Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii niwe sehemu ya wachangiaji kwenye Mpango wa Maendeleo wa Mwaka Mmoja. Natumia fursa hii kwanza kupongeza juu ya utekelezaji wa Mipango iliyopita na huu ambao tupo nao. Naunga mkono, nasema hongereni sana Wizara kwa Mipango hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo tumeweza kuona Mipango iliyopita, utekelezaji umeenda siyo vibaya, unaenda vizuri. Mpango huu ambao tupo nao wa Bajeti ya shilingi trilioni 47 na fedha za miradi ya maendeleo, tuna shilingi trilioni 15 ambapo iko ndani ya makubaliano kati ya asilimia 30 mpaka 40, na mpango huu una asilimia 33. Kama fedha zote hizi ambazo tumezitenga za shilingi trilioni 15 tutazitoa na kuzipeleka kwenda kwenye miradi ya maendeleo, tuna hakika Taifa letu litapiga hatua kubwa na kuleta maendeleo chanya kwa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi kwa Serikali kuhakikisha fedha hizi ambazo tunazitenga kupitia mipango yetu, zitoke ziende kutekeleza. Tukifanya hivyo, Taifa litapiga hatua. Mfano, tumeweza kuona Mpango huu ambao tunatembea nao, ambao unatekelezwa kupitia Bajeti ambayo tumepitisha mwaka jana 2022/2023, tulitenga fedha nyingi kwenye upande wa kilimo. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais, ameleta mabadiliko makubwa sana kwenye Sekta ya Kilimo kwa fedha nyingi ambazo amewekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo zamani miaka miwili nyuma Bajeti ya Kilimo ilikuwa chini ya shilingi bilioni 250. Tumetoka shilingi bilioni 250 kwenye Bajeti ya Kilimo tunazungumzia karibu zaidi ya shilingi trilioni moja. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa nia ya dhati kuhakikisha kwamba anakikomboa kilimo chetu. Tumeona fedha nyingi zimetolewa kwa ajili ya kuboresha, kuchimba mabwawa makubwa na pia kujenga schemes za umwagiliaji. Hii inaonesha nia ya dhati ya kumkomboa Mtanzania maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba katika fedha hizi zinazotolewa kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa. Najua Mpango huu ni mwendelezo wa kuhakikisha kwamba tunajenga mabwawa makubwa ya kuhifadhi maji. Tulikuwa tunalalamika miaka ya nyuma maji yanapotea na mvua zinanyesha; tunapata mvua za kutosha lakini hatujawekeza kwenye kuyapokea yale maji na kuyatengenezea mazingira ya kuyalinda kwa ajili ya manufaa ya kilimo, mifugo yetu na kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili nawapongeza. Nataka kutoa ushauri kwenye masuala mazima ya uchimbaji mabwawa. Naweza nikatolea mfano Jimboni kwangu Manonga, Wilaya yetu ya Igunga. Tumepata fedha za kuchimba mabwawa, lakini moja ya changamoto ambayo tunaiona, tunaichukua ardhi kubwa, tunachimba mabwawa kwa ajili ya kupata maji, lakini mabwawa haya ni makubwa ambayo yanachukua karibu vijiji vinne au vitano. Sasa wanufaika wa bwawa zima unaweza kukuta ni vijiji viwili, vile vijiji vitatu maana yake wao hawatapata. Kama walikuwa wanalima, maana yake wakitoa lile eneo, hawatalima tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, sisi pale Chomachankola tuna Kijiji kinaitwa Bulangamilwa, kutoka Kijiji cha Bulangamilwa mpaka Choma ni kilometa 12. Kijiji hiki ni sehemu ya vijiji vinavyotoa eneo kwa ajili ya bwawa kubwa kwa kilimo cha umwagiliaji. Wanaoenda kunufaika na bwawa hili ni Kijiji cha pili kinachoitwa Choma. Sasa hawa watu wa Bulangamilwa wanaotoa eneo lao ambalo ndilo wanalotumia kwa ajili ya kilimo. Wakishatoa lile eneo, hawana eneo lingine la kulimia. Tafsiri yake ni nini? Hao wananchi