Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZULFA MMAKA OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia leo. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima na uhai wake na kuweza kuwepo katika Bunge hili Tukufu na kutupa pumzi za kuchangia.
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyofanya kazi zake kwa weledi, umahiri na kwa utulivu kabisa kwa kuzingatia kwamba sisi tunamtegemea na tunampenda, kwa hiyo nimpongeze sana kwa kazi hizo nzuri ambazo anazifanya. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, pamoja na watendaji wote wa Wizara hii ya Fedha kwa jinsi wanavyofanya kazi zao katika kuinua uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze na suala zima la ukusanyaji wa mapato kule TRA. Mimi ni balozi wa kodi ambaye kwa uwezo wangu nafasi hii niliipokea katika bajeti tunayoimalizia kutoka kwa Mheshimiwa Waziri. Nimpongeze sana kwa uteuzi huu na nimwambie kwamba kazi ile ambayo alinituma naifanya na ni kazi nzuri, nimejifunza mengi na naendelea kujifunza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze na suala zima la mipakani. Wakati tupo katika ziara zetu tulibahatika kutembea katika mipaka mingi ya Tanzania. Katika mipaka hiyo tulienda katika mpaka mmoja wa Rombo Tarakea. Hii ni sehemu ambayo wanakusanya pesa nyingi, wanazalisha pesa nyingi, wanafanya kazi nzito na sehemu ile inafanya kazi kubwa, ila wanafanya katika mazingira mazito. Pale hakuna kituo ambacho wanafanya kazi kwa pamoja kama katika Vituo vingine kama cha Namanga, ambao wao wana Kituo cha Pamoja ambacho kinarahisisha ufanyaji kazi na kinawarahisishia wale ambao wanakwenda kufuata huduma pale, kuipata huduma ile kwa muda mfupi na huduma nzuri. Kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri vituo hivi avitembelee, vinakusanya mapato makubwa lakini wanafanya kazi nzito kwa sababu hakuna vitendea kazi, hawana usafiri, hawana majengo mazuri hata huduma ya afya katika vituo vile kwa kweli haiko vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia katika bajeti ya uanzishaji wa Ofisi za TRA tulikuta kwamba kuna baadhi ya maeneo kama eneo la Kotoro katika Mji wa Kahama kuna kilomita tisini kutoka mjini ambapo watu watafuata kwa ajili ya huduma hii. Hiki kinapelekea wananchi kuwa na uzito kidogo wa kufuata huduma hizi katika vituo vile na uzito ule unapelekea kutokulipa kodi na kodi ya nchi yetu kushuka kidogo. Kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri katika bajeti hii aiangalie vizuri bajeti ya uanzishaji wa ofisi ili waweze kukusanya mapato kama ambavyo tumejipangia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende katika ukurasa wa 54, hapa kuna jambo zuri ambalo limefanywa na mama yetu na sisi hatuna budi kumpongeza kwa sababu tunaona kuna vifaa vya afya ambavyo vimeandikwa pale vinavyoenda kununuliwa kwa ajili ya wananchi. Hivi vyote vinatokana na kodi ambazo zinakusanywa. Vifaa hivi ni kama x-ray machines 130 ambazo zitanunuliwa, CT scan pamoja na mashine za oksijeni. Hili ni jambo zuri na tunampongeza sana mama yetu kwa kujali afya za wananchi wake na sisi tumwambie kwamba malipo haya atayakuta kwa Mwenyezi Mungu na tutakuwa naye bega kwa bega. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niongelee pia kuhusu suala zima la Kitengo cha Elimu kwa Mlipakodi, katika kazi ambayo inatakiwa kuongezwa na kuzidisha kuifanya ni suala zima la elimu. Tunakuta kwamba wananchi wengi hawana elimu hasa ya ulipaji wa kodi. Unakuta anakwambia kwamba hela nyingi inakwenda kwa ajili ya kununua mashine, ila sasa wanapopata ile elimu kwamba hela ile ambayo tunanunua mashine mwisho wa siku ukienda kulipia kodi inaangaliwa ulitoa shilingi ngapi, baada ya hapo ndiyo unapigiwa hesabu ambayo imebakia kwa ajili ya ile mashine, wataelewa. Hivyo, tunasema kwamba elimu bado inahitajika kwa wananchi, kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kile Kitengo cha Elimu kwa Mlipakodi akiongezee bajeti yake ili iweze kuwafikia wananchi wengi kwa haraka na kwa ufanisi. Kwa hiyo, naamini kwamba kwa kazi ambayo wamefanya na kwa asilimia ambayo wameipata ya ukusanyaji wa kodi atazidi kuwaangalia zaidi watu hawa ili elimu izidi.
