Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Regina Ndege Qwaray

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia mpango wa Serikali. Kwa kuanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anaendelea kuipambania nchi yetu kwa kutuletea maendeleo katika kila sekta. Lakini nimpongeze sana kwa kurejesha Tume ya Mipnago, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuanzisha Wizara hii ya Mipango. Kupitia Wizara hii ya Mipango, tunaamini kabisa kwamba sasa maendeleo na mipango itaenda kupangika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta inayobeba watanzania wengi ni kilimo, uvuvi na ufugaji, na mimi nimeweza kupitia katika ripoti ya kamati na niungane na kamati kwamba bado kasi ya sekta ya umwagiliaji iko chini mno. Serikali inahitaji kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta hii ya umwagiliaji, kwa sababu nchi yetu mpaka sasa suala la mvua sio suala lenye mashaka. Kwa hiyo, Serikali ikiwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji tuna uhakika wa kupata chakula cha kutosha lakini pia sekta ya mifugo itakwenda kustawi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio kila jambo lazima Serikali ifanye, Serikali inaweza kutengeneza mazingira wezeshi katika private sector, wakawekeza katika private sector kwenye sekta hii ya umwagiliaji. Uwezeshaji wake huo ni kupunguza kodi katika mitambo ya uchimbaji wa visima na mabwawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza kupata mabwawa ya kutosha, tuna uhakika wafugaji watafuga vizuri. Tuna uhakika tunaweza kufuga Samaki, tuna uhakika tutapata maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu. Lakini hivyo hivyo tukiweza kuwekeza kwenye visima tutakuwa tumetatua tatizo la kilimo na uzalishaji. Kwa hiyo, ushauri wangu mkubwa ni kwamba bado Serikali iwekeze kwa nguvu kubwa katika kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali na kuishukuru sana kwa kuendelea kutupatia mbolea ya ruzuku, kwa sababu wananchi wanapata mbolea, lakini bado ninatamani kuona kwenye mpango, Serikali iende kwenye kuwekeza katika viwanda vinavyochakata gesi asilia. Tukiwekeza kwenye viwanda vya kuchakata gesi asilia tunapata nishati mbadala lakini tunapata mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi nchi yetu tunaagiza mbolea aina ya urea nje ya nchi kwa asilimia mia moja, jambo ambalo linafanya gharama kubwa Serikali kuagiza hiyo mbolea ya urea, lakini tukizalisha hapa nchini ni uhakika kwamba mbolea hiyo itapatikana kwa urahisi na wananchi watakuwa wamepata hiyo mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunatakiwa kuwekeza kwenye matumizi ya mbolea ya asili kama mbolea ya samadi na mboji kwa kuwaelimisha wananchi wakulima na wafugaji kwamba baada ya mavuno zile takataka za mashambani, wapewe elimu namna ya kuhifadhi na baadae kuzitumia kama mbolea katika kilimo. Pia, mbolea ya samadi tunaweza kupata kupitia mifugo, mifugo nchi hii bado ni mingi sana lakini wananchi bado hawajapata elimu ya kutosha namna gani tunaweza kutumia mbolea ya samadi katika kilimo chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia inaweza kuwekeza katika majiji makubwa kama Jiji la Dar es Salaam, Jiji la Dodoma, Jiji la Mwanza, kwa sababu haya majiji makubwa kuna ukusanyaji mwingi wa taka ngumu, lakini Serikali ikiamua kuwekeza kwa kupitia viwanda, tukawekeza kwenye kuchakata taka ngumu kupata nishati mbadala, hapo hapo tuna uwezo wa kupata mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, badala ya taka ngumu kutupwa na kuziba mitalo na nini. Serikali ianzishe viwanda ambavyo vitaweza kuchakata hizo taka ngumu ili kujipatia nishati mbadala, lakini pia tuna uwezo wa kuzalisha mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wetu hasa wakulima wadogo wadogo wamekuwa wakilima kilimo kisicho na tija na hii inasababishwa na nini? Hii inasababishwa na kwamba wakulima wanalima bila kujua ardhi yao inahitaji kustawishwa mazao ya aina gani. Wakulima wanalima bila kujua kwamba udongo ule unafaa kustawisha mbegu za aina gani na hii kazi ilitakiwa ifanyike, kwamba maabara zetu zifanye kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, maabara zimewekwa katika ofisi za kanda, maabara ziko mbali na wananchi. Mfano, sisi Mkoa wa Manyara, maabara tunayoitegemea ni maabara iliyoko Arusha Serian Tengeru au uende Tanga. Jambo ambalo unampa mkulima gharama kubwa kwenda kufanya vipimo vya udongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, amewawezesha Maafisa Ugani pikipiki pamoja na vifaa vya kupimia udongo lakini jambo la kusikitisha sana, Maafisa Ugani mpaka sasa ukienda kuuliza huko kwa wakulima kazi hiyo haifanyiki. Kwa hiyo, wakulima wamekuwa wakilima bila kujua kwamba udongo wake unatakiwa kustawisha zao gani lakini mbolea ya aina gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri ifike wakati Maafisa Ugani warudishwe chini ya Wizara ya Kilimo ili waweze kusimamiwa ipasavyo, kwa sababu sasa hivi wanawajibika kwa Mkurugenzi, jambo ambalo linakuwa gumu sana kuwafuatilia mpaka ngazi za chini. Hivyo, wakulima wadogo wanatakiwa wapewe elimu kwa sababu wakulima wakubwa wana uwezo wa kupeleka hizo sample za udongo katika maabara na kuweza kufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishauri vile vituo vyetu vya utafiti viboreshwe, hata vile vifaa vinavyotumika bado havikidhi haja. Wakati mwingine hawapati majibu yanayoendana na uhalisia. Hata mtu akisema apeleke udongo, ukiwa na hekari kumi, ukichukua udongo wa sehemu moja yawezekana ndani ya hekari kumi labda una udongo wa aina tatu, kuna udongo wa kichanga, labda una mfinyanzi, ukipeleka udongo wa aina moja maana yake hutapata matokeo mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kilimo cha mbogamboga. Kilimo hiki cha mbogamboga ni kilimo ambacho watu wanalima bila kuwa na usimamizi hawana bodi ni watu wanaamua kujilimia tu lakini ndio kilimo ambacho kinazalisha kwa wingi zaidi, kwa hiyo niombe Serikali iwawezeshe wakulima wadogo wadogo kupata mbegu kwa urahisi.

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kumetokea…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Ndege kwa mchango mzuri.

MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)