wanahitaji tutenge fedha za kuwapa angalau fidia wapate fedha waweze kwenda kutafuta maeneno mengine. Kumchukulia mtu eneo lake bure, haumpi fidia, unapelekea kumkosesha uhuru wake. Unamnyang’anya eneo ambalo alikuwa akipata uchumi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara, tutoe fidia kwa wale wananchi wa Kijiji cha Bulangamilwa na vijiji jirani Kwanzega, kwa maana ukichukua ardhi yake hatapata sehemu nyingine ya kupata uchumi. Naiomba sana Wizara. Unaponiambia kwamba utampa mashamba eneo la pili, hujaweka mpango wa kwenda kumnunulia na hujui unaenda kuchukua eneo la nani? Kwa sababu yale maeneo ya vijiji vingine yana watu ambao wanayamiliki. Fidia yenyewe haifiki hata shilingi milioni 200 au 300. Unaenda kuweka mradi wa bwawa la zaidi ya shilingi bilioni tano, lazima Serikali iweke fedha za kumfidia huyu ambaye anachukuliwa eneo lake ambaye hana tena sehemu nyingine ya kwenda kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na watu wa Mipango kuhakikisha kwamba watu wa Bulangamilwa wanaangaliwa. Mheshimiwa Waziri Bashe, kule Nzega ambako ni Nzega Vijijini, wananchi wanalia kwa sababu maeneo yao yanachukuliwa, na wewe ndiye mwenye eneo lile. Naomba sana mwangalie jinsi gani ya kuwasaidia hawa wananchi. Kwa sababu kuna wananchi wana makaburi ya wazazi wao wanatakiwa walipwe fidia. Kuna watu wana nyumba zao zinabolewa, wanatakiwa walipwe fidia, kuna watu wana majaruba ambao ndiyo uchumi wao, unapochukua na kuchimba bwawa inatakiwa umpe fidia ili anapoenda akatafute sehemu nyingine kuliko kumwambia sasa atanufaika na bwawa wakati hana eneo lingine kwa ajili ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwambia Mheshimiwa Waziri, unapochukua lile eneo, tulipe fidia katika yale baadhi ya maeneo kwa sababu siyo fedha nyingi. Pia hawa watu wana uchumi. Kwa hiyo, tusiwafanye wananchi wetu wakawa maskini. Hatuwezi tukawaambia wananchi wetu sasa wahamie kwingine. Watapata fursa ya mabwawa, ndiyo, lakini hana ardhi ya kulima, analima wapi? Ardhi nyingine inayobakia ni dhahabu. Hawezi kwenda kuchimba dhahabu kwa sababu maisha yake ni kulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Wizara, hawa watu mkichukua maeneo yao mwangalie namna bora ya kulipa fidia. Haiwezekani mumchukulie mtu eneo lake, umwambie utanufaika na hili bwawa, utaogelea humu, utavua samaki humu. Sasa kuvua samaki, ndiyo atavua, kama ataendelea kupata eneo lingine ambalo litamsaidia kuweza kufanya kilimo akapate chakula. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, mwangalie katika suala zima la haya mabwawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mfano wa Choma lakini naamini ni nchi nzima tunafanya hivyo. Kwa wale ambao watanufaika na lile eneo la kupata maji, hiyo haina shida, watapata maji, yatakayoingia kwenye majaruba yao. Kwa wale ambao hawatanufaika na yale maji maana yake wapewe fidia ili wahame katika yale maeneo waende maeneo mengine waweze kuanza maisha mapya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo tutawatia watu wetu umaskini na hali ambayo italeta mgogoro mkubwa kati ya wananchi na Serikali yao. Nawaomba sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo hili suala alichukue…


MWENYEKITI: Ahsante. Kengele ya pili.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono Mpango, uko vizuri, lakini mwangalie jinsi gani ya kuboresha katika malipo ya fidia kwa watu mliochukua maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuchangia kwenye huu Mpango wa Serikali wa Mwaka mmoja. (Makofi)