Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijaalia kuwepo hapa na kwa kutujaalia sote. Sina mengi ya kusema zaidi ya kumshukuru Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais yuko katika kipaumbele, hana ubaguzi, ana mapenzi na watu wote hata ikiwemo watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua Waziri wa Fedha ni balozi wa watu wenye ulemavu, katika Bunge la Bajeti alitoa ahadi ndani ya Bunge hili kuwa atatoa shilingi bilioni moja kwa ajili ya maendeleo ya watu wenye ulemavu katika Wizara ya Kazi, Ajira na Watu Wenye ulemavu. Kwa kweli watu wa Mheshimiwa Waziri wanatuangusha, ni kizunguzungu ambacho kinakuwa hakina mwisho, watu wenye ulemavu wanashindwa kufanya kazi zao na wanashindwa kufanya majukumu yao. Hizi hela alizozitenga Waziri shilingi bilioni moja mpaka leo hazijafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani kwa hili ana uwezo nalo. Balozi wangu mtukufu, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba afuatilie hilo suala ili tuondokane na hilo iwe mwisho leo hapa. Tukitoka hapa tunazungumza ukurasa mmoja. Fedha za watu wenye ulemavu zimeingia Wizara ya Ajira, Kazi na Watu Wenye Ulemavu. Mheshimiwa Rais anawapenda walemavu, amekaa nao zaidi ya mara tatu anakula nao chakula Ikulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yeye ni balozi na ni mlezi wa watu wenye ulemavu, tunakwenda na mpira watu wenye ulemavu AFCON, hatuna bajeti na hatuna pesa tangu mwezi Julai. Ilibidi wakakae kambini, hakuna uwezo. Hivyo naamini kuwa balozi wangu atalifanyoia kazi na najua yeye anawapenda walemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, natoa shukrani za dhati, Wizara ya Ujenzi tayari ime-deal na wakandarasi. Wakandarasi walikuja karibu mabasi, amefanya nao kazi na tunaonekana tunakwenda vizuri. Wizara ya Uchukuzi, wakandarasi wa ATCL mafanikio yanaanza kuonekana. Walisema wametoa shilingi bilioni 10 zimepelekwa Hazina; Hazina wanakwamisha, naomba Mheshimiwa Waziri akae nao chini watu wake, hawa watu ni wastaafu, wamenyanyasika kwa miaka mingi sana; wanahitaji wapewe hela zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa watu wa ATCL peke yao, watu 70 wameshafariki sasa hivi, hawakupata mafao yao, ni miaka 10. Watu wa TAZARA wamekufa watu 100 mpaka sasa hivi hawajapata mafao yao. Tumekwenda Wizara zote nimepita kutembea nao wamesema hela zilishapelekwa tayari hazina. Sasa bila Waziri kukaa chini na hawa watu watatu sisi hapa hatuna jibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake itakuwa kila siku hawa wanapanda juu, wanateremka chini. Hakuna majibu, lakini hela zilishatengwa katika bajeti iliyopita, mpaka leo hatujui mafao haya yako wapi. Naomba Mheshimiwa Waziri kwa unyenyekevu na upendo ninaompenda, naomba alisimamie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mjusi, nilisahau kwa muda mrefu. Hili ni pato ambalo nchi italipata kwa kupitia mjusi. Ujerumani inapata pato la dollar bilioni 3.8 kwa watu kutembelea katika eneo lile la exhibition ya mjusi. Leo mjusi ametoka Lindi nilitegemea Rais wa Ujerumani angepewa taarifa kuwa yule mjusi ametoka Lindi na akatembelea Lindi. Amechukuliwa amepelekwa maeneo mengine, sikatai. Vitu walivyoenda kumwambia sijui kuna mafuvu la machifu je, gawio letu la mjusi Mkoa wa Lindi liko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, dollar bilioni 3.8 siyo hela ndogo. Mjusi ametolewa pale hakuna barabara na hakuna shule. Tangu Mwaka 2005 nazungumza lugha ya mjusi, ifikie mahali tujiulize. Haya ni mafanikio ya nchi yetu, wenzetu Namibia wamefuatilia wamelipwa trilioni 4.0 na zinawasaidia. Sisi leo unaona pale hatuna shule, hamna barabara wala nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru Serikali inapambana lakini kuna hela nyingine ni direct huhitaji hata kutumia nguvu, ni hela za mjusi. Natamani nikutane na Rais mwenzangu, maana yake ni Rais wa herufi ndogo, Rais wa Mjusi nilitegemea na yeye tungekutana nikamwambia hiki kilio chetu cha mjusi tunatamani tunataka mapato ya mjusi. Tutaendelea kupigania ni haki yetu ya msingi, watu wa Mipingo, watu wa Matapwa…

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

TAARIFA

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Riziki naomba anivumilie nilitamani ijibiwe kesho, lakini kwa kuwa ameendelea kulisemea na nampongeza kwa namna ambavyo amekuwa ukilisemea suala hili kwa nia nzuri na kwa kweli tunamuunga mkono kama Serikali na Wabunge wengine wote ambao wamekuwa wakilisemea suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na ratiba ya Rais wa Ujerumani alipotembelea Tanzania, walikuwa wameweka schedule yao na waliona watembelee eneo lile kwa muda mfupi waliokuwa nao, lakini pili nimhakikishie kama Serikali tayari kupitia mazungumzo ambayo Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyafanya na Rais wa Ujerumani, tunayo Kamati ya Kiserikali yenye taasisi zaidi ya nane ambayo itasimamia suala hili. Baadaye tutaendelea na majadiliano ambayo Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia ametoa baraka zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tuko katika taratibu za kidiplomasia kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ili sasa mazungumzo rasmi yaweze kuanza. Hiyo inahusianana na art fact zote pamoja na vifaa vingine ambavyo ni kwa ajili ya kumbukumbu ya Tanzania ikiwemo pia na mjusi pamoja na mengneyo. Tuone huko baadaye pia wakirudishwa watatunzwaje pamoja na mengine. Kwa hiyo, nampongeza niliona nisisubiri kesho niliweke hivyo sawa na waunga mkono wote.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Riziki, taarifa hiyo.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Angellah Kairuki. Bunge la Kumi na Moja nilizungumza, Watanzanoia tuwe tunahudhuria mikutano kwa wingi ili tupate nafasi mbalimbali hizi katika umoja wa mataifa. Nampongeza Mheshimiwa Angellah Kairuki amepata nafasi katika UNWTO, hii ni nafasi kubwa kama Makamu wa Rais.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndiyo tunasema tunataka watu waadilifu, watu wanaoona maono kuwa tuna haki ya vitu vyetu kufanikiwa. Kupitia mikutano hii yetu na Spika wa Umoja wa Madola, leo vilevile tuna Makamu wa Rais wa UNWTO, tuna Rais Dkt.Ndugulile…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MH. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja nimalizie.

MWENYEKITI: Sekunde mbili malizia.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia suala la fungu. Kuna shilingi 20,000 za wafanya biashara ndogondogo, tunapoteza nchi. Kama tukipiga hesabu 20,000 kwa watu 30,000 tuna shilingi milioni 600, Wizara nne tayari tutakuwa tumezifanyia kazi.