Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali 2022/2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Awamu ya Sita, Mama shupavu, Mama mchapakazi kwa kutuletea bajeti ya kizalendo na ambayo ina harufu ya mapinduzi. Bajeti hii imekuwa ya tofauti kwa sababu ya mambo mawili makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ni bajeti inayoelekeza kubana matumizi; na jambo la pili ni bajeti ambayo inakwenda kuimulika Sheria ya Manunuzi na kuiwekea control. Mambo hayo mawili ni mambo makubwa ya msingi sana, naipongeza sana Serikali kwa jambo hili kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2021 bajeti yetu ilikuwa shilingi trilioni 37.99 na makusanyo ya ndani tulilenga tukusanye shilingi trilioni 21, lakini tukaishia kukusanya shilingi trilioni 17 mpaka Aprili. Mwaka huu bajeti yetu ni shilingi trilioni 41.48 na makusanyo ya ndani tunalenga tukusanye shilingi trilioni 28.02. Kwa maana hiyo, katika haya makusanyo ya shilingi trilioni 28.2, TRA inatakiwa ikusanye shilingi trilioni 23.65. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pale TRA zipo department nne za kikodi. Ipo Department ya Custom and Excise, Department ya Domestic Revenue, Department ya Large Tax Payers na Department ya Kikodi ya Tax Investigation. Mimi nitaongelea department moja ya Custom and Excise, Department yetu ya Forodha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye makusanyo ya TRA mwaka 2021 ya shilingi trilioni 17.2 department hii ilikusanya asilimia 40. Vivyo hivyo hata makadirio ya mwaka huu wa fedha shilingi trilioni 23.68 makusanyo ya ndani, tunatarajia Department hii ikusanye asilimia 40, karibia shilingi trilioni 10. Sasa department hii inakusanya wapi? Maeneo yake makubwa ni wapi? Maeneo yake makubwa ya kwanza ni bandari zetu, kwenye airports zetu na kwenye mipaka yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaangazia eneo moja katika hayo niliyoyataja nalo ni la bandari. Natambua kwamba tunazo bandari nyingi, lakini nitazungumzia bandari zetu tatu kubwa; Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Tanga na Bandari ya Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bandari ya Dar es Salaam peke yake kwa Tanzania ndiyo bandari pekee ambayo International Trade kwa ukubwa inafanyika kwa karibia asilimia 90. Asilimia 90 ya biashara yetu ya Kimataifa inafanyika Bandari ya Dar es Salaam. Sasa ni nini tunatakiwa tufanye kwenye maeneo haya ya hizi bandari tatu ili tukakusanye zaidi? Maana kupanga matumizi siyo shida, shida ni namna ya kukusanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, tunatakiwa tukanunue vifaa vya kisasa kwa ajili ya ku-deal na containers. Kwenye biashara ya bandari, fedha nyingi ipo upande wa containers. Vifaa ninavyoviongelea hapa, siongelei hizi cranes ambazo tunazo kwa sasa, hizi Gottwald Cranes, tunatakiwa tuwe na vifaa vya kisasa SSG. Hii inaitwa Ship-to-Shore Gantry Cranes.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya gati zetu zilivyo, kwa namna ambavyo Mheshimiwa Rais ameweka fedha pale Bandari ya Dar es Salaam, tumeiendeleza gati ya kwanza mpaka gati ya saba. Tumeweka pale mradi wa dola milioni 420 kwa ajili ya kuendeleza hizo gati. Sasa gati namba sita na namba saba ndizo gati ambazo zita-deal na containers. Tunatakiwa tukanunue hivi vifaa SSG (Ship-to-Show Gantry Cranes). Kifaa kimoja katika hivi, kinagharimu kama Euro milioni 11 hivi au milioni 10 na kitu. Kwa ukubwa wa gati zilivyo pale, gati moja itahitaji angalau kwa uchache, tena hizi SSG angalau tatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, upanuzi tuliyoufanya pale, bandari yetu kwa sasa ina uwezo wa kupokea meli kubwa sana zile za post-panamax, na zile meli zikija pale zina urefu mkubwa na zinabeba containers nyingi. Kwa hiyo, kutumia vifaa hivi vidogo vidogo tulivyonavyo pale, tunapoteza biashara. Meli zinakaa muda mrefu kwenye kushusha na zinakaa muda mrefu kwenye kusubiri kuingia. Kwa hiyo, tunapoteza biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiweka SSG tatu tatu kwenye kila gati, tafsiri yake ni kwamba hizi post-Panamax ships huwa zinakuwa na partition tatu. Kwa hiyo, kila crane itashambulia partition moja. Tutashusha mizigo yetu ndani ya muda mfupi, meli zitaondoka na tutavutia watu kuja kufanya biashara na sisi kwenye eneo letu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, tunatakiwa tufunge mifumo ya ku-control containers ambayo ni ya N-generation; mifumo ya kisasa ambayo inai-trace container kutoka the pot of loading mpaka hapa inapofika kwetu na mpaka inaporudi kwa wenye nayo. Biashara ya container duniani ndiyo biashara kubwa inayo-control biashara za meli. Kwa hiyo, tusipofanya hivi tutakuwa hatujawekeza vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni skilled labour. Watu wetu tuwaelimishe, tuwasomeshe wajifunze mambo haya. Sasa ukurasa wa 27 wa Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti inasema, “Kamati imebaini kwamba Mamlaka ya Bandari, badala ya kuendeleza kuwekeza ili kuwe na ufanisi katika uondoshaji wa shehena bandarini inafikiria kutumia makampuni ya nje kama vile DP World na TICTS. Hatua hii inaweza kuleta mafanikio ya ufanisi lakini itapunguza kwa kiasi kikubwa mapato ya Serikali.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kushauri ni nini? Ninashauri kwa uwekezaji huu ambao tumeufanya bandarini, tusiende kufikiria kuwapa watu kuendesha bandari yetu. Tumeweka hizo Dola milioni 420 Bandari ya Dar es Salaam, tumeweka Shilingi bilioni 256 za Kitanzania Bandari ya Tanga, na tumeweka Shilingi bilioni 157 Bandari ya Mtwara. Sasa uwekezaji huo mkubwa; vifaa hivi kuvinunua hata Shilingi bilioni 500 haifiki. Sasa Shilingi bilioni 500 ndiyo itufanye tuigawe Bandari yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tusifanye hivyo. Twendeni tukafanye utafiti kama ili tuone kama kuna genuine reasons ya kumpa mtu kuendesha bandari yetu. Tunao uzoefu, tuliwapa TICTS, leo ni mwaka wa 22 tunao pale, wakipata Shilingi bilioni 230, sisi tunachoambulia ni Shilingi bilioni thelathi na kitu tu. Ukiweka na hela ya pango ni kama Shilingi bilioni tisini na kitu tu, it is a loss.

