Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Mimi kwa pole mbili; pole ya kwanza, unapoisoma ile hali ya uchumi iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha jana asubuhi, unaona kabisa kwamba kuna mazingira magumu kabisa ya uendeshaji wa uchumi katika dunia; na kwa sababu Tanzania siyo kisiwa, nasi tumefikiwa na matatizo makubwa sana ya uendeshaji wa uchumi wetu hususan kutokana na matatizo haya ya UVIKO-19 na matatizo haya yaliyoletwa na vita vya Urusi na Ukraine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli naipa pole sana Serikali, lakini naunga mkono juhudi za Serikali ambazo zimetajwa na Waziri wa Fedha. Hongera sana kwa juhudi hizo, nakuunga mkono sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pole ya pili; ni ushawishi mbaya dhidi ya juhudi za Serikali kulinda rasilimali zetu hususan maliasili na utalii, hasa hasa kwenye eneo letu la Ngorongoro. Tunaona kwamba Rais amefanya juhudi kubwa sana, ameongoza filamu ya Royal Tour ili tuongeze watalii, lakini ushawishi mbaya unaweza ukasababisha watalii wakaogopa kuja Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana sana, tunahitaji kulinda maliasili na utalii wetu kwa nguvu zote. Hapa msisitizo niweke kwenye Ngorongoro, nikitoa takwimu kidogo. Hifadhi ya Ngorongoro ni sehemu ya ikolojia kuu tatu za hifadhi. Kwanza ni ikolojia ya Serengeti; pili ni ikolojia Nato-Longido and Events Amboseli na tatu ni ikolojia ya Manyara – Tarangire. Hizi zinahusiano wa moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikolojia hizo ni muhimu kwa mazalio na movements za wanyama wanaokaribia karibu milioni tatu kwa eneo hilo. Eneo hilo la Hifadhi ya Ngorongoro linatambuliwa na UNESCO kama urithi wa dunia. Kwa hiyo, ni lazima tuulinde urithi wa dunia ambao ndiyo urithi wa Watanzania wote. Maana yake tunapozungumzia habari ya maliasili ipo mahali fulani, siyo mahali hapo tu, bali maliasili hiyo ni ya Taifa zima. Kwa hiyo, kupinga juhudi za Serikali kama zilivyoelezwa humu Bungeni na Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hiyo haikubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije kwenye eneo la pongezi. Kwanza, nampongeza sana Mheshimiwa Rais na timu yake yote ya Mawaziri kwa utekelezaji mzuri sana wa Ilani ya Uchaguzi. Sisi tunatembea kifua mbele, hata Jimboni kwangu kule natembea kifua mbele, kwani miradi mingi imetekelezwa kwasababu ya mawasiliano mazuri kati ya Madiwani na mimi Mbunge na kati ya mimi na Serikali kupitia Mawaziri kwenda kwa Rais. “Usione vyaelea vimeundwa.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya watu wanajaribu kuwatoa Madiwani kwenye mafanikio, wasiwatoe Madiwani. Kuna watu wanamtoa Mbunge kwenye mafanikio, wasimtoe Mbunge. Kuna watu wanamtoa Rais; nasema hivi “usione vyaelea, vimeundwa.” Ushirikiano kati ya Diwani, Mbunge na Rais ndiyo umesababisha kufanyika yote hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi ya pili katika uchumi wa kisasa, ili tuendelee tunahitaji kuendeleza uwekezaji katika sekta za uzalishaji, biashara na viwanda, na sekta nyingine. Wawekezaji wanahitaji maeneo manne muhimu. Eneo la kwanza, wanahitaji gharama nafuu za usafiri na usafirishaji. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Serikali nzima kwa jinsi alivyowasilisha hapa mipango ya kujenga barabara, mipango ya kujenga reli, mipango ya kujenga bandari, mipango ya kujenga airport, mipango ya kujenga usafiri wa majini. Kwa hiyo, hongera sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ya pili, wawekezaji wanahitaji gharama ndogo za huduma za uendeshaji wa mitambo. Napongeza juhudi za Serikali katika kuboresha upatikanaji wa mafuta, kueneza umeme na maji. Haya yanahitaji wawekezaji. Eneo la tatu, wawekezaji wanahitaji malighafi ya uhakika. Napongeza juhudi za Serikali za kuboresha Sekta ya Kilimo ambayo bajeti ya kilimo imeongezwa, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji wanahitaji wafanyakazi wenye ujuzi. Kwa hiyo, napongeza sana juhudi za Serikali kupitia hotuba ya bajeti ambayo imesema itajenga vyuo vya ufundi katika Wilaya zote vyuo vya VETA, hongera sana. Naipongeza Serikali sana sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napongeza Serikali kuondoa mfumo wa mapato kwenye sheria ya kodi. Nawapongeza Serikali kuboresha mfumo wa ununuzi wa umma kwa ajili ya kupunguza udanganyifu, hongera sana. Nawapongeza Serikali kuendeleza matumizi ya TEHAMA kwenye kazi za Serikali ili kupunguza matumizi, hongera sana. Napongeza juhudi za Serikali kuanza maandalizi ya Sera ya Taifa ya ufuatiliaji wa Tathmini, naipongeza sana. Naipongeza Serikali kuboresha ukaguzi wa ndani na kujenga uwezo zaidi wa CAG, napongeza sana sana, hongera sana! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nina maeneo matano ya ushauri na ninaomba mnisikilize. Eneo la kwanza ambalo nashauri; Serikali imeondoa ada ya Kidato cha Tano na cha Sita; hiyo ni safi kabisa, hongera sana. Ila wakati wanapofanya uchaguzi wa vijana kwenda Form Five na Form Six, ndiyo kipindi hicho hicho Serikali hufanya uchaguzi wa vijana wanaokwenda kusomea kozi za kati za ujuzi. Kwenye vyuo vya kati; kwa manesi, mafundi maabara na nini, hao nao wanahitaji msamaha wa ada, tumewasahau. Naomba sana Serikali izingatie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili; Serikali imependekeza kupunguza asilimia 10 ya mikopo ya akina mama walemavu na vijana kwenye Halmashauri. Kama unatoa asilimia tano Sikonge unaileta kwenye TAMISEMI halafu ikajenge soko la wamachinga Dodoma Mjini, hapa unakuwa hujawatendea haki watu wa Sikonge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba yale majiji na manispaa ambayo wana mipango ya kujenga hayo mabanda ya wamachinga, ndiyo hao wapatiwe hiyo asilimia tano iende kule, lakini Halmashauri za Wilaya ambazo hazina mpango wa kujenga mabanda ya wamachinga, waachiwe asilimia 10 zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa tatu; wakulima wanapouza mazao yao, naomba walipwe ndani ya wiki moja. Kule Sikonge imejitokeza wakulima wa tumbaku wameuza mazao yao mwezi wa Tano, kuna mtu anatangaza anasema watalipwa mwezi wa Nane. Naomba sasa Serikali iingilie kati wakulima wetu walipwe haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne; wananchi wa vijijini wanaotaka kupimiwa ardhi zao, labda wanahitaji mikopo kwenye benki, hawawezi kupima ardhi zao. Naomba sana Waziri wa Fedha anapoleta Finance Bill aainishe maelekezo kwamba anaelekeza kupitia Sheria ya Fedha kwamba mtu yeyote anayetaka kuwekeza vijijini kwa kuomba mkopo, ardhi yake ipimwe bila kusubiri mpango wa matumizi bora ya ardhi ya Kijiji iishe, isipokuwa tu maombi yake yawe yameidhinishwa na Mkutano Mkuu wa Kijiji, Halmashauri yake pamoja na Mkuu wa Wilaya, hapo apimiwe ili kusudi tupate maendeleo vijijini na watoto wa vijijini waweze kukopa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kwa uratibu wa Mkuu wetu wa Mkoa; tuna Mkuu wetu wa Mkoa mzuri sana, siyo kwa sura tu, hata kwa kazi, Dkt. Batilda Buriani anafanya vizuri. Ameanzisha mpango wa kujenga Chuo Kikuu cha Tabora. Wale ambao wanafahamu historia ya elimu ya nchi hii, watakubaliana nami kwamba Chuo Kikuu cha Tabora kilikuwa kijengwe miaka 50 iliyopita. Sasa kwa sababu tumechelewa, naomba Serikali iunge mkono juhudi za Mkuu wetu wa Mkoa kujenga Chuo Kikuu cha Tabora haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii. Naunga mkono hoja. (Makofi)