Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia katika bajeti hii kuu. Naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa utendaji wake mzuri sana uliotukuka. Kimsingi Mheshimiwa Rais anafanya vizuri sana katika sekta mbalimbali. Amejipambanua hivyo kama mwanamke mahiri ambaye kimsingi sisi kama Watanzania tunajivunia yeye kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nimpongeze sana Waziri wa Fedha kwa namna ambavyo amekuwa akifanya kazi nzuri ya kumsaidia Mheshimiwa Rais pamoja na viongozi wengine waandamizi; Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na pia nampongeza sana Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha pamoja na delegation yote. Mnafanyakazi nzuri sana, Mungu awatangulie katika utekelezaji wa majukumu yenu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na kazi zote zinazofanywa na Mheshimiwa Rais za kuhakikisha kwamba maendeleo ya nchi yetu ya Tanzania yanaendelea kukua, lakini pia ipo haja ya kuangalia vizuri zaidi masuala mazima ya usalama katika nchi yetu. Ninavyosema hivyo ninamaanisha. Zipo barabara za pembezoni ambazo zinaunganisha nchi ya Tanzania na nchi nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii nitaizungumzia barabara ya Chiwindi mpaka Lumesule yenye kilometa 535. Barabara hii ni barabara ambayo inapita pembezoni mwa Mkoa wa Ruvuma kwenye Mto Ruvuma ambapo sasa Mkoa wa Ruvuma ndio kiunganishi cha nchi ya Mozambique. Kwa misingi hiyo, ninaizungumzia hii barabara kwa sababu ni barabara ya kiulinzi na kule Mkoani Ruvuma Mkuu wetu wa Mkoa ni Mwanajeshi. Kwa hiyo, mara zote amekuwa akiomba sana hii barabara iweze kutengenezwa kwa ajili ya kusaidia masuala ya ulinzi katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni kwa sababu barabara hii inaungana na Mkoa wa Niassa, siyo Nyasa; Mkoa wa Niassa wa Nchi ya Mozambique, katika Jimbo la Niassa nchini Mozambique ambako sasa hivi kumekuwa na tishio kubwa sana la vikundi mbalimbali vya ugaidi. Kwa hiyo, ndugu zangu naomba sana hii barabara iende ikaanze kutengenezwa kwa kiwango cha lami ili kuweka mazingira mazuri ya masuala ya ulinzi katika maeneo hayo. Tusisubiri mambo yakaanza kujitokeza halafu ndiyo tunagundua shuka wakati kumekucha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie suala la pili ambalo linahusu Ngorongoro na Loliondo. Ngorongoro ilianzishwa mwaka 1959 na Ngorongoro hii kimsingi ndiyo maeneo ambayo yana mfumo wa ikolojia ambapo maeneo mahsusi katika yanatambulika kwa majina haya yafutayo: Natron, Longido, Enduimet na mfumo huu wa ikolojia unakwenda mpaka Manyara na Tarangile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa eneo hili la Ngorongoro ulitambulika mwaka 2010 eneo hili sasa limetambuliwa kama ni eneo la urithi wa dunia. Kwa misingi hiyo, na kwa umuhimu wake, kuna mambo ya urithi wa kidunia lakini pia kuna mambo ya kitamaduni. Kipekee kabisa, naomba nitaje baadhi ya vitu ambavyo vinapatikana hapo Ngorongoro pamoja na kwamba baadhi ya Wabunge wamezungumza vitu vingi vinavyopatikana, nami nitataja vichache.