Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Mpango huu wa mwaka 2023/2024.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuleta maendeleo kwa kasi kubwa sana katika Nchi yetu ya Tanzania. vile vile, jambo la pili niwapongeze Mawaziri wawili hawa, Waziri wa Fedha na Waziri wa Mipango. Nilipokuwa nawatazama hapa kwa haraka nilimtambua Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, lakini yule Waziri mwingine wa Fedha sikumtambua kwa sababu ya mabadiliko makubwa sana aliyonayo pale usoni kwake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nichukue nafasi hii kuishauri Serikali kwamba, tumekuwa tukitumia kitu kinaitwa force account kwa ajili ya kupeleka fedha za miradi kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo Miradi ya Afya, Elimu, Maji na mambo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka nishauri kama Mjumbe wa Kamati ya PAC kwamba, tumekuwa tukitembelea miradi hiyo ufanisi wake kwa kweli ni mdogo. Sasa, ni kwamba hii force account mimi nilikuwa nafikiria kwamba ingetazamwa upya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamekuwa wakitumika mafundi wa kawaida ambao kimsingi ukija kuangalia majengo unakuta yana crack. Pia, huwezi kwenda kukamata fundi wa kawaida labda ni mtoto wa mjomba au wa shangazi ndiye alipewa ile kazi, badala yake inakuwa ni hasara na mzigo mkubwa sana kwa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii force account tuiangalie upya na ikiwezekana basi tupate watu wenye qualifications kabisa wawe na vyeti sahihi kabisa…
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo taarifa, hapana. Umeshachangia bwana unanipotezea muda…
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Kiti unaniongoza. Naomba kumpa mchangiaji taarifa kuhusiana na hiyo hoja yake nzuri. Issue ya force account ningependa Bunge hili na Watanzania wafahamu kwamba, hatuikatai force account. Shida kubwa ya force account ni double handling. Hii double handling ya kwamba wakati huo huo rasilimali za ndani zinatumika….
MWENYEKITI: Ameshakuelewa. Ahsante.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: …na rasilimali za nje zinatumika, ndipo upotevu wa fedha unapotokea.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Msongozi.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ulenge ungechangia kwenye mchango wako. Ulikuwa na dakika 15 au ulikuwa unataka uje utietie maneno hapa …
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Nimekuongezea nyama, siyo kukuponda.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki bwana, tafadhali sana. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea. Ziwa Nyasa na maziwa mengine katika nchi yetu hii ya Tanzania. Naona iko haja ya kufanya uboreshaji kwenye maziwa yetu haya. Kwa mfano kwenye Ziwa Nyasa ukiangalia Bandari ya ile ya pale Mbamba Bay, bado haijakamilika. Kwa hiyo, tunaomba pesa zipelekwe pale ili kuweza kuiboresha ile Bandari ya Ziwa Nyasa pale Mbamba Bay ili ile bandari iwe na sifa ambayo itakuwa kweli na uwezo mkubwa wa kuweza kusafirisha mizigo mbalimbali katika bandari ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti jambo lingine niombe sana Serikali, tunapozungumzia kupeleka pesa za miradi ya maendeleo, basi ziharakishwe. Tumezungumza hapa katika bajeti iliyopita kwamba, pesa zitagawiwa kupelekwa kwenye maziwa mengine ambazo zilitengwa na Mheshimiwa Rais, ambapo Mheshimiwa Rais alitoa pesa hizo kupitia Wizara ya Mifugo. Karibu bilioni 20 zimekwishapelekwa katika Wizara, lakini kwa nini zinacheleweshwa kupelekwa kwenye Maziwa hayo ikiwemo Ziwa Nyasa ambalo pia tumepata kuambiwa kwamba tutatengewa bilioni tatu. Pia, mpaka sasa hivi tunavyozungumza tumefikia nusu ya mwaka, lakini bado pesa hazijaenda. Kwa hiyo, tunaomba sana tunapokuwa tunazungumza, pesa ziende mara moja zikafanye kazi, ilihali Mheshimiwa Rais amekwishatoa hizo pesa, basi ziharakishe utekelezaji huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka niishauri Serikali yangu kuhusiana na Mradi wa Reli. Reli ya Mwendokasi ya kutoka Mtwara mpaka Mbamba Bay. Hii reli ni muhimu sana kwa ajili ya kuchochea uchumi wa Tanzania katika ukanda wa kusini kwa sababu reli hii itasaidia kusafirisha mizigo mbalimbali ambayo itatokana na:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa tutakuwa na Mradi wa Liganga na Mchuchuma pale. Kwa hiyo, reli hii itasaidia kusafirisha chuma kutoka pale Liganga