Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika hoja iliyoko mbele yetu, na mimi nitakuwa na hoja moja tu kuhusiana na maduka ya kubadilishia fedha za kigeni hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, tunakumbuka mwaka 2018 Serikali iliunda task force na ikafanya uvamizi katika maduka haya ya kubadilishia fedha na hususan katika Kanda ya Kaskazini, mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ndio ambao wameathirika kwa kiwango kikubwa. Task force hizi zilivamia maduka haya zikachukua fedha, zikachukua vifaa mbalimbali ikiwemo computers, EFD machines, baadhi ya wafanyabiashara wakachukuliwa hati za ardhi, na kadhalika. Na leo nazungumza hii ni kama mara ya tatu au sio ya nne ndani ya Bunge hili kutaka kujua kauli ya Serikali kuhusiana na wafanyabiashara hawa ambao wameporwa fedha zao toka mwaka 2018 mpaka leo hakuna muafaka wowote uliofikiwa kuhusiana na jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mmechukua mpaka hati za ardhi za watu, mmechukua fedha cash, mmechukua vifaa mbalimbali, wafanyabiashara hawa hawajui hatima yao. Ni lini Serikali mtafikia muafaka kuhusiana na mashauri haya ya wafanyabiashara hawa ambao mlikwapua fedha zao katika maduka ya kubadilishia fedha? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kama haitoshi mmeunda tena task force mpya, mmeenda kwa wafanyabiashara hawa kuwaambia tena wanadaiwa. Sasa mmewachukulia kila kitu, mmewanyang’anya, bado mmeunda task force tena kuwaambia wafanyabiashara hao wanadaiwa, kwa nini? Na kwa nini mnafanya kazi kwa task force tu ya kutishia watu na si kuleta amani na muafaka ili watu wafanye biashara kwa uaminifu? (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, naomba tupate majibu ya kina na ya ukweli. Na wafanyabiashara hawa wanataka kujua hatima ya fedha zao mlizozichukua bila utaratibu.
Mheshimiwa Spika, na niliwahi kusema hapa, hawa watu wanavyofanya biashara wana leseni za biashara, wamefuata taratibu zote, hakuna mtu ambaye alikuja tu akawa anafanya biashara hajafuata taratibu. Mliwatambua, walifanya biashara kwa utaratibu, kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni. Bado mkaja mkawanyanyasa na kuwavamia na kuwachukulia fedha na kila kitu. Naomba kupata majibu Mheshimiwa Waziri kwa sababu ni mara nyingi nimeshaongelea suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia kama haitoshi mmeweka masharti mapya magumu ya watu wanaotaka kufanya biashara ya kubadilisha fedha kwa kuanzisha maduka. Mmeweka masharti magumu sana ambayo kwa kweli, hayawezi kutekelezeka. Mnataka mtu ili apewe leseni hii awe na fedha shilingi bilioni moja ndio aweze kufungua, na tena katika hiyo bilioni moja ili aweze kupata sasa leseni na kibali, maana yake awe na fedha asilimia 70 ya hizo fedha, maana yake ni shilingi milioni 700. Hivi kwa nini kuna ugumu kwenye jambo hili katika kufanya biashara hii?
Mheshimiwa Spika, huko nyuma watu walifanya biashara, Arusha ndio biashara ambayo ipo na Kilimanjaro kwa sababu ni miji ya kitalii. Sasa kwa nini mnaweka masharti haya magumu kiasi hicho? Kuna nini kimejificha hapa Mheshimiwa Waziri?
Mheshimiwa Spika, lakini kama haitoshi wako baadhi ya wafanyabisahara pamoja namasharti hayo magumu, wako baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekidhi hivyo vigezo. Wameleta maombi, lakini mpaka leo wana karibu miaka miwili, mitatu, hamjatoa leseni, kuna nini hapa? Kuna nini ambacho kimejificha? (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, ningetamani nipate majibu ya masuala haya niliyoyaeleza, lakini kama haitoshi tunataka kujua hii biashara ya kufungua maduka ya kubadilishia fedha ndani ya nchi hii, kama mtangaze ni janga mseme ni janga, kama mnaona ni biashara ambayo ni hatari muwaambie. Hawa wafanyabiashara wamekaa hawajui hatima yao, hata hao wapya ambao wamekidhi vigezo wameleta kwenu bado mmekaa kimya, kuna nini hapa ambacho kinaitishia Serikali na mnapata kigugumizi kuhusiana na suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikushukuru. Langu ni hilo na kama sitaridhika nafikiri tutakutana kwenye shilingi baadae Mheshimiwa Waziri. (Makofi)