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna creator tatu kubwa ambazo zipo pale Ngorongoro, lakini pia kuna wanyamapori wa kila aina pale Ngorongoro wakiwemo ndege wa aina mbalimbali. Pia kuna mchanga mweusi pale Ngorongoro na huo mchanga una tabia ya kuhamahama. Mchanga wa aina hii huwezi kuupata mahali pengine popote pale duniani, unapatikana Ngorongoro tu. Kwa hiyo, ni vitu muhimu sana vya kuvilinda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie kuhusu Mheshimiwa Rais namna ambavyo amejikita kwenye suala la Royal Tour na amefanya vizuri sana katika eneo hili na wengine wamesema katika kutangaza nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitaje faida kubwa ambazo zimepatikana mpaka sasa hivi baada ya Mheshimiwa Rais kujitoa na kuhakikisha kwamba anatangaza kupitia hii video ya Royal Tour. Mambo ambayo tumefanikiwa kwa sasa hivi nataka niseme, watalii wameongezeka na wamekuwa wengi sana sasa hivi na viashiria vya kuongezeka kwa watalii vinapatikana hapa ambapo tunaona kabisa kumekuwa na ongezeko la watalii ambao wameshafanya booking kwenye zile hoteli ambazo zipo huko Mbugani. Mwaka mzima huu hakuna nafasi, kupo full booked. Kwa hiyo, hii ni moja ya viashiria kwamba utalii unakua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kumekuwa na wawekezaji wa mitaji mbalimbali. Wawekezaji wa masuala ya hoteli wamejitokeza wengi ambao wanahitaji kuwekeza katika eneo la Ngorongoro. Kuna kampuni ya Mariot na kiwanda kikubwa sana cha Wachina ambapo wanakuja kwa ajili ya kutengeneza magari, wana-reassemble magari ambayo yatakuwa ni special kwa ajili ya watalii. Kwa hiyo, hivi ni viashiria vikubwa sana kwamba uchumi wetu unakua. Pia kupikia suala la Ngorongoro, napo pia tunanufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuongezeka kwa mashirika mbalimbali ya ndege; kwa mfano, kuna Air Qatar ambapo kwa kipindi cha wiki moja wanaweza wakafanya trip mpaka 15. Pia tumeona Mheshimiwa Mbarawa, amekubaliana na nchi ya Marekani ya kwamba ndege zipelekwe Marekani zitoe watalii Marekani moja kwa moja wanaenda kutua maeneo husika; na maeneo ya Ngorongoro kwa ajili ya kuboresha masuala ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niseme hivi ndugu zangu, tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri hii ambayo ameifanya. Pia wamekuwa wakijitokeza watu ambao hawaitakii mema nchi yetu na kwamba suala la utalii sasa hivi kwa kuwa ajenda kubwa ni kukuza utalii katika nchi yetu ya Tanzania kutoka watalii 1,500,000 hadi kufikia 5,000,000 ifikapo mwaka 2025, kwa hiyo, ajenda hii iliyofanyika ya Royal Tour kwa vyovyote vile imewastua hata majirani zetu kwamba eneo hili linaendelea kukua kwa kasi, na ushindani huu umekuwa ni mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana wale watu wote wenye nia mbaya ya kutaka kudhoofisha ajenda hii ya utalii ambayo imefanywa na Mheshimiwa Rais, kwa kweli tuwapige vita vibaya sana wasiweze kupata nafasi yoyote ya kuweza kuchukua huu uhalisia uliopo wa kupambana dhidi ya masuala ya uchumi kupitia utalii na baadaye wakaenda kujinufaisha wao kwa namna moja au nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninawalaani wapotoshaji wote katika mitandao ya kijamii, na hao wote wanaopotosha kwa namna moja au nyingine hawana tofauti na maharamia. Kwa hiyo, tusichukulie poa kama ambavyo wengine wamesema.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nataka kuzungumzia suala la EPZ. Kumekuwa na suala la EPZ, kuchukua maeneo mbalimbali katika nchi yetu. Maeneo haya wanayahodhi kwa muda mrefu likiwepo eneo la Kata ya Mwengemshindo katika Mkoa wa Ruvuma, Wilaya ya Songea Mjini wamechukua eneo la EPZ. Mpaka sasa hivi ni takribani miaka 14 wananchi wale wamekaa hawajui hatma yao, hawaelewi wafanye nini na wamezingirwa na vichaka, hawawezi kufanya maendeleo ya jambo lolote lile.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante. Ni kengele ya pili.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)