Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kondoa Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango pamoja na Bajeti hii ya 2022/2023. Kwanza niipongeze Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza vilivyo Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kutuletea mpango ambao kwa kweli umekwenda kuwagusa wananchi wa maeneo yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuanzia mwanzo mpaka mwisho sijaona mahali pameelezea japo kwa ufupi Sekta ya Ardhi. Kwa hiyo, naomba angalau wakati Mheshimiwa Waziri anakuja ku-windup japo atuletee maelezo mafupi kuhusiana na Sekta ya Ardhi kwa sababu shughuli zote za kiuchumi zinafanywa kwenye ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ardhi hii inaipa nchi kipato kikubwa sana, kwa sababu ardhi iliyopimwa ina uwezo wa kuchangia kipato kikubwa sana kwenye Taifa hili. Moja, wakati wa mauzo ya ardhi Serikali inapata fedha, pia wakati wa kodi ya viwanja na wakati wa malipo ya kodi ya majengo. Kwa maana hiyo, tupate japo maelezo kidogo tuone namna gani Wizara hii inakwenda kuweka umuhimu wa sekta ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya vizuri sana kwenye Sekta ya Ardhi. Leo Serikali imetoa mikopo kwa ajili ya halmashauri kwenda kupima ardhi zao. Halmashauri nyingi zimenufaika kwa mikopo ya Serikali. Mwezi huu tu Wizara ya Ardhi imeweza kukopesha halmashauri mkopo usio na riba wenye thamani ya shilingi bilioni nne kwa halmashauri nne. Kwa maana hiyo, sekta hii ni muhimu sana na Wizara inafanya vizuri sana kuhakikisha maeneo haya yanapimwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la Sekta ya Utalii tumeona namna gani watalii wameongezeka kutokana na filamu ya royal tour na tuna habari kwamba Zanzibar imejaa wageni, lakini hata Bara wamejaa wageni kutokana na royal tour. Sasa sisi kama Taifa tunatakiwa sasa katika mipango yetu ya ndani tuhakikishe ujio huu wa wageni wengi usikome na uendelee muda wote. Utaendelea vipi? Ni kwa sisi wenyewe kupanga mikakati yetu ya ndani kuanzia tunapoweza kumpokea mgeni anapoingia mpaka wakati anaondoka, kiasi kwamba wakati anaondoka atamani tena kurudi ama atamani kwenda kushawishi wageni wengine waje kuitembelea nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunapaswa kutoa vikwazo vyote ambavyo vitakuwa ni kero kwa wageni wetu. Kwa hili naamini Wizara itafanya vizuri na itahakikisha kazi kubwa iliyofanywa na Mheshimiwa Rais itaendelea vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoongelea Sekta ya Utalii katika nchi hii, ni sekta ambayo inachangia katika pato la Taifa zaidi ya asilimia 17. Ni sekta ambayo imetoa ajira zaidi ya wananchi wa Tanzania 1,600,000. Kwa hiyo, ni sekta muhimu sana. Kwa hiyo, sisi tunapoiongelea Wizara ya Maliasili, tunatakiwa tuongelee Wizara kwa umakini sana kwa kujua kwamba Wizara hii imebeba uchumi mkubwa wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mawazo yoyote ya mtu yoyote ambayo yanaenda kwenda kuudumaza utalii wetu tuyakatae kwa nguvu kubwa sana. Ukishateuliwa na Mheshimiwa Rais kwenye sekta hii, katika Wizara hii usitegemee utasifiwa kwa sababu Wizara zote zinawatetea wanadamu, wewe peke yako utakuwa unatetea wanyama. Kwa maana hiyo, hakuna nafasi ya kusifiwa, unachotakiwa kufanya ni kusimamia sheria kwa ajili ya kulinda urithi wetu ambao sisi tumerithishwa na Watanzania, watoto wetu na wajukuu zetu watatamani kwenda kuona hivyo ambavyo tumevitunza tukarithishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda Sekta ya Ujenzi. Kuna jambo moja hapa ambalo nataka Bunge lako liweke sawa. Tuna Ilani ya CCM ambayo imeandaliwa vizuri sana na viongozi wetu makini na nina uhakika Ilani ile ni Ilani bora sana na