Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia ripoti hizi tatu, Ripoti ya PAC, PIC, LAAC. Pia, nichukue fursa hii kwanza kabisa kumshukuru Mungu Azza wa Jalla kwa kunijalia siku ya leo kuamka salama na mimi kupata nguvu ya kuchangia ripoti hii ya leo. Pia, nimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya.

Mheshimiwa Spika, anafanya kazi kubwa sana kuhakikisha ya kwamba anatutafutia fedha nyingi sana na kuzileta hapa nchini ili ziweze kutekeleza miradi mbalimbali. Ni ukweli usiopingika, mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anapambana usiku na mchana kuhakikisha ya kwamba taifa letu la Tanzania linajenga mahusiano mazuri nje ya nchi lakini pia, linatengeneza fursa ya kupatiwa fedha mbalimbali zinazokuja hapa nchini ili ziweze kutekeleza miradi hii.

Mheshimiwa Spika, nilishuhudia siku moja nikiwa kwenye mkutano mmoja, siku ya walimu duniani. Mheshimiwa Rais alipiga simu akaongea hadharani kuwapongeza walimu siku yao ya walimu Tanzania.
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo alisema yupo safarini anaelekea India na akasema ninaenda India wanangu kwenda kuwatafutia fedha. Ni ukweli usiopingika kwamba Mheshimiwa Rais amekuwa na kasumba ya kusafiri kwenda kutafuta fedha na fedha hizo zinakuja kwenye nchi yetu ya Tanzania. Kazi ya kusafiri kwenye ndege si kazi rahisi. Inawezekana watu wengine wakahisi kusafiri kwenye ndege ni furaha na starehe, kazi ya kusafiri na ndege ni kujitoa muhanga kwa sababu, wakati wowote ule likitokea la kutokea wewe safari yako imeishia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kazi ya kusafiri kwenda kutafuta fedha si kazi rahisi. Hivyo, hatuna budi sisi kama Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumsaidia kuhakikisha kwamba fedha ambazo anazileta hapa nchini zinaenda kufanya kazi iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, sitaki kurudia, mambo mengi yamezungumzwa hapa. Amezungumza Mheshimiwa Luhaga Mpina juu ya Lot namba 3&4 ya reli, wamezungumza hapa habari ya TANOIL, wamezungumza hapa habari ya fedha ambazo zimepotea katika ukusanyaji wa mapato kwenye halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, mimi niseme, inawezekana chanzo cha upotevu wa fedha, chanzo cha mafisadi kwenye nchi hii ni kizazi ambacho sisi wenyewe tumekiandaa. Mimi ninapenda kuchukua fursa hii kuishauri Serikali. Moja, iweke utaratibu kabla ya vijana wetu na vijana wenzetu kupatiwa ajira, moja kuanzishwe chuo maalumu cha uwajibikaji ili kabla ya watu hawa kwenda kuajiriwa Serikalini wapite kwenye chuo cha uwajibikaji ambacho kitakachowafundisha namna bora ya kwenda kuwajibika kwenye taifa letu hili la Tanzania.

Mheshimiwa Spika, sambamba na kuwaelekeza wawe wazalendo kwa nchi yao hii ili waweze kutimiza majukumu yao ya kuwasaidia Watanzania. Ninaamini kabisa, kama mpango huu utaanzishwa unaweza ukarekebisha taifa hili la Tanzania kuwa na watumishi ambao wana maadili.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba, hapa tunapozunbgumza ninaona Mawaziri hapo wanachati. Mawaziri acheni kuchati, nisikilizeni hapa. Tusikilizeni. Mnanong’ona nini hapo? Lengo sisi hapa tunataka tuwasaidie nyinyi. Tunataka tumsaidie Mheshimiwa Rais fedha hizi zinazotafunwa za wananchi walipa kodi… (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Mbunge anachangia tujitahidi kusikilizana, tupunguze sauti tafadhali. Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Niseme tu Waheshimiwa Mawaziri mtuheshimu Wabunge, heshimuni Wabunge. Nyinyi mmekuwa tukiwapigia simu, amezungumza Mheshimiwa Maganga hapa, mimi nampinga kwamba Wabunge tunafanya nini?

Mheshimiwa Spika, Wabunge tunatekeleza majukumu yetu huko tunapoona ubadhirifu kwenye maeneo yetu huwa tunawatumia meseji na kuwaeleza Waheshimiwa Mawaziri juu ya mambo yanayoendelea kule lakini hawachukui hatua. Ninao ushahidi hapa kwenye meseji, sitaki kumtaja leo, nimemtumia Waziri kumweleza juu ya fedha ambazo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta kwa ajili ya ujenzi wa shule na shule hiyo haijakamilika.