Mheshimiwa Spika, niende katika suala zima la pongezi kwa Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, tunaona kwamba ni jinsi gani anawapenda wananchi wake wakubwa na wadogo. Kitendo cha kufuta malipo kuanzia elimu ya chini hadi kidato cha sita ni suala kubwa sana. Hili halijawahi kutokea na sisi tumwambie Mama Samia kwamba tunamshukuru sana kwa sababu mzigo huu hata sisi Wabunge ulikuwa unatuhusu pamoja na wananchi lakini sasa katutua mzigo huu mzito. Kwa sababu tunafahamu kwamba malipo yale yanakwenda moja kwa moja kwa mzazi na wazazi wengi sana ambao wanaumia na haya mambo ni wanawake. Kwa hiyo sisi wanawake tunamshukuru kwa kututua mzigo huu na tunamtakia kila la kheri katika masuala ya uendeshaji wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende katika suala la ufutaji wa kodi. Tumeona kuna mambo mengi sana ambayo yamefutiwa kodi zake. Yapo yale ambayo yalipandishwa kodi zake kama masuala ya urembo kama vile nywele. Kwa kweli hili ni suala zuri kwamba Mheshimiwa Rais anataka tuwe natural. Kwa hiyo, hili suala nalichukulia kwamba ni zuri kidogo kwa sababu naamini kwamba haya masuala yatakapopandishwa kidogo kodi tutazidi kuwa natural, tutazidi kuwa wazuri na uhalisia wetu watazidi kuuona. Kwa hiyo nipongeze sana suala hili ambalo litaleta tija kwa watu wengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata wewe tunakuona hapa uko natural, kwa hiyo naamini kwamba ni jambo zuri la kuiga na ni jambo zuri ambalo hata wewe unatupa mfano na unapendeza. Kwa hiyo hili ni suala zuri na tuwapongeze kutaka kutupeleka huko kwa njia rahisi hii ya kupandisha haya mambo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, pia nipongeze sana kwa kufuta asilimia 40 ya tozo katika mashine za EFD. Hili ni jambo zuri kwa sababu wafanyabiashara wengi walikuwa wanalalamika kuhusu suala la ulipaji au ununuaji wa hizi mashine, lakini sasa hivi baada ya kufuta hizo tozo, naamini kwamba wafanyabiashara watakwenda kununua mashine zile na wataweza kuzitumia bila malalamiko, kwa sababu tunafahamu kwamba ukinunua unatakiwa udai risiti na ukiuza unatakiwa kutoa risiti. Kwa kauli mbiu hii ya TRA, naamini sasa inaenda kufanyika kiurahisi.
Mheshimiwa Spika, nimalizie…
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Zulfa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Nicholaus Matiko.
TAARIFA
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nampa taarifa tu Mheshimiwa Zulfa kwamba lengo la Serikali kuweka kodi kwenye hizi nywele bandia; mosi; ilikuwa ni kuhakikisha kwamba inalinda viwanda vya ndani. Hapa tunavyoongea kuna viwanda vya ndani ambavyo vinazalisha hizi nywele bandia. Sasa kwa kauli anayoitoa Mheshimiwa Zulfa ambaye amesema ni balozi wa kodi, akihamasisha watu wawe natural ina maana vile viwanda vyote vya ndani vitakufa na Serikali itakosa kodi, sasa sijui huo ubalozi utaenda wapi.
Mheshimiwa Spika, nilitaka kumpa taarifa hiyo tu. (Kicheko)
SPIKA: Mheshimiwa Zulfa, unaipokea taarifa hiyo?
MHE. ZULFA MMAKA OMAR: Mheshimiwa Spika, nafahamu kwamba viwanda vya ndani vinakusanya kodi, lakini sasa nirudie kumwambia dada yangu kwamba natural ni bora kuliko kwenda huko ambako anafahamu yeye. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)