Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BALOZI LIBERATA R. MULAMULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii niweze kuchangia kwenye hoja iliyoko mbele yetu. Nimefuatilia kwa umakini sana wasilisho la Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na mjadala unaoendelea niseme tu kwamba wasilisho lake ni zuri sana. Linatupa mwanga wa mbele tunapokwenda na kutupa matumaini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake wa kuiondoa mipango katika Wizara ya Fedha na kuiweka chini ya Ofisi yake. Niseme katika nchi zilizoendelea mipango ndiyo huwa inaelekeza, inaongoza hazina na siyo vinginevyo. Nimefurahi sana kuwaona Waheshimiwa Mawaziri hao wawili Mheshimiwa (namwitaga pacha) Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo wakiwa wameketi pamoja kama mapacha kwa kuwasilisha Mpango wa Maendeleo na Mtazamo wa Bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile ni mara yangu ya kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Kitila Mkumbo kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kuongoza Wizara hii. Kama wengi walivyosema ni msomi mwenye upeo na mawazo mapana, ana uwezo mkubwa na ushawishi mkubwa. Kwa hiyo, sifa zote hizi niseme ni muhimu sana kwa Waziri wa Mipango na sifa hizi zinaonekana pia katika wasilisho lake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kusikiliza wasilisho la Mheshimiwa Mkumbo na Mpango wenyewe niseme nimevutiwa na mambo matatu. Moja ni kuhusu maendeleo vijijini, lakini ya pili ni mabadiliko ya tabianchi, ya tatu ni uchumi wa kijani na uchumi wa buluu (green economy and blue economy). Najua wamegusa maeneo mengi lakini nasema maeneo haya matatu yakisimamiwa vizuri yanaweza kuwatoa Watanzania wengi kwenye wimbi la umasikini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme pia nimesikitishwa kwamba Mpango huu bado haujaupa umuhimu wa kutosha shughuli za utafiti na maendeleo (research and development) imepewa pesa kidogo sana chini ya Sekta ya Elimu ambayo ni kama 0.003% wakati lengo ni kuwa na 1% ya pato la Taifa. Bahati nzuri nimekaa hapa na Mheshimiwa Profesa Mkenda na ninaamini kwamba na yeye pengine ana uchungu kuona kwamba Sekta hii imepewa hela kidogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi bahati nzuri nimekuwa kwenye vyuo vikuu kwa Chuo Kikuu cha George Washington University na nikatumia muda pia kwenye Massachusetts Institute of Technology nikiona wenzetu hela kubwa sana inaenda kwenye R and D. Kwa hiyo, wito wangu kwamba Mheshimiwa Profesa Mkumbo kwa kweli hii muipe umuhimu sana ili tutoboe. Hii kwa kweli hatuwezi kuendelea kuipa peanut. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema nimevutiwa maeneo matatu muda ukinitosha nitaweza kuyaongelea lakini nianze na kuhusu maendeleo vijijini. Tumesikia shule nyingi zimejengwa, vituo vya afya vimefunguliwa, maji yanasambazwa, mambo mazuri sana na kwa lugha nyepesi tuseme Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonyeshwa kuguswa sana na wananchi vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeguswa pamoja na kwamba nimekuwa na nyadhifa mbalimbali nimekuwa nimekaa nchi za nje lakini mimi ni mtoto wa kijijini kama pengine walivyo wengi hapa na nilikuwa najiita I am a rural girl kwa hiyo, nafuatilia sana. Mzee wangu marehemu Mheshimiwa wakati ule marehemu sasa Novat Rutageruka alikuwa akisema, “Ukitaka kupima maendeleo tumefikia wapi tumetoka wapi, tumefika wapi angalia hali ya kijijini.” Kweli alikuwa ananiasa kila wakati anasema nakusikia kwenye mihadhara huko na watu wa World Bank mnatoa takwimu, mnazipata wapi mbona hamtuulizi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasema naguswa sana na hali ya umasikini of course na maendeleo vijijini yanayoendelea na ninaamini kama tutajielekeza kuwapa maarifa na mtazamo wanavijiji baada ya kuwapelekea hizi huduma mbalimbali. Tumesema sasa hivi vijiji vingi vimepata umeme, minara ya mawasiliano imesambazwa lakini wanaitumiaje katika kupata maendeleo ambayo tunayataka?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kijijini kwetu sehemu imeweza kupata umeme lakini kwa watu wetu umeme ni taa na sisi ni watu ambao siyo kama watu wa Kilimanjaro siyo watu wa biashara sana kwa hiyo mtu anafurahia na anawasha taa pengine anaweka na TV. Nadhani wananchi wetu wanataka elimu tuwaelimishe kwamba huu umeme waanzishe viwanda vidogo vidogo, waongeze thamani kwenye mazao yao katika maeneo waliyonayo na hiyo BBT nasema kwamba hiyo BBT ya kilimo ipelekwe pia kwenye masuala haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilikuwa natoa ushauri tu kwamba pengine tufikirie kuanzisha Mamlaka ya Maendeleo Vijijini (Rural Development Authority). Maana yake huko nyuma tulikuwa na Wizara zinazohusika na maendeleo vijijini. Nchi zilizopiga hatua kwenye maendeleo vijijini nyingi zina Wizara na taasisi hizi. Sasa sisi shughuli hii imesambaa kwenye TAMISEMI, Wizara mbalimbali kwa hiyo inakuwa ni vigumu katika kuratibu. Kwa hiyo mimi naamini pengine Mheshimiwa Profesa Kitila anaweza akamshauri Mheshimiwa Rais kuangalia uwezekano wa kuanzisha Rural Development Authority, namuona ana-note kwa hiyo nadhani umelipata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tabianchi pia haina mwenyewe na yenyewe. Mabadiliko ya tabianchi na yenyewe muangalie jinsi gani inaweza ikawa na taasisi mbali na NEMC ya kuweza kuangalia maana yake ni eneo kubwa zuri sana hasa tukiangalia katika carbon credit. Sasa hivi mkutano wa COP 28 unakuja, itatoka maazimio mengine nani anayachukua? Kwa hiyo, nadhani itakuwa vizuri pia katika kutazama uchumi wa green economy. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nadhani itakuwa vizuri pia kuwa na hiyo katika kutazama green economy. Mambo ya uvuvi yameongelewa, lakini nasema hiyo ni sehemu ambayo kwa kweli hatujaitendea haki. Uvuvi tunauona kama ni wa watu maskini lakini ndiyo potential kubwa iliyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabla hujanigongea kengele nyingine, niseme uchumi wa blue nao kwa kweli tujifunze mengi kutoka Zanzibar kwamba wameanzisha Wizara inayohusika na uchumi wa blue. Hii ni kweli kuna fursa nyingi sana ambazo hatujazitendea haki. Maana yake nayo imesambaa katika Wizara mbalimbali na sekta mbalimbali. Tuondokane na dhana ya sector approach. Profesa Mkumbo tuondokane na sector approach tutazame dhana ya uchumi in a holistic manner. Kwa namna hiyo nadhani itaweza kuleta yale ambayo tunatarajia kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba nimpongeze Mheshimiwa Tulia Akson kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa IPU. Ushindi wake umenipa hamasa kwamba mgombea wa nafasi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola kwamba inawezekana. Tukijipanga vizuri na kutumia ushawishi wetu mkubwa kidiplomasia na Kimataifa aliotujengea Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Naomba mniunge mkono, ahsanteni sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa balozi umesema tukuunge mkono au umeunga mkono?
MHE. BALOZI LIBERATA R. MULAMULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
MWENYEKITI: Sawa.
MHE. BALOZI LIBERATA R. MULAMULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo yote, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)