Mheshimiwa Spika, nimemtumia meseji kumweleza juu ya fedha za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta kwa ajili ya kukamilisha zahanati hazijakamilisha na zimeibiwa fedha lakini hawajajibu na hakuna hatua zozote zile zinazochukuliwa, matokeo yake wanatuchonganisha Mawaziri na watumishi wetu kwenye maeneo yale. Tunapowaambia matatizo ya fedha kuibiwa kwenye maeneo yetu wanarudisha taarifa kwa watendaji wetu wa kule kututengenezea fitina sisi Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, hii haikubaliki, haikubaliki, mtaona ya kwamba labda tunawaonea wivu lakini hatuwaonei wivu, sisi tuko hapa kuwasaidia wananchi, tuko hapa kumsaidia Mheshimiwa Rais.

SPIKA: Mheshimiwa Kassim kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jerry Silaa.

TAARIFA

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa rafiki yangu na swaiba wangu Mheshimiwa Iddi Kassim kwamba hoja ya Mheshimiwa George Simbachawene ya jana iliyoungwa mkono leo na Mheshimiwa Maganga ya wajibu wa Waheshimiwa Wabunge kwenye halmashauri zetu ni hoja ya kisheria na kikanuni; kwamba sisi ni wajumbe wa kamati za fedha na uongozi kwenye halmashauri zetu. Kwa hiyo masuala ya usimamizi wa fedha kwenye halmashauri sisi tuna nguvu ya kikanuni ya kusimamia kwenye halmashauri zetu na hatupaswi kutuma meseji kwa Waziri bali kutimiza wajibu wetu kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa. (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, jambo analolizungumzia Mheshimiwa Waziri Silaa liliombewa mwongozo hapa na kiti hakijatoa bado mwongozo. Sasa, pamoja na sheria kusema hivyo kama huo ndio uelewa sisi kama Wabunge sina hakika kuna Mbunge atasimama hapa ambaye halmashauri yake haipo kwenye taarifa ya CAG, kwa sababu kama sote taarifa zetu mbaya ziko kwenye taarifa ya CAG na sisi ni sehemu ya hicho kilichotokea hatuna sababu ya kukaa hapa ndani tukawa tunajadili hii taarifa. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, natoa huu ufafanuzi kabla ya mwongozo ili tuelewe tunasimama wapi. Huwezi kuwa mwamuzi kwenye kesi inayokuhusu; na kama sisi Wabunge kila mmoja wetu anahusika kwenye halmashauri zetu ambao ndio uhalisia; kama kila mmoja wetu anahusika na ule ubadhirifu iliofanywa kule hatuna mamlaka sasa hivi ya kukaa hapa ndani kujadili hiyo taarifa. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, maana yake tutafute chombo kingine cha kujadili jambo hili na kufanya maamuzi. Kwa hivyo kwenye hili kwa sababu mwongozo uliombwa na haujatolewa tusubiri Mwongozo wa Kiti haya ni maelezo ya awali. Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi malizia mchango wako. (Makofi/Vigelegele)

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, lakini pia rafiki yangu Jerry mimi na wewe tunaheshimiana sana. Tulipo hapa tupo kumsaidia Mheshimiwa Rais hatuko hapa kutetea majambazi, hatuko hapa kutetea wizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesema kwamba kianzishwe chombo cha kufundisha uwajibikaji kabla ya watumishi kwenda kupata ajira mpya Serikalini. Ni ukweli usiopingika karne ya sasa mtumishi yeyote yule akiajiriwa leo anataka aanze kuishi maisha kama ya Mo Dewji, anataka aanze kuishi maisha kama ya GSM na watu wengine, matokeo yake yanapelekea ubadhirifu mkubwa kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, imetajwa hapa moja ya Halmashauri ya Ushetu ambayo ni miongoni mwa Halmashauri inayopatikana kwenye Wilaya ya Kahama. Mimi nimpongeze CAG kwa kazi kubwa anayoifanya pia na mimi leo niseme kwamba CAG naye tuone namna ya yeye kurekebisha kuanzia ngazi ya mkoa kwenda huko na wao wana changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi halmashauri yangu imetajwa kuwa ni halmashauri iliyopata hati safi lakini mpaka mwenyewe najishangaa wakati mwingine hii hati safi tumeipataje! Yaani mimi mwenyewe