Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri, lakini pia kwa namna ambavyo hotuba imejielekeza kwenda kujibu kero za msingi ambazo zilikuwa zinasumbua hasa katika maeneo ambayo nimeona kwenye eneo la uvuvi ambalo nina interest nalo na eneo la madini. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Rais hasa kwa kuondoa kwa kweli utaratibu uliokuwa unatumiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania, pamoja na kazi yao nzuri ya kupitia mahesabu ya nyuma, hii watu wengi sana sio tu walikuwa wanapata tabu, lakini ukweli ni kwamba ukiniambia nitoe hesabu ya miaka kumi, miaka sita iliyopita lazima litaishia kwenye mazungumzo na ninayefanya naye hesabu. Kwa hiyo namshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuliona hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali mwezi huu ilitoa bilioni mia moja kwa ajili ya ku-control bei ya mafuta na kusaidia kupunguza mfumuko wa bei. Naipongeza sana Serikali kwa hatua hiyo, lakini kama ambavyo watu wengi wanataka kujua bado tuna hamu ya kufahamu ufanisi wa jambo hili. Mimi ambaye ninatoka katika Kanda ya Ziwa, pamoja na jambo kubwa hili ambalo Serikali imefanya bado hatukuona kimsingi ile impact kubwa ya hii fedha ambayo imewekwa na nadhani kuna haja ya kuwa na transport equalization fund ili kumfanya Mtanzania anayeishi Dar es Salaam, ugumu ya maisha na urahisi wa maisha yake usitofautiane kwa kiwango kikubwa sana na mtu anayeishi Kagera, Kigoma na Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kutoa mfano, kwamba pamoja na fedha hizi zote kuingia, lakini kule hazijasaidia sana kupunguza gharama za usafiri, zimebaki pale pale, bado mfuko wa sementi Geita Mjini ni Sh.24,000, lakini utaona Dodoma hapa ni Sh.15,500 kwa hiyo inaona katika nchi moja kuna tofauti ya Sh.9,000, lakini ukiuliza sababu ni gharama za usafiri. Kwa hiyo kuna haja ya kulitazama jambo hili vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri kwa kufuta ada ya kidato cha tano. Hili ni jambo kubwa sana na laiti Serikali ingejua namna ambavyo Wabunge inapofika muda wa kufungua shule tunavyohangaika kuwalipia watu, basi jambo hili limetusaidia sana. Hata hivyo, niombe ombi moja, bado tuna shida kwenye vyuo vikuu, bado tunatoa fedha kwenye vyuo vikuu kwa kutumia zile lettings na vigezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kushauri kwa sababu mkopo wa chuo kikuu ni mkopo, madam nataka mkopo na nimejaza fomu ya kuomba mkopo habari ya kuangalia nani anastahili na mwingine hastahili kukopa hili jambo lingeangaliwa vizuri sana ili iwe ni haki ya Watanzania wote waliopata sifa ya kwenda kusoma wapate mkopo. Sasa hivi hiyo mean testing yao inamwacha mtoto yatima, ninao watoto wawili ambao ni yatima, lakini kwa bahati mbaya walipata wafadhili kusoma na wafadhili waliowafadhili walishakufa, kwa hiyo hawawezi tena kwenda kusoma na wameshindwa kusoma kwa sababu wamekosa mkopo. Nimejaribu sana kwenda kwa Mkurugenzi wa Bodi lakini ilishindikana, kwa hiyo jambo hili liangaliwe vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo nimeliona kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri, amezungumzia sehemu ambapo anaomba Bunge limpe ridhaa ya kusamehe baadhi ya kodi, niipongeze sana Serikali hasa Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo anazunguka huko nje na kutengeneza picha ambayo inavutia wawekezaji kuja Tanzania na hili ni jambo zuri sana. Hata hivyo, ni lazima twende na tahadhari kubwa, tumekuwepo na harmful tax incentives ambazo kimsingi hazijawahi kuisaidia nchi. Ukiangalia huko nyuma kote ambako tulikuwa tunalalamikiwa kwamba Serikali inapoteza trillions of moneys ni kwa sababu ya misamaha mikubwa ya kodi ambayo tulidhani inavutia wawezekaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, wawekezaji wanakuja kwa mambo makubwa, yapo machache. La kwanza, wanakuja kwa sababu ya hali ya usalama. Pili, wanakuja kwa sababu ya kutabirika kwa nchi ile (predictability) yaani kama nchi inakuwa na sera zisizotabirika tabirika mwekezaji hawezi kuja. Tatu, anakuja kama infrastructure na energy supply ni kubwa. Nne, anakuja kama kuna masoko na human resource. Sasa unaweza ukaweka incentive ya fedha haijawahi kusaidia kumfanya mwekezaji aje, kwa sababu mwekezaji anakuja kwenye eneo hata ambalo wewe hujampa incentive kama anapata profit anakuja. Kwa hiyo hili ni angalizo ambalo inatakiwa kuliona. Kwa sababu juhudi kubwa hizi zinafanywa na Serikali, lazima pia tuangalie kwenye mianya ambayo tunaweza tukajikuta tunapoteza fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye eneo ambalo sasa hivi linatupatia fedha nyingi za kigeni la madini. Tunafanya vizuri sana kwenye madini, lakini bado tuna shida moja kwenye madini. Niliwahi kusema hapa kwamba, haya madini tunayoona kwa wachimbaji wadogo wanayauza mpaka