ikitekelezwa tunakwenda kumuinua mwananchi mmoja mmoja. Sasa katika ujenzi lengo la CCM ni kuhakikisha wanaendelea kujenga barabara ili kuwawezesha wananchi waweze kujijengea kipato chao na maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hii barabara ya Handeni inayokwenda mpaka Singida. Barabara hii nimepata mashaka kidogo, kwanza kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameitaja vizuri barabara hii. Amesema kwamba barabara hii ya kilomita 460 itaanzia Handeni – Kibrashi – Kibaya na kwenda mpaka kwa Mtoro, lakini katika Mpango wa Serikali pia umetaja kama alivyotaja Waziri wa Fedha, hii haina mashaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro unakuja kwenye taarifa ya Wizara ya Ujenzi, wao waliitaja kwamba inatokea Handeni – Kibirashi – Kijungu – Kibaya – Njoro – Ugoloti – Mrijo Chini – Dalai – Bicha halafu inarudi tena Chambalo inakwenda tena Chemba ndiyo iende kwa Mtoro halafu Singida, jambo hili ambalo haliwezekani. Ni kwamba barabara imezungushwa eneo moja lilelile ambalo nadhani Ilani ya CCM ambayo ndiyo ilitaka Serikali ijenge ile barabara, imeeleza vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Ilani ya CCM ukurasa wa 73 imetaja kwamba barabara hii itajengwa kuanzia Handeni - Kibirashi – Kondoa kwenda Singida wakifahamu kwamba, barabara hii ni barabara ya TANROAD ambayo ilikuwepo miaka mingi na ndiyo inafahamika. Barabara hii inatakiwa ijengwe kuanzia Handeni – Kibirashi – Mrijo Chini iende Dalai, iende Mondo, iende Bicha, iende Selya ikatokee kwa Mtoro ndizo hizo kilomita 440 zitatimia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mpango huu na nilikwenda kuonana na Naibu Waziri wa Ujenzi, yeye pia ana mpango wake, ambao mpango wake niliona unakata vijiji na mitaa mingi sana inaishia nyuma ya kijiji ambacho kinaitwa Dalai, halafu inakwenda Chemba halafu ndiyo inakwenda kwa Mtoro, Ilani ya CCM haijasema hivyo. Ilani ya CCM imesema barabara hii inakwenda Kondoa halafu ndiyo kwa Mtoro, halafu ndiyo ufupi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukitokea Kondoa kwenda Singida kwa njia ya Kwa Mtoro haizidi saa moja na robo, lakini kwa namna Wizara ilivyosema, ukitokea Kondoa kwenda Singida kwa barabara hii wanayoisema ni zaidi ya masaa manne. Kwa hiyo, utaona kwamba barabara hii inatakiwa Mheshimiwa Waziri akija, atamke ili wananchi wa Dalai, Mondo, Bicha na Selya wajue kwamba mpango wa CCM kwenye Ilani yake utatekelezwa kama namna Ilani ilivyosema.
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu wakati vikao vya chama vinapendekeza barabara hiyo ni kama vilijua. Barabara hii ndipo Mradi ule wa Bomba la Mafuta unapopita. Sasa ukiikwepesha barabara hii maana yake shughuli nyingi za uchumi zitakwama. Kwa maana hiyo, barabara hii ni muhimu kwa sababu kuna bomba la mafuta na kuna kituo kikubwa ambacho kitajengwa katika Kata ya Selya. Kwa maana hiyo, kutokuitendea haki barabara hii kutasababisha kwamba mengi kutoenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu barabara hii ya TANROADS ndiyo barabara ambayo itapokomea hapo Selya itakuwa inaelekea Usandawe ambako ndiko huko kwa Mtoro. Hapa inapokomea ni barabara ya TANROADS ambayo inakwenda kuunganisha na Hanang’. Tunafahamu Hanang’ ni wakulima wazuri wa zao la ngano. Sasa kuzunguka kwenda Moshi mpaka Tanga kwenda Dar es Salaam au Singida kuja Dodoma – Morogoro watakuwa wanatembea kilomita zaidi ya 600, lakini kwa kupitia Kondoa ni hizi hizi kilomita 460.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, naunga mkono hoja, lakini Mheshimiwa Waziri akija atuelezee kwamba CCM ilivyopanga kwenye Ilani ndicho kitakachofanyika kwenye barabara hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)