Mheshimiwa Naibu Spika, wote tumeshakubaliana kama Watanzania, Bandari ya Bagamoyo tutawapa watu. Hakuna mwenye ubishi juu ya hilo. Sasa na hii ya Dar es Salaam nayo tuwape watu? Hata ukiwa na nyumba yako ya kupangisha, unapangisha vyumba vyote mpaka unakosa pakukaa? Haiwezekani! (Makofi)

Mhehimiwa Naibu Spika, nami naishauri Serikali, na huu ushauri ni kwa nia njema, twendeni tukawekeze vifaa ambavyo vinatakiwa ambavyo ni hizi cranes, tuwekeze hii mifumo ya kisasa ambayo ni N-generation na tuwaeleimishe watu wetu halafu tuendeshe bandari yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa uwekezaji huu mdogo hata bila hivyo vifaa, mwaka huu wa fedha, 2022/2023 mpaka kufikia mwezi wa Aprili, Bandari ilikuwa imekusanya Shilingi bilioni 888, ukilinganisha na mwaka 2021 kabla ya uwekezaji ambapo muda kama huu tulikuwa tumekusanya Shilingi bilioni 751. Hapa tuna-handle container 600,000 tu, tukiweka hivi vifaa ninavyovisema, tutaenda kwenye full swing ya ku-handle container 1,500,000. Tukifanya hivyo, hii department ya TRA ambayo naisemea hapa ya Customs itakusanya zaidi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, sijajua ni kengele ya kwanza au ya pili.

MJUMBE FULANI: Ya pili.

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana kwa fursa. (Makofi)