anapata labda gramu moja ameshakula hasara yenye thamani ya gramu 10. Sasa hapo niombe mambo mawili; moja tuimarishe sana GST na watu wa STAMICO ambao wanafanya mambo ya utafiti, lakini tubadilishe mfumo wa kutoa leseni kwa gharama ile ile. Unakuta mtu amepewa leseni anachukua leseni ya PML, SML, MML anaitunza kwa miaka 20 kwa kulipa fee tu kumiliki leseni. Wenye leseni walazimishwe kufanya utafiti halafu tuweke rates za leseni kulingana na deposit au value ya kitu kilichopo pale chini, ili huyu mtu kama akichelewa kulipa kwa miaka mitano aone gharama ya kutunza ile leseni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, niende kwenye utalii, naomba kumpongeza sana Mheshimiwa Rais hasa kwa filamu hii ya kuitangaza Tanzania. Ukweli ni kwamba Watanzania wengi hatufahamu kwamba nchi yetu huko nje ilikuwa haijulikani. Tulipata bahati hapa, Mheshimiwa Spika alitupeleka nje tulikwenda China, tumefika kule mtu ukisema Tanzania lazima a-google kuitafuta ilipo, halafu akitazama pale mtu wa kwanza anayemjua ni Nyerere, basi anasema Oooh! Nyerere’s country basi. Kwa hiyo, kuna watu duniani hawajui kama Tanzania ipo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuitangaza.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa juhudi hizi za kutangaza Tanzania na kuvutia watalii zinakuja sambamba na maandalizi tuliyonayo. Jambo kubwa sana amesema hapa Mheshimiwa Sima asubuhi, duniani huko watalaii wanataka kwenda kwenye nchi ambayo usalama ni wa uhakika. Kwa hiyo, jambo la usalama ni la msingi sana. Tetesi zozote zinazoashiria kutokuwepo kwa usalama zinamfanya anayefikiria kuja Tanzania asije na ukiona kama jirani yako au mwenzako yeyote anatangaza sana ubaya wa usalama kwenye nchi yako, maana yake hiyo tayari ni vita ya kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapa ni lazima tuangalie vizuri. Naiomba Serikali jambo hili isilichukulie poa, kwenye biashara ya utalii hakuna mtu atakwenda kwenye nchi ambayo ana taarifa za kwamba wananchi wanapigana na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la pili ni ukarimu. Tanzania lazima tujue kwamba ili tuweze kuwapokea watalii wengi lazima tufanye maandalizi. Maandalizi haya ni pamoja na kulinda maeneo yetu ya asili, na pili kuandaa sehemu za kuwapokea. Sasa ipo shida kidogo ambayo niliiona juzi hapa na ninaomba niseme vizuri, inaweza kuwa ni misconception au ni misleading ambayo imetokea kwa wananchi wa Loliondo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachotakiwa kufanyika kwenye eneo lile siyo kuigeuza Loliondo nzima ile ya square kilometa 4,000 kuwa game reserve. Ni kiini cha Lake Natron na sehemu ndogo ya square kilometa 1,500 kwa sababu kubwa mbili. Moja, lile ziwa kuna ndege ambao wanakuja kuzalia pale na wanakwenda Ulaya, lakini limeendelea kupata seriation kutokana na uingiliaji wa watu. Kwa hiyo, lazima tulinde nusu ya lile eneo. Naipongeza sana Serikali kwa juhudi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, wanyama wote unaowaona, wana maeneo maalum ambapo huwa wanakwenda kufanya mazalia na maeneo ya mtawanyiko. Kwa hiyo, kale kaeneo lazima ukalinde. Sasa inawezekana kuna taarifa zisizo sahihi ambazo zinasambaa za kufikiri eneo lote lile zima wananyang’anywa wananchi na kupewa wawekezaji, jambo ambalo naamini siyo sahihi. Kwa sababu maandalizi ya andiko hilo yalifanywa na wizara na yakapelekwa kwa viongozi na yakafanyiwa kazi vizuri. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, elimu ya kutosha ipelekwe eneo hili, watu wasipewe picha ambayo siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la nne, ambalo nataka kuzungumza ni eneo la uvuvi. Miaka ya nyuma tulikuwa na TAFICO na nimeona hapa Mheshimiwa Waziri umeweka TAFICO unataka kuwapa fedha. Mimi nilipata bahati ya kusoma uvuvi na nilipata bahati ya kufanya field TAFICO, sielewi mnakwenda kufanyaje TAFICO ili ije kutusaidia kutoka kwenye mchango wa kiuchumi. Maana yake sasa hivi uvuvi unachangia chini ya 3% kwenye GDP.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni aibu sana. Miaka ya nyuma, mwanzoni mwa mwaka 2000 uvuvi ilikuwa ni kwenye export; kwenye forex ilikuwa ni zao la pili Tanzania kwa kuingiza fedha za kigeni. Tumekuja tukavuruga wenyewe. Nimeona hapa umetoa exemption ya nyavu, hakuna kodi, lakini tulivuruga wenyewe. Wawekezaji wenye viwanda ndiyo walikuwa wanaleta nyavu. Wakileta nyavu, wanawauzia wavuvi. Sasa zote zikakamatwa, zikachomwa moto.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ombi langu hapa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tutengeneze sera ambazo siyo kila atakayekuja kwenye Wizara hii atabadilisha ili wavuvi waweze kuvua vizuri.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Kanyasu. Ni kengele ya pili, ahsante sana.

MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)