Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Mwantum Dau Haji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa fursa hii. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia kuwa na hali ya uzima na afya. Pia nakushukuru wewe Mwenyekiti, kwa wakati huu kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia katika Bunge lako hili tukufu leo hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Waziri wangu wa Fedha kwa mpango wake huu aliouleta humu Bungeni ambao sasa hivi tunaweza kuuchangia Wabunge humu ndani, na sote tumesimama tunachangia suala hili lake kuhusu Mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu, naye anafanya kazi kubwa sana nchini, anafanya kazi kila mahali, Mwenyezi Mungu amjaalie hatua, ampe wepesi, ampe kila la heri na amuoondolee shari, ampe heri Inshaallah. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuendelea, nizungumzie suala la kuboresha huduma ya mama na mtoto. Huduma ya Mama na Mtoto, nashauri iendelee kutolewa. Akina mama wahudumiwe na akina baba, na hao akina baba waweze kuwahudumia akina mama. Maana ndiyo kama ninavyosema, tunawapenda sana akina baba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la watoto. Watoto wetu nao wanatakiwa kuhudumiwa, lakini kuna janga sasa hivi limejitokeza au tunasema changamoto. Kuna changamoto ya kiafya juu ya watoto wetu imeingia hapa nchini, nalo ni ugonjwa wa figo kwa watoto. Huu ugonjwa unaathiri sana watoto wetu huu. Ninavyokwambia watoto wengi wameshafariki kwa ugonjwa huu wa figo. Huu ugonjwa wa figo sio Watoto tu, hata sisi watu wazima; na huu ugonjwa unaleta changamoto ya haja ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaposhikwa haja ndogo unatakiwa ufukuzie kwenda chooni, kwa sababu unapohitaji kwenda haja ndogo, basi ile figo inaathirika mle ndani. Kwa hiyo, figo inaumia sana; lakini kwa watoto imezidi kuwaathiri. Kwa hiyo, kwa mpango huu, nasema kwamba wanawake tupewe kipaumbele pamoja na hawa watoto waweze kushughulikiwa ili hili janga lililojitokeza kuhusu figo litazamwe kwa kina. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la ulinzi; kuna suala la Mambo ya Ndani ya Polisi kwamba Polisi wanafanya kazi vizuri, wanaendelea kushughulikia mambo ya usalama nchini, wanafanya kazi kusema ukweli. Kutwa kucha wao wamo ndani kwa kutulinda sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Polisi ukiwatazama, wale watu wamekuwa wanyonge sana, hawana kipato cha kuweza kuwasaidia hawa ndugu zetu Polisi hasa wanapostaafu, mafao yao yanakuwa kidogo, hayawakidhi maisha yao wakasema kwamba hapa sisi tujenge au waweze kufanya miradi ya kuweza kuwasaidia mpaka hapo watakapofika kwa Mwenyezi Mungu. Fedha yao inakuwa ndogo. Kwa hiyo, katika huu mpango, namwomba Mheshimiwa Waziri, hawa ndugu zetu Polisi nao waweze kusaidiwa katika suala hili ili wafanye kazi vizuri na wajisikie kama wapo katika nchi yetu hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea, kuna ulinzi wa Jeshi hivi sasa. Hapa sasa! Ulinzi wa Jeshi nao niwapongeze; jeshi linafanya kazi vizuri, linatulinda, lipo kila pembe, lipo kila rika, wanaangalia kila mahali, lakini ukija ukazingatia Jeshi wanavyofanya kazi humu nchini, kwetu sisi ukiingia katika Mkoa wa Kusini kwenye Jimbo la Tunguu, kuna vijiji ambavyo vimevamiwa na Jeshi, ni kilio. Kuna sintofahamu kubwa sana ya wananchi kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiri, kuna eneo moja la Ubago lile limekwenda na maji, watu toka enzi ya ukoloni wapo pale; wamelima, wana minazi, wana majumba wamehamishwa hawapo, kilio kimewafika, hadi sasa hivi haijajulikana hii sitofahamu itafikia wapi? Siyo Ubago tu, ukija Dunga nako liko hilo suala, lakini siyo Dunga, mambo yote yapo hapo Kijiji cha Kikungwi. Kijiji cha Kikungwi Uwandani wapo wananchi wanalima ndimu pale, wana minazi, wana mazao mbalimbali kule wanalima. Matokeo yake, juzi tu wameambiwa wajiorodheshe majina. Wakajiorodhesha majina, kumbe kile Kijiji tayari kinachukuliwa na Jeshi.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuwalipa.

MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Eh!

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake kilichojitokeza, wale wananchi wanaendewa na wale Waarabu wanye madevu makubwa yanayoning’inia hapa, kweli hawa ni Jeshi? Hiki kijiji kweli kimevamiwa na Jeshi hiki? Kwa nini waende wale Waarabu? Ndio wanakwenda kule kuangalia na wanasema khel khel khel, wanazungumza mle. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wana sintofahamu, wanasema hiki kijiji pengine sio jeshi hawa, jamani kilio hiki Mheshimiwa Waziri hebu kama unaona uongo, tufuatane twende kwenye hicho Kijiji cha Kikungwi ukaone hali halisi iliyokuwepo kule. Hatari hii kwa sababu kila mahali Ubago, Jeshi; Nunga, Jeshi; sasa hivi Kikungwi, Jeshi; kuna Unguja Kuu, kuna Cheju, huko kote ni mahali pa Jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashangaa kwamba Kikungwi wamekwenda kuorodheshwa watu kuhusu mazao yao. Mwisho wa Habari, wanakwenda Waarabu sasa. Haya, tuseme nini hapo? Kweli hilo ndiyo Jeshi? Jamani Serikali, mwangalie, tusije tukavamiwa hapa, ikaja ikawa balaa imetutokea hapa, akina mama wenyewe kama mnavyotujua, hatuna nguvu hizo na wengi kule ndio wanaolima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu kwa mpango huu ipangwe siku waende wakaangaliwe wale watu kwenye Kijiji kile cha Kikungwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuhusu Watumishi wa Umma wastaafu. Kama ninavyokwambia, watumishi wa Umma wamefanya kazi Serikali hii miaka mingi mpaka wamefikia kipindi kile cha kustaafu, miaka yao 60 au 65 au 55, sheria ipo hiyo. Wamefanya kazi, lakini mwisho wa Habari, stahiki zao bado wengine mpaka leo hawajalipwa ingawa Serikali inawalipa. Naishukuru Serikali yangu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafanya kazi kubwa sana kuwalipa hawa wastaafu ambao walistaafu katika nchi yetu, lakini bado wanasikitika, wanasema mafao yao hawajapewa. Hili nalo naomba liangaliwe kwa kina, hawa wenzetu walipwe stahiki zao kwa mujibu wa sheria inayohusika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme, mimi hapa pamenitosha. Naunga mkono hoja asilimia mia moja kwenye bajeti yangu hii ya mpango iliyowasilishwa hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)