Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Yustina Arcadius Rahhi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu kipindi kilichopita tulikuwa tunapanga pia vipaumbele na kupitisha bajeti yetu, lakini Mheshimiwa Rais ametoa fedha za utekelezaji wa mpango ambao sasa hivi unaendelea kutekelezwa na ametoa fedha nyingi sana. Nampongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata sasa hivi tukiweka mpango wetu vizuri na vipaumbele vizuri kwa vyovyote vile utapata fedha na utatekelezeka. Pia, nampongeza kwa maono aliyonayo tulikuwa tumetamani sana irejeshwe Wizara ya Mipango na Uwekezaji ambayo sasa amewekeza na tunaomba isimamie rasilimali za Watanzania ziweze kutumika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kupanga ni kuchagua. Tuna mahitaji mengi sana ya wananchi na hasa ukienda vijijini mahitaji ni mengi, kuna barabara ni mbovu zinatakiwa zitengenezwe, kuna vivuko, kuna zahanati na kuna elimu lakini kwa sababu rasilimali hizi ni chache, hizi resource ni scarce, ni lazima tuwe makini kuona kwamba ni vipaumbele vipi vinatakiwa viingie katika mpango wetu huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nampongeza Waziri kwa sababu amekuja na mapendekezo ya mwongozo, kwamba kati ya vipaumbele, kwanza ni kukamilisha miradi mikubwa iliyokuwa inaendela ikiwemo mradi wa reli, wa viwanja vya ndege na hasa huu wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ili tuweze kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme ni hitaji kubwa sana katika kuendeleza uchumi wa Tanzania, lakini sasa nchi mara nyingi tunaingia kwenye mgao wa umeme. Hili jambo ni baya sana, umeme unahitajika, kuna vijana kule wana viwanda vyao vidogo vidogo vya kuchomelea na kadhalika, sasa tunavyokata umeme, tunavyoweka mgao kwa kweli ni changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbe tungeweza kuweka kipaumbele kikubwa kwa kuachana na hii changamoto ya upungufu wa umeme, kwa sababu kwanza rasilimali za kuzalisha umeme tunazo, tumebarikiwa na Mungu tunaweza kuzalisha umeme hata kutoka kwenye vyanzo vya jua, akazalisha mtu mmoja mmoja tukaingiza kwenye gridi ya Taifa. Tunaweza kupata umeme pia kutoka kwenye vyanzo vya upepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaongea kila siku habari ya gesi asilia ambayo pia inaweza ikazalisha umeme. Tunaongea habari ya gesi kule Mchuchuma na Liganga ambapo watafiti wanasema kuna takriban shilingi bilioni mbili potential ambazo pia tungeweza kufua umeme kutoka huko wa kati ya megawatt 600 mpaka 900 tukaweza kuingiza kwenye gridi ya Taifa, tena kwa gharama ndogo ya shilingi 103 mpaka 108 kwa unit. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema kipaombele changu kingine ni kuwekeza katika viwanda. Tumeona nchi zote zilizofanya vizuri katika uchumi wamewekeza kwenye viwanda na sisi tunasema dhima ya uchumi wetu ni uchumi shindani. Tunawezaje kwenda kwenye uchumi shindani kama hatufikirii habari ya viwanda? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna changamoto nyingi kwenye viwanda, tuna viwanda vidogo vidogo vingi ambavyo vinachukua karibu asilimia 98. Kwa mfano, tuna viwanda vidogo vidogo sana 62,400 ambayo ni asilimia 77 ya viwanda vyetu. Tuna viwanda vidogo 17,274 ambayo ni sawa na asilimia 21, tuna viwanda vya kati 684 ambayo ni asillimia 0.8 na tuna viwanda vikubwa 618 ambayo inaenda asilimia 0.76. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda hivi vidogo bado vina mahala pake. Tunajua umuhimu wa viwanda, vinaweza vika-absorb nguvu kazi kubwa ambayo kila siku inakimbizana na ajira. Vilevile, viwanda hivi vinasaidia, kwa mfano agro-processing viwanda, kufanya value chain ya mazao yetu na tukapata faida. Changamoto kubwa ya viwanda hivi vidogo vidogo ni mitaji. Serikali iwasogelee hao wenye viwanda vidogo vidogo, pengine ni vikundi vya kina mama, wengine wanafanya usindikaji wapate mitaji, skills na knowledge pamoja na masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa nasema habari ya viwanda hivi vya kati na viwanda vikubwa kuviboresha, kwa mfano viwanda ambavyo mahitaji yake ni makubwa Tanzania. Kwa mfano, kiwanda cha mbolea tuna viwanda viwili tu vya mbolea, kiwanda cha Minjingu pamoja na Intracom ambapo inazalisha mbolea kidogo. Minjingu kinazalisha tani 100,000 na hiki kingine kinazalisha tani 250 mpaka tani 300 na mahitaji ya mbolea ni zaidi ya tani 1,000,000. Sasa tunaagiza na kuweka mbolea ruzuku, natamani nguvu zote hizi tungewekeza katika kujenga viwanda vya mbolea ili tuweze kujitosheleza kwa mbolea.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna viwanda vya saruji pamoja na chuma. Nasema Watanzania wamekubali kupata maendeleo na kujenga makazi bora, lakini saruji na chuma bado bei yake imekuwa ni kubwa sana. Naiomba Serikali iweze kuwekeza katika viwanda hivyo ili Watanzania waweze kwenda kwenye makazi bora. Tunajua ni matokeo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kupeleka fedha nyingi katika lower level ambapo imeongeza mzunguko wa hela. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule ambapo Mama Lishe, vijana na maduka madogo madogo wameweza kuzungusha hizi hela na kwa ajili hiyo watu wameamua kujenga makazi bora, lakini ukienda saruji inauzwa ghali, chuma inauzwa ghali. Tuna uwezo mkubwa sana wa kuweza kuzalisha saruji yetu wenyewe pamoja na chuma kwa sababu malighafi zote ziko huku. Changamoto ni kusafirisha hizi malighafi kutoka kule kusini, kwa mfano gesi asilia inayotoka kwenye makaa ya mawe, huko chini tunaomba reli ijengwe. Wameongea sana Wabunge wa Songea na wote wa Kusini, kuna umuhimu sana wa kujenga reli. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante, kengele ya pili imepigwa, ahsante kwa mchango mzuri.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.