Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Salim Alaudin Hasham

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SALIM A. HASHAM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata nafasi siku ya leo ya kuchangia kwenye Bunge lako Tukufu. Pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake kwa sababu wanafanya kazi nzuri sana. Nawapongeza kwa sababu kazi zinaonekana na sisi Wabunge wote humu ndani ni mashahidi wa kazi ambazo zinafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitajielekeza kwenye kuchangia kwenye Wizara ya Afya na nikiapata nafasi nitachangia kwenye Wizara nyingine. Tunaishukuru sana Serikali na tunamshukuru sana Mama Samia Suluhu Hassan kwa sababu kiukweli tumepata vituo vya afya vingi sana pamoja na zahanati za kutosha sana kwenye majimbo yote ambayo Wabunge wanayamiliki. Haipingiki kwamba kazi hizi nzuri zinafanywa na Serikali ya Awamu ya Sita lakini haina maana kwamba hakuna changamoto ambazo zinaendelea kwenye maeneo yetu hasa kwenye huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakupa mifano kadhaa kwa sababu changamoto hizi bado zipo. Kwenye mwaka wa fedha 2023 tulipata pesa shilingi milioni 200 kwenye jimbo langu. Nakupa mifano kwa sababu kuna changamoto nimeiona kati ya MSD na Serikali yetu. Nilipata shilingi milioni 200 ziligawanywa kwenye makundi mawili. Shilingi milioni 50 ilikuwa imeenda kwenye Zahanati yangu ya Minepa lakini shilingi milioni 150 imeenda kwenye kituo cha afya kipya kabisa kwenye Tarafa yangu ya Lupilo Kata ya Iragua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2018/2019 tulipata pesa shilingi milioni 300 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye Kituo cha Afya cha Lupilo. Mpaka hivi ambavyo ninaongea, shilingi milioni 50 kwenye Zahanati ya Minepa tumepata vifaa vya shilingi 3,800,000 toka mwezi wa Tano tumewalipa MSD, lakini pia kwenye vifaa tiba, kwenye Kituo changu cha Afya cha Iragua tumepata vifaa vya shilingi milioni 25 kutoka kwenye shilingi milioni 150 tangu mwezi wa Tano. Kwenye fedha tuliyoipata tangu mwaka 2018/2019 tumepata vifaa, bado tunadai vifaa vya milioni shilingi 106 kutoka MSD. Sasa hilo ndilo ambalo nililokuwa nataka kulizungumzia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa upana kabisa, kwanza kuna tatizo kwa sababu inaonekana pia Sheria za Manunuzi zimekiukwa kwa sababu supplier huyu anaonekana alilipwa kabla ya ku-supply vitu ambavyo sisi tunavihitaji. Muda unaenda kwa sababu limeshapita, tufunike kombe mwanaharamu apite, ameshalipwa, lakini kwa nini ha-supply? Kitu ambacho nimekiona kwa MSD, na hapa Wabunge wenzangu wapo ni mashahidi, ukizungumza na Ma-DMO wanakwambia kabisa tatizo lipo MSD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa MSD ni kazi inayofanyika kati ya Serikali na MSD. Labda Serikali ituambie kuna tatizo gani kati ya MSD na Serikali? Kwa sababu inaoneka MSD wanafanya kazi vile ambavyo wao wenyewe wanajisikia kufanya. Unalipa hela mwaka 2019, leo miaka mitano vifaa vya shilingi milioni 300 havijafika kwenye hospitali yetu. Leo hii tunataka tudumishe afya bora na huduma bora za afya kwenye maeneo yetu. Namwomba sana dada yangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa sababu amesikia changamoto hii, naomba anisaidie niweze kupata vifaa tiba ili wananchi wake na wananchi wangu pia waweze kupata huduma ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimesimama hapa karibu mara mbili kwenye Bunge hili hili nikitoa maelezo juu ya hospitali yangu ya wilaya ilivyochakaa, ina miaka zaidi ya 60. Mnamo mwaka 2017/2018 tulipata pesa za ukarabati, shilingi milioni 400, ilishindikana kufanya ukarabati kwenye hospitali ile kwa sababu ni hospitali kongwe na ni chakavu. Matokeo yake tukalazimika kuongeza majengo kwenye hospitali ile. Hivi ninavyokwambia sasa hivi, eneo lote limejaa na hatuwezi kufanya ukarabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali kwa sababu ni kongwe, watu walikuwa 50,000 sasa hivi wameshafika kwenye 200,000, hospitali ile haiwezi kuhudumia tena wananchi wale. Ukiacha hilo pia, kuna kaka yangu, ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Biteko, Mheshimiwa Naibu Waziri alijitahidi sana kutafuta wawekezaji kwenye jimbo langu na tumepata makampuni karibu mawili na yote yameshasainiwa mkataba. Wanaenda kuajiri wafanyakazi zaidi ya 1,000 waajiriwa rasmi, na ajira ambazo siyo rasmi ni zaidi ya 3,000 mpaka 5,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, itakuwa ni aibu kubwa sana leo hii wawekezaji wale wanaenda kutafuta hospitali kwenye wilaya inayofuata au mkoani kwa sababu sisi hospitali ya wilaya hatuna. Dada yangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu nilikuomba mara ya mwisho hapa, kama huamini haya ambayo nakwambia, twende ukajionee mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nimeletewa shilingi milioni 900 za ukarabati tena kwenye hospitali ile ile ambayo nimesema kwamba haikarabatiki. Tunashukuru tumepata, lakini tunawaambia kwamba changamoto yetu haikuwa hiyo. Halafu mimi niliyesimama hapa mbele ndio Mwakalishi wa Wana-Ulanga, ndio najua shida za Wana-Ulanga. Leo hii hamnisikilizi mimi, sasa sijui mtakuwa mnamsikiliza nani? Kwa hiyo, namwomba dada yangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu na hili nalo alichukue tusaidiane. Tuna shida ya kupata hospitali ya wilaya kwa sababu kwetu imeshakuwa ni changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda wangu bado unanitosha, naomba nichangie kwenye sekta ya kilimo. Hatuna budi kuwekeza kilimo chetu kwenye skimu za umwagiliaji. Kama tunataka tupate tija kwenye kilimo nchi hii kwa sababu asilimia 80 ya Watanzania ni wakulima, basi ni lazima tuwekeze kwenye skimu za umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu kuna skimu kama nne ambazo zinahitajika kwenye Jimbo langu. Kuna Skimu ya Minepa ambayo haijaisha, lengo iishe iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi. Kuna Skimu ya Lupilo ambayo imeshafanyiwa study, kuna Skimu ya Lukana ambayo imeshafanyiwa study na kuna Skimu ya sehemu moja Kata ya Euga ilijengwa tangu nikiwa mdogo haijawahi kutumika mpaka imeharibika na sijui tatizo ni nini? Huu unaonekana kabisa ni uharibifu wa fedha za Serikali kwa sababu zilitumia fedha kujenga ile skimu lakini haikutumika kwa sababu haikuisha, leo hii tunaenda tena kuianza kuijenga upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo la pili ambalo linaendelea kwenye maeneo yetu kwenye majimbo yetu; suala la stakabadhi ghalani. Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyokuwa Singida alielekeza watendaji wake kwa maana ya Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi waende wakaangalie namna sahihi ya kuliingiza zao la mbaazi kwenye kuliuza kwenye stakabadhi ghalani. Jamani haikuwa sheria, kuna baadhi ya watendaji wetu na viongozi wana tabia ya kumfurahisha Mheshimiwa Rais, hatuko hapa kwa ajili ya kumfurahisha Mheshimiwa Rais jamani. Tuko hapa kwa ajili ya kumsaidia Mheshimiwa Rais na wale ambao huwa wanafanya maamuzi ya kumfurahisha Mheshimiwa Rais mkifika wakati wa uchaguzi hawaingii uwanjani kucheza, wanatuletea shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo wananchi hawako tayari kulifanya, halina afya kwa wananchi wala halina afya kwa sisi viongozi ambao wa kuchaguliwa katika maeneo yetu, kwa sababu ukifanya hivyo wananchi hawa kuna mwananchi analima yuko sehemu ya mbali kabisa ana debe zake mbili ghala liko kilometa 50 kutoka alipo, abebe debe mbili aende akauze, nauli peke yake shilingi 20,000? Hii mimi naona kwa kweli kwa upande wetu halina afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata maghala hayapo, mnataka mtu anafanya implementation kuhakikisha kwamba anatekeleza agizo la Mheshimiwa Rais lengo amfurahishe Mheshimiwa Rais lakini halijamsaidia Mheshimiwa Rais kwa sababu anaowafanyia vile ni wananchi ambao Mheshimiwa Rais mwaka 2025 tunategemea kwamba ataingia uwanjani na wale wananchi tunatakiwa kupata kura kwa ajili yake. Naomba Mheshimiwa Bashe kama unanisikilza hili suala halina afya kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna budi kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake lakini ndani ya hivyo hivyo vitu pia, ndani ya vitu ambayo wanavifanya changamoto bado zipo ndiyo kama hizi ambazo tunazieleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)