kupeleka Mtwara na kusafirisha kwenda maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tunayo makaa ya mawe katika Mkoa wetu wa Ruvuma. Hiyo nayo pia ingesaidia sana kurahisisha usafirishaji wa makaa ya mawe yale katika kuchochea hali ya uchumi katika nchi yetu. Vile vile, niseme kwamba, pamoja na kwamba tunatengeneza miundombinu ya barabara lakini kuongeza reli itasaidia sana kuzifanya zile barabara ziendelee kutumika kwa muda mrefu bila kuharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda katika upande ule wa kwetu Mikoa ya Kusini, Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma pamoja na Njombe barabara zimekuwa zikichimbika sana kwa sababu ya magari mengi, malori mengi ambayo yanatumika kwenye zile barabara kubeba makaa ya mawe, kubeba korosho, kubeba kahawa, kubeba mahindi, maharage na vitu vingine vingi kwa sababu ukanda ule wote sisi ndiyo tunaoilisha Nchi yetu hii ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana reli hii ikajengwa ili kuweza ku-balance hii miundombinu na kuweza kuifanya Serikali, pesa inayowekeza miundombinu, siyo unawekeza kwa muda mrefu kwenye miundombinu ya Barabara, halafu unaacha kwenye reli. Kwa hiyo, mpaka barabara inaharibika unarudi sasa na kuanza kutengeneza barabara wakati reli bado hujanza kuitengeneza. Kwa hiyo, nadhani kwamba uko umuhimu wa kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la Liganga na Mchuchuma. Limesemwa sana na Wabunge wengi hapa, naomba Serikali itueleze katika Mpango huu wamejipangaje kuhakikisha huu mradi unaanza mara moja ili huu wimbo tunaoimba hapa kila siku sasa upungue na twende kwenye utekelezaji, hii itatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi huu ukianza kutekelezwa utaongeza ajira katika nchi yetu ya Tanzania lakini pia utachochea uchumi kwa kasi sana. Hata hivyo, chuma kile klitakachochimbwa pale ndicho kitakachotumika katika kutengeneza magari, vipuri mbalimbali na mambo mengine kadha wa kadha. Niombe sana, ajira ni muhimu sana, lakini pia uchumi wetu kuimarika ni muhimu pia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda sasa kwenye suala la viwanda. Ili uchumi wetu uweze kuimarika ni lazima tuwe na viwanda hivi ambavyo vitachochewa na Sekta ya Kilimo. Kwa hiyo sasa, hebu mtuambie, Waheshimiwa Mawaziri watakapokuja ku-wind-up watueleze wamejipangaje kuhakikisha kwamba tunapata viwanda katika Nyanda za Juu Kusini na maeneo mengine katika nchi yetu ya Tanzania ili tuweze ku-balance kila eneo tuwe na viwanda, kwa sababu tukiwa na viwanda moja kwa moja tutachochea ajira kwa wananchi wetu lakini pia tutazalisha bidhaa ambazo tutaziuza ndani na tutaziuza nje ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, uzalishaji huu utakuza uchumi kwa kasi sana. Mheshimiwa Kitila Mkumbo, tunamtegemea sana, tunaona amekuja na kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya. Kwa hiyo, tunategemea tutapata matokeo chanya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kwenye masuala ya viwanda, kwa kuwa sisi tumekuwa tukizalisha sana mazao ya nafaka katika ukanda ule wa kusini, basi tunataka tuone Mheshimiwa Kitila anatupelekea viwanda vingapi katika kipindi hiki cha Mpango huu kufikia 2024. Mheshimiwa Waziri ana uwezo wa kutafuta wadau ambao watakuja kujenga viwanda vikubwa kule, tupate viwanda vya kukamua mafuta. Sisi kwenye uzalishaji hatuna shida. Shida ni namna ya kupata masoko, namna ya kuongeza thamani ya mazao yetu, hiyo ndiyo shida tuliyonayo lakini kwenye uzalishaji hatuna shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mvua za kutosha. Karibu nusu ya mwaka sisi mvua zinayesha tu. Hata sasa tunavyozungumza watu wako shambani. Kwa hiyo, nataka niseme nguvu za wananchi hawa zisipotee bure. Tuletee viwanda vya kuchakata mafuta, tukachakate sembe, tunayo soya ya kutosha, tukamue wenyewe mafuta ya soya. Vile vile, tunao ufuta wa kutosha. Nataka niseme tukifanya hivyo kwa kweli itakuwa imesaidia sana.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kiwanda cha Sonanko.
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sekunde moja tu. Kiwanda cha Sonanko, Kiwanda cha Tumbaku pale Songea Mjini. Kiwanda hiki kimekuwa kinaajiri wananchi wengi sana zaidi ya 3,000. Hata hivyo, sasa hivi ni zaidi ya miaka nane, tumeambiwa kiwanda kitafufuliwa mpaka leo hakijafufuliwa…
MWENYEKITI: Ahsante. Mengine andika.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.