Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nikiangalia katika mapendekezo haya ya mpango kwa mwaka 2024/2025, tunaona Serikali inatarajia kutenga trilioni 15.3 na hii ikiwa ni ongezeko la trilioni 1.2 kutoka kwa hesabu za mwaka wa fedha 2023/2024 ambao tuko nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ni fedha nyingi sana na endapo zitatumika ipasavyo na Bunge hiki likaridhia kutenga kiasi hiki cha fedha, narudia kupiga mstari, zikatumika ipasavyo yawezekana kabisa tukaenda kuleta mafanikio makubwa katika uchumi wetu na kuwasaidia Watanzania pamoja na Tanzania yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hili nimpongeze Mheshimiwa Rais Samia kwa maono yake. Ukisoma mpango unaweza ukaona ni kwa jinsi gani maono ya Serikali na maono ya Mheshimiwa Rais yalivyoweza kuchukuliwa. Vilevile, nampongeza Mheshimiwa Mwigulu Nchemba pamoja na Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, naona wametengeneza timu nzuri sana sawasawa na mithili ya ile timu ya tano, moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa mapendekezo haya na hasa ukisoma katika ukurasa wa 40 wa Taarifa ya Kamati ya Bajeti, sekta binafsi inakwenda kuchangia shilingi trilioni 12.29. Vilevile, Kamati imebaini kuwa, hakuna mfumo rasmi ambao umewekwa na Serikali katika kubaini mchango wa sekta binafsi. Hii ni hatari kwa sababu sekta binafsi tumekubaliana iwe ndiyo engine ya kuchochea uchumi wa Taifa letu. Hivyo, ni dhamira ya Serikali na ningependa iwepo hiyo kwamba, ijitokeze kwa wingi sana kuweza kui-support sekta binafsi ili hakika iweze kufanya vile inavyofanya. Iwe ni engine ya kuusaidia uchumi wa Tanzania uweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata hiyo dhamira ya Serikali yenyewe iliyopo, ukiangalia na hili nalizungumza kwa mara nyingine tena kwamba sekta binafsi ipo kwa minajili ya kufanya biashara, lakini pamoja na kufanya biashara, yenyewe ndiyo inayotuletea viwanda na iende hadi kufikia suala la private public partnership. Tunaona hapo kuna kusuasua na laiti kama Serikali ingeweza ikajipeleka kwenda kutafuta suluhisho la kuisaidia sekta binafsi kama ilivyo katika nchi jirani ambazo nitazitaja, hakika Tanzania tunaweza tukapiga hatua kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukiangalia katika upande mzima wa ufanyaji wa biashara ambao ndiyo unaochagiza suala la uchumi, ningependa kuangalia nchi jirani ya Rwanda. Nchi ya Rwanda, iko namba 38 katika ile orodha ya easy of doing business. Nchi ya Kenya, majirani zetu ni nchi ya 56. Tanzania tuko wapi? Tanzania ni nchi ya 141, tuko mbali mno. Hii ni hatari, kwa sababu ukiangalia Mpango huu, mchango mkubwa kama tulivyoona unatokana na Serikali. Serikali ndiyo inakwenda kuchangia shilingi trilioni 15 katika masuala yanayohusiana na maendeleo ambayo nimeyataja kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta binafsi ni shilingi trilioni 12. Nchi hizi ambazo zimefanikiwa ni the other way round. Utakuta Rwanda sekta binafsi ndiyo inayoongoza katika kuchangia, Kenya sekta binafsi ndiyo inayoongoza kuchangia katika uchumi. Natamani niione Serikali yangu inajikita zaidi katika kuisaidia sekta binafsi ili iweze ikapiga hatua kuisaidia nchi hii kutimiza malengo yake ya kuwaletea Tanzania maendeleo ya haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kwamba, nchi yetu hii ni nchi ya ujamaa na kujitegemea na hata kwenye Katiba, ukiisoma Katiba Ibara ya 9 inasema hivyo. Waheshimiwa, pamoja na kwamba sisi ni wajamaa thinking yetu itoke kule. Kwa sababu tulikubaliana na Benki ya Dunia kwenye ile Structural Adjustment Program kuwa private sector iwe ndiyo sekta inayokuwa kama vile tunaita andamizi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa. Tuonyeshe hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe rai kwamba, tunapoangalia mipango yetu, zile fikra za miradi kuwa miradi yote mikubwa imilikiwe na Serikali tuondoke huko, kwa sababu tunaweka fedha nyingi sana katika utengenezaji wa miradi mikubwa. SGR, kufua umeme, wakati fedha zile yawezekana zingeingia katika kusaidia maendeleo ya wananchi moja kwa moja kwenye service delivery.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta sehemu kubwa ya fedha zile zinakwenda katika miradi mikubwa ambayo ingeweza ikasaidia kabisa kuwafanya sekta binafsi ndiyo wakawa wachangiaji. Tuingie katika mambo ya public private partnership, inaweza ikatusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kuboresha private sector na tunaiboreshaje. Hili narudia tu, ni somo ambalo tunalizungumza wakati wote. Jambo la kwanza katika Mpango huu, wafikirie kuangalia ni kwa jinsi gani wanakwenda kupunguza utitiri wa regulatory authorities. Wakazipunguze hizi ili angalau kuwepo na unafuu katika ufanyaji wa biashara na sekta binafsi iweze kufanikiwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Serikali haijafanikiwa kuondoa vizuizi katika soko la mitaji. Hebu waliangalie hili, full liberalization of capital market. Wakifanya hivi maana yake ni kwamba sekta binafsi inaweza ikapata nguvu ya kujisogeza mbele zaidi kuliko hivi sasa. Naishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kutoshindana sana katika soko la fedha la hapa ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, Hati Fungani za Serikali kwa mwaka mmoja riba ni asilimia 9.2 na ukienda kwenye mabenki yetu hasa CRDB na NMB riba ni 9.5. Maana yake ni nini? Ni kwamba katika hali ya kawaida wawekezaji wengi wa kifedha kama hivi watazipeleka fedha Serikalini na watawatia njaa kidogo. Naomba nitumie neno ambalo siyo zuri sana, lakini ku-suffocate private sector. Hili ni jambo ambalo inabidi tuliangalie sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la pili kubwa ambalo ningependa kulizungumza ni kuhusu mapato ya Serikali. Hapa najipeleka moja kwa moja katika mashauri ambayo yamekwama katika hizi Mahakama ya TRAB na TRAT. Hili neno lilileta maneno kidogo. Ni zile Bodi ya Rufani ya Kodi na Mahakama ya Rufani ya Kodi. Kwa haraka kesi ambazo ziko na hii ni kwa mujibu wa CAG; kesi ambazo ziko kule kwenye TRAT ni kuanzia mwaka 2018 hadi 2022 kuna jumla ya kesi 36, thamani yake zinazoshindaniwa ni shilingi bilioni 90. Ukienda kwenye TRAB utakuta kuna kesi zipatazo 287 na thamani yake ni shilingi trilioni 2.2. Maana yake ni kwamba, hizi Fedha za Serikali zingekuwepo na utaratibu mzuri wa TRA kuelewana na wafanyabiashara katika ufanyaji wa mahesabu, fedha hizi zingeingia katika Bajeti ya Serikali. Tunavyozichelewesha kuziweka kule maana yake tuna wa-suffocate tena wafanyabiashara, lakini tunatengeneza uncertainties; kutokuwa na uhakika katika kufanikisha private sector.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka, nashauri Serikali itengeneze mifumo ambayo itawafanya wafanyabiashara watambue kwa uhakika kodi zao ambazo zinatakiwa zitolewe mapema kabisa. Kwa sababu kuwavizia wafanyabiashara katika zile audits ambazo zinafanyika mnawapa mzigo wafanyabiashara. Hiki siyo kitu chema kabisa katika… (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Tarimba.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napongeza Serikali na niwatakie kila la kheri. Mwenyezi Mungu ajalie hiki kitu kiweze kupita. (Makofi)