mikopo ya riba nafuu. Haya ni mambo makubwa na ni ya kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. Ndio amesababisha tukaendelea kuwa stable kama nchi katika hali ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nitajielekeza katika maeneo kama mawili hivi, na muda ukiniruhusu eneo la tatu.

Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza ni madeni; nitumie nafasi hii kumpongeza tena kama wenzangu waliotanguliwa kusema, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuweza kutoa shilingi bilioni 772.87 kuweza kulipa madeni mbalimbali. Madeni ya wakandarasi zaidi ya shilingi bilioni nne, wazabuni zaidi ya shilingi bilioni 81.6, watumishi nje ya mishahara shilingi bilioni 25.7, watoa huduma shilingi bilioni 52.7 na madeni mengineyo zaidi ya shilingi bilioni 608.51, jumla yake ni takribani shilingi bilioni 772; siyo jambo la kawaida, ni jambo la kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, taarifa inatuambia yapo madeni mengine ambayo yako chini ya Msajili wa Hazina, yapo madeni ya mashirika na taasisi za umma ambayo yanatakiwa kulipwa na Msajili wa Hazina; hapa shida ipo.

Mheshimiwa Spika, Watanzania wenzetu hasa wa sekta binafsi, wanajitahidi sana kujiinua kiuchumi kwa kukopa na kadhalika ili waweze kusaidia kutoa huduma Serikalini. Lakini Watanzania wengi wanakufa, wafanyabiashara wenzetu hawa wanaumia. Leo nataka nikwambie mfano mdogo sana, mwaka 2005 kampuni moja na hii niliwahi kuwasilisha hata kwenye Kamati Kampuni moja, NICOS ilifanya kazi na TRL wakati ule wa kampuni tanzui ile HSC sijui. Toka wakati huo, mwaka 2005, ikalipwa mara moja, mbili, baadaye mgogoro, mwaka 2009 mahakamani, mwaka 2014 hukumu ikatoka mumlipe pamoja na riba na gharama zake zote za mahakama. Mpaka leo mwaka 2022 miaka saba, kimya, hakuna cha kulipa wala kujibu barua.

Mheshimiwa Spika, lakini mwisho wa siku leo, baada ya kubanana sana watu ndio wanataka kwenda tena mahakamani kusema hatujaridhika na hukumu ya mahakama ya miaka nane, siyo sawa. Huyu ni Mtanzania. Sasa huyu ni mmoja, je, Watanzania wangapi ambao wamekopa na leo wamefilisika kwa sababu ya kushindwa kulipwa madeni yao?

Kwa hiyo, niliona ni vizuri jambo hili wenzetu mliangalie kwenye sura ambayo itawasaidia Watanzania waweze kujiinua kiuchumi badala ya kuweza kuanguka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme jambo la pili; wengine wamesema pia kuhusu Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani (Internal Auditor). Taarifa yetu inajieleza sana juu ya taarifa ya Mkaguzi wa Ndani kuelekezwa kwenye Kamati ya Ukaguzi (Audit Committee), na tukazungumza pale idadi ya watu watano, lakini tungetamani sana ili kuondoa inpairness, wawili watoke ndani watatu watoke nje. Ushauri mzuri nami naunga mkono kwa sababu ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti.

Mheshimiwa Spika, katika kuboresha, ukiangalia Taarifa ya CAG sehemu kubwa hasa kwenye LGAs, kwenye taarifa kule kwenye Halmashauri zetu, shida ikitokea kule kwenye Taarifa ya CAG anakwenda kubebwa Internal Auditor, Mhasibu na Mweka Hazina, hakuna wengine wanaobwebwa. Lakini furaha ikija kwenye taasisi ya kupata hati safi anapigiwa makofi Mkurugenzi na wasimamizi wao ambao ni Sekretarieti za Mikoa; hii ni shida. Jicho letu liende vizuri, niliwahi kushauri humu mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi natoa experience, nimetumika kwenye Sekretarieti za Mikoa. Kuna mtu anaitwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani (Regional Chief Internal Auditor), hana kazi, hana kazi. Na kwa nini hana kazi, anahitajika akitumika huyu naamini CAG atakwenda kufurahi kufanya kazi zake vizuri na ata-rely on the work of internal auditors. Vinginevyo, kama alivyosema Mheshimiwa Subira, siyo lazima, sheria haimlazimishi external auditor aka-rely kwenye kazi ya internal auditor, akikuta internal control iko vibaya anaachana nayo, anakuja na ya kwake.

Mheshimiwa Spika, sasa liko jambo hapa, ni la kimuundo tu na nitoe mfano, Sekretarieti hizi chini kule, kutoka kwenye Sekretarieti za Mikoa kuna mtu anaitwa Katibu Tawala Msaidizi - Local Government. Huyu mtu ana vi-organ pale, yuko autonomous kabisa, katengeneza mtu wa fedha na katengeneza internal auditor, lakini hawa watu ni ma-junior sana, ma-junior in such a way kwamba hawawezi kwenda kusimamia kazi ya wakubwa wao chini. Haiwezekani kuna ma-internal auditors ambao ni Wakuu wa Idara wanakwenda kusimamiwa na senior auditor ambaye anatoka kwenye kitengo cha Katibu Tawala Msaidizi - Local Government. Kwa nini wakati kuna Chief Internal Auditor hana kazi, hawezi kushuka chini anaishia kufanya kazi kwenye ofisi za ma-DAS tu, ndiyo anakagua. Sasa huo u-chief wa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi nashauri ni vizuri mkatengeneze muundo ili uboreshwe mumpe majukumu Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Mkoa aweze ku-oversee kazi za ma-internal auditors ambao kimsingi hata kwenye ikama zenu yule ni bosi wa ma-internal auditors wa Local Government. Kwa hiyo utaona ile seniority inaweza ikaenda vizuri. Na mwisho wakitoka na taarifa kimkoa basi ni vizuri sana ninavyoona internal auditors wanaweza kwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, la mwisho kwa dakika moja ni contingency fund (CFE).

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30, kengele ilishagonga.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, basi hili niliache, nashukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)