Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuchangia kwenye Mpango wa Maendeleo wa Nne na Mwongozo wa Maandalizi wa Mpango wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Nitaanza kwa kuangalia uhalisia wa Mpango ambao tunaletewa versus utekelezaji kwa maana ya bajeti zinavyotengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mathalan, kwa mpango wa mwaka 2022/2023 kwa maana ya bajeti tulikuwa na bajeti ya shilingi trilioni 41 na fedha za maendeleo ambazo zilipelekwa kwenye utekelezaji wa mpango ilikuwa shilingi trilioni 15, sawa na 36%, walau hapa tulitenga vizuri. Ukija mwaka 2023/2024 ilikuwa na bajeti shilingi trilioni 43.3 lakini tukatenga shilingi trilioni 14 sawa sawa na 32.4 tu. Mwaka 2024/2025 tuna-project kutenga bajeti yetu kuwa shilingi trilioni 47.4 lakini bado tunatenga shilingi trilioni 15 tu. Kwa hiyo, utaona kuna ongezeko kati ya bajeti hii, yaani takribani shilingi trilioni nne na kitu, lakini kwenye fedha za maendeleo tumeongeza shilingi trilioni 1.2 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miradi mingi ambayo Mpango unatakiwa u-reflect kwenye sekta ya afya, kilimo, nishati na hata elimu. Mathalan, sasa hivi Bunge lako Tukufu limepitsha hapa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, tukasema ili iweze kutoa huduma bora na kufanya kazi vizuri, tutahitaji tuwe na miundombinu kwa maana ya vituo vya afya zahanati, watumishi toshelezi, vifaa tiba, dawa na vitendanishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mpango wa mwaka 2022/2023 mathalan, Serikali ilipanga kujenga zahanati 495, lakini mpaka tunamaliza mwaka ilikuwa wamejenga zahanati 228 tu sawa na 46%. Sasa utajiuliza, kama usipotenga fedha toshelezi, hii Bima ya Afya kwa Wote itaenda kutendeka vipi kwa uhalisia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa taarifa ya Serikali, mpaka Machi, 2023 mahitaji ya Wahudumu wa Afya ni 219,000, waliopo 106,000 pungufu 112,000. Ni lazima Serikali ijiwekeze kuhakikisha kwamba inatenga fedha ili sasa zile sekta zote muhimu ambazo zinaweza kuchagiza kwenye uchumi zinapelekewa fedha ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine, sote tunajua kwamba kwenye sekta ya nishati mathalan, tuna tatizo kubwa sana la umeme kukatika na pia nishati ya mafuta inapanda bei kila kukicha. Tuna gesi ya asili hapa Tanzania ambapo pia mzunguko utakuwa unafanyika Tanzania tu bila ku-import fedha na kupelekea upungufu wa dola nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika gesi asilia, nimejaribu kupitia hapa kwenye Mpango, tunajua, gesi asilia inatumika majumbani, kwenye viwanda, kwenye magari, na pia kufua umeme, na tunayo hapa Tanzania. Kwa hiyo, nilitarajia Mpango ujielekeze zaidi kutenga fedha toshelezi ili sasa tuweze kuchakata hii gesi kuhakikisha kwamba Watanzania wengi wanaunganishiwa magari yao na kutumia gesi ya asili ambayo itakuwa ni affordable.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi mafuta; petroli ni shilingi elfu tatu na kitu, lakini gesi ya asili tumeelezewa pale. Ukijaza gesi ya asili kwa shilingi 20,000 au shilingi 30,000 unafika mpaka Morogoro, zaidi ya kilometa 200. Kwa hiyo, itapunguza gharama za maisha kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia majumbani. Mpango unaonesha kwamba wameunganisha nyumba 209 tu kwa Dar es Salaam, nyingine zimekamilika 980 na hata hii ya vituo vya mafuta ya gesi ime-concentrate tu huko Mkoa wa Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara; Tanzania hii, mikoa mingine huwa mnaiacha ya nini? Kwa hiyo, lazima mweke fedha nyingi. Tuwe na vituo vya kutoa gesi katika kila wilaya, katika kila mkoa ili mimi nikiweka gari langu niki-convert liweze kuweka Dar es Salaam likinifikisha Morogoro, likinifikisha Dodoma kote na-fill. Kuacha hizo faida za kiuchumi lakini pia faida za kimazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipange tu ilimradi tunapanga tu, tumesoma hapa imependeza, lakini kiuhalisia unakuta haina mafanikio chanya kwenye uchumi wa Taifa letu. Katika kuhakikisha kwamba tunakuwa na umeme toshelezi, lazima tuwekeze fedha nyingi, lakini mpango hau-reflect hayo yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwenye NIDA. Sote tunatambua umuhimu wa Vitambulisho vya Taifa na sasa hivi kila idara ukienda, kila sehemu ukigusa unaombwa Kitambulisho cha Taifa. Mamlaka ya Kitambulisho cha Taifa ilianzishwa tarehe 1/8/2008, mpaka sasa hivi ni miaka 15. Kwa takwimu ya sensa, Watanzania wapo zaidi ya milioni 61 walio na stahiki ya kupata vitambulisho nimeangalia hapa, ni zaidi ya milioni 35. Kwa mujibu wa Kamati yako ambao wameainisha hapa, inaonesha vitambulisho vya Taifa kwa maana kadi zilizochapishwa ni milioni 12 tu kwa Watanzania ambao wamepewa, waliosajiliwa ni milioni 24.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni just 50%. Ndani ya miaka 15 tumefanikiwa kutengeneza kadi milioni 15 tu, bado milioni 23 kwa mujibu wa sensa. Kama ndani ya miaka 15 tunatengeneza kadi milioni 12 hizi milioni 23, Kitambulisho cha Taifa tunasema ni muhimu sana na tunatarajia kutengeneza zaidi ndani ya miaka 30 au 35 ijayo. Hii ni kitu ambacho hakiwezekani.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na zaidi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Esther Matiko kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Engineer Hamad Yussuf Masauni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

TAARIFA

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mchangiaji kuwa tumeshalipia fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya mwaka 2022, shilingi bilioni 42.5, zinazalishwa kadi milioni 11 ambazo zikija zitakuwa zimemaliza tatizo la mahitaji ya kuwapa kadi wote ambao wana namba za vitambulisho. Idadi yao siyo kama alivyotoa takwimu; ni 25,000 na siyo 35,000 kama alivyosema. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Esther Matiko, taarifa hiyo unaipokea?

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei. Angenisikiliza vizuri. Nimesema mpaka sasa hivi ni milioni 24 something, uki-round off inakuwa ni milioni 25 ambazo mmesajili. Sasa kuna Watanzania ambao hamjawasajili mpaka sasa hivi. Nimechukua takwimu ya sensa, watu ambao wako eligible kupata vitambulisho ni 35 million plus. Kwa hiyo, una about 11 million hujawasajili. Hizi ni takwimu zenu wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi hawa watu walikuwa na deni, wakalipiwa deni shilingi bilioni 17, kodi wameondolewa kwenye zile kadi, vi-tip sasa hivi siyo adimu sana…

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Esther Matiko, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, atulie, atulie Mheshimiwa Waziri.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikosea siyo elfu, ni milioni. Ninachosema ni kwamba, takwimu yake ya shilingi milioni 35, haipo sahihi.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Esther Matiko unaipokea taarifa hiyo?

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ananipotezea muda kusema, anabishana na sensa. Mheshimiwa Waziri, kaa chini nipokee taarifa. Would you sit down please?

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kila Mtanzania anastahili kupata kadi ya NIDA, ni umri wa miaka 18 kwenda juu kwa mujibu wa sheria.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Esther Matiko taarifa unaipokea?

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa takwimu ya sensa watu wenye umri wa miaka 18 na kuendelea ni takribani 35 million, just google. Hapo ulipokaa chukua google and do the analysis and statistics utapata uhalisia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu ulindwe. Sasa wana gap ya watu milioni 11 hawajasajiliwa, ukijumlisha ni takribani milioni 23 hawana kadi. Mmepewa msamaha wa kodi, mmelipiwa deni shilingi 17 billion, unasema hapa mnakaribia kuchapisha. Kamati imeenda imedhihirisha kwamba mtambo huo unaweza ukazalisha kwa saa kadi 4,500 lakini kwa mwaka mzima imezalisha kadi 1,800,000 tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati kadi 4,500 kwa saa mlikuwa mnatakiwa kwa mwaka walau m-produce kadi milioni (nimefanya hesabu zangu hapa), ni almost 11 point something million kama mtu anafanya kazi kwa saa tisa ndani ya siku tano kwa miezi 12.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima kama Taifa tuhakikishe Watanzania wote wanapata kadi tena ambazo zipo centralized. Mfuko wa Bima ya Afya unakuwa mle, leseni zinakuwa mle, huduma…

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Esther naomba ukae. Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani taarifa.

TAARIFA

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Mheshimiwa mchangiaji anashindwa kuelewa. Nimeeleza kwamba tumeshalipia shilingi bilioni 42.5 kwa ajili ya kuweza kuzalisha vitambulisho milioni 11 ambayo ni pungufu. Hivi tunavyozungumza, kadi hizo zimeshaingia zaidi ya milioni 17. Yaani watu milioni 17 ukijumlisha na zile 11,000 ambazo zipo njiani, kwa hiyo, tunatarajia mwisho wa mwezi Desemba tatizo la NIDA la kadi litakuwa limepatiwa ufumbuzi kwa watu milioni 24 ambao wanastahili kupata kadi, waliokuwa na namba za utambulisho.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Esther Matiko, taarifa unaipokea?

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo Waziri apunguze kujitetea. You are talking about the future, mimi naongea current ambacho kimeripotiwa hapa. Sasa hayo mengine utakuja kuyasema huko baadaye. Naongea sasa hivi, hayo maneno mengine unakuta mnaongea ni unreality, ukija tena unaambiwa aah, zilikuja, zikakwama, hazikuprintiwa, zikapotea, we don’t need that. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na unilindie muda wangu. Mwisho kabisa ni kwenye huu mpango, lazima u-reflect na maendeleo ya watu. Tumezungumza hapa hasa sisi ambao tunapakana na hizi hifadhi, tunapata kero nyingi sana kiuhalisia. Achilia mbali kutekwa, kuchukuliwa mifugo yetu, watu wetu kutekwa na kunyanyaswa na kupotezwa, ni kweli imekuwa ni taratibu wanaswaga ng’ombe some kilometers, ambapo hata hazipo hifadhini, wanaenda wanaziingiza. Mbaya zaidi, wakikamata ng’ombe milioni moja, watasema zilikuwa ng’ombe laki nane. Sijui hizi laki mbili zinaenda wapi? Wakikamata mbuzi 2,000 atakwambia zilikuwa mbuzi 500…

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza,…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Esther taarifa, japo kengele imegongwa.

TAARIFA

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napenda kumpa taarifa Mheshimiwa kwamba kule kwetu tunamwita Msubati Mara, hivi ninavyozungumza, Kata ya Kuzugwa ng’ombe 500; juzi ng’ombe 63, wanalipa faini, Serikali haitaki kuachia ng’ombe na yenyewe eti ina- lobby ooh, tutakata rufaa, wanashindana na wananchi kuwafilisi.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Esther, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa.

MWENYEKITI: Malizia, muda wako umeisha.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Taifa we need to say no to this. Lazima tujue. Kwanza inashangaza, eti ruling inatoka leo, then kesho yake unaambiwa ng’ombe zote mia nane na kitu zimeuzwa. Hao wanunuzi walikuwa wako standby waje kununua?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Esther ahsante sana, muda wako umeisha. Nashukuru sana.