Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na niwashukuru ndugu zangu wa Wizara hii, lakini kwa ujumla wake nilifarijika niliposikia kwamba hawataacha kupeleka fedha katika maeneo yetu hata kama tutakuwa tumepata hati chafu. Jambo hili ni jema na yule aliyehusika kupelekea hati chafu ndiyo aadhibiwe, wananchi waendelee kupelekewa maendeleo, hilo ni jambo zuri na ni jambo lenye afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya kwanza kama si 2015 nilisimama hapa nikaendelea kuongelea habari za utalii, lakini habari za Ngorongoro. Bahati nzuri kipindi hicho nilikuwa ni Mjumbe wa Kamati hiyo wa mambo ya Maliasili na Utalii. Nilitembelea Ngorongoro, nilitembelea Loliondo, moja kubwa ambalo niliwahi kulisema wakati ule na nitalisema leo, bila utashi wa kisiasa hatuna Ngorongoro, bila utashi wa kisiasa hatuna Loliondo. Niseme, leo tunaiona hiyo Ngorongoro nzuri, Loliondo nzuri ni kwa sababu imehifadhiwa, bila uhifadhi hatuna maeneo hayo. Leo utatamani ni kwa sababu tumehifadhi, lakini tusipohifadhi ni eneo kama eneo lingine lolote, lakini kwa kupitia uhifadhi ndiyo panapata heshima hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana na tusisahau hiyo kauli nimemsikia hata mwenzangu mwingine akiongea hapa, mazingira yaliyoharibiwa hayana huruma, yatakuadhibu tu hata kama ni miaka hamsini ijayo. Kwa hiyo, hilo Mheshimiwa kwa unyenyekevu mkubwa sana naomba tusilisahau. Katika eneo la utalii bosi wetu kafarijika kwa masuala ya Royal Tour na vitu vingine, lakini bosi wetu na naomba hapa tuelewane vizuri, atafanya yote, lakini katika eneo la utalii, bosi wetu ni mtalii na usipotii kiu yake haji, usipotii kiu ya mtalii haji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu anahangaika, anakusanya fedha zake kwa muda mrefu ili kuja kutembea Tanzania, kwa hiyo wewe usipotii kiu yake, usipotengeneza mazingira rafiki haji, ana uwezo wa kwenda sehemu nyingine yoyote. Hapa naomba tuendelee kuelewana vizuri, yawezekana sisi kama Tanzania, kama nchi, leo nafarijika, kuna baadhi ya maeneo huko duniani vyanzo vyao vya utalii labda ni jengo refu, kitu cha namna hiyo, sisi Mungu ametupa zawadi ya pekee, leo hii fanya ufanyavyo hata kama utaweza yasukume maji kama ambavyo wengine wamesukuma maji ya bahari ya hindi but thus not Ngorongoro, fanya ufanyavyo hata kama utatumia grader kupalilia viwanja kama 10 au 15 but that is not endless plains kwa maana ya Serengeti. Serengeti ina namna ya pekee, Ngorongoro ina namna ya pekee, hao wenzetu wengine vitu vyao ni artificial, vya kwetu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo, zawadi hii isiwe laana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tabia ya Mtalii nimesema usipotii kiu yake haji na naomba hapa tuelewe vizuri, kuna matabaka ya watalii. Wakati tumejipanga vizuri kabisa kwenda kuimarisha utalii wetu, kutangaza utalii wetu, vipi kuhusu sekta nyingine, naomba sana, kuna eneo hili, je, tumejipanga vizuri kwa maana ya trained personnel, watu ambao wapo well trained, kwa sababu kuna mtalii wa madaraja, achilia kuna mtalii wanamwita labda mtalii kishuka, mtalii ambaye tunabanana wote huku huku, mahindi ya kuchoma na vitu vingine vya namna hiyo, lakini kuna mtalii anakuja anauliza je, kama nime-fall sick, nimeugua napata wapi tiba? Je, kama nchi tumejiandaa kwa hilo? Nitatibiwa wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, isije kuwa tumetengeneza vizuri, tumeimarisha utalii wetu, lakini ikitokea amekuja mtalii wa kiwango hicho, unaanza kuzungumzia habari ya flying doctors labda tumsafirishe kumpeleka nchi ya Jirani, maana yake nini? Mmepambana kuinua utalii lakini inapokuja ni suala kama hilo kwamba you are finding flying doctors ili kumpeleka nchi za jirani. Kwa hiyo, maana yake tujipange kwenye maeneo mapana zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanashindwa kuelewa jambo dogo kwa maana ya customer care. Leo hii kuna baadhi ya nchi ukifika tu uwanja wa ndege hata jinsi taxi drivers wanavyokupokea, inakupa nafasi ya kujua kwamba hapa napokelewa. Katika maeneo hayo wenzetu wa Wizara watengeneze mazingira, waandae watu wetu hata kama ni kwa kupitia semina tuwaandae watu hawa. Nimezungumzia habari ya well trained personnel, waiters and waitresses, watu hawa wakiwa well trained hata kama ni kwa semina, najua ni chanzo cha mapato kwa sababu mtalii huyo ambaye atakuwa amehudumiwa vizuri hawezi akaikimbia nchi hii, lakini hawa watu ambao ni well trained wana uwezo wa kuiuza nchi hata katika sekta nyingine. Unakutana na mtu anakwambia Tanzania hii tuna madini haya, tuna haya, lakini sio mtu unakutana naye, ndiyo kwanza anasema kama hutaki acha. Tunawaandaje watu wetu? Hili ni jambo la msingi sana hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo, naomba niende katika sekta nyingine ambao ni eneo la madini. Naomba ifahamike vizuri, madini ya Tanzania, utajiri tuliopewa na Mungu, hatuko peke yetu. Hata kama ni dhahabu, hatuko peke yetu. Kwa hiyo, unapokuja na tozo; kwa mfano, sasa hivi tuna asilimia mbili ya kodi ya zuio. Wachimbaji wadogo waliwahi kukaa na Mheshimiwa Marehemu Dkt. Magufuli, tukazungumzia habari ya kutoa tozo hizo, na hii ndiyo unaona sasa hizi makusanyao ya dhahabu ni makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri mkafahamu tunapozungumzia mchimbaji mdogo, tuelewe mchimbaji mdogo ni yupi? Tafsiri ya mchimbaji mdogo ni ipi? Kuna mchimbaji mdogo jamani, hata machinga ana nafuu. Sasa mtu huyu, kama ndio huyu kweli mnamlenga kwa maana ya kodi hiyo, maana yake katika maeneo hayo ya machimbo kuna mtu unakuta amekaa miezi sita hajapata hata gramu hata moja. Ni vizuri pia mkayasoma mazingira hayo. Kwa hiyo, katika mazingira hayo, kuna mtu huyu kama hujamtengenezea incentives, atatorosha madini yako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba watu wa Wizara, Serikali imefanya kazi nzuri ya kutengeneza masoko, wachimbaji wanatoka katika maeneo yao, wanapeleka dhahabu sokoni. Bananeni na hawa wanunuzi wa pale; kama kuna utoroshaji hapo, mbanane hapo, lakini nje ya hapo nakuhakikishia… (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kapufi!
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Naam Mheshimiwa Naibu Spika.
NAIBU SPIKA: Kaa chini kwanza.
Kanuni yetu ya 68 kutozungumza jambo ambalo lina maslahi binafsi ya kifedha. Wakati wa majadiliano Bungeni au kwenye Kamati yoyote ya Bunge, Mbunge hataruhusiwa kuzungumzia jambo lolote ambalo yeye mwenyewe ana maslahi nalo binafsi ya kifedha. Ina utaratibu mwingi sana. Kwa nini nakwambia hivyo? Kifungu kidogo cha (2) kinasema, “kwa madhumuni ya Kanuni hii, Mbunge au mwananchi yeyote anaweza kumwarifu Spika kwa maandishi akitoa na ushahidi kuwa Mbunge amezungumzia jambo ambalo ana maslahi nalo binafsi. Unatakaiwa u-declare interest.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, na-declare interest, pia mimi ni mchimbaji mdogo wa madini. Kwa msingi huo, hili ninaloliongea ni kwa uzoefu mpana na lengo langu ni jema la kuisaidia nchi hii ili eneo la uchimbaji liwe na msaada kwa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kusisitiza, nawaomba sana kwa sababu lengo ni kufanya nchi iendelee kupata kipato kikubwa. Kwa hiyo, kwa sura hiyo nawaombeni sana wenzetu wa Wizara, katika eneo hilo nina uhakika tuna uwezo wa kuitoa nchi. Nafahamu tulikuwa na asilimia 6.7 mwaka 2020, lakini tukaenda asilimia 7.2 mwaka 2021. Kwa hiyo, tuna uwezo wa kwenda mbali zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa utoaji mikopo kwa wachimbaji, ni jambo jema, ni jambo la afya. Siyo kwa maana ya mwisho, lakini GST, kwa maana hawa watu ni wenzetu wa utafiti. Nchi hii ni kubwa, ina maeneo mengi, lakini hawa wenzetu wa GST tusipowazesha; leo karibia nchi kila sehemu utasikia leo kuna mfumuko wa madini, sasa wenzetu wa GST mko wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Bashe alipokuwa anazungumzia habari ya kuimarisha kilimo, lakini eneo la uchimbaji lina uwezo pia wa kuajiri Watanzania wengi especially vijana, lakini wenzetu watusaidie kitu kimoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema katika kilimo tutakuwa na extension officers waende kwa mkulima mmoja mmoja, vipi wenzetu wa madini? Mnasemaje Ma-geologist kwenda kwa wachimbaji huko kumsaidia mchimbaji? Kwa sababu hapa unaweza ukasema eneo hili labda akiba (reserve) ni kilo 20 za dhahabu. Maana yake kumbe tukifanya kitaalamu, tuna uwezo wa kuzipata kilo 20 za dhahabu, lakini watu wanachimba kwa design ile ile ya zamani ya kuganga njaa. Watusaidie kwenda mbali zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo, nimalizie na suala la kilimo.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Nakushukuru, naunga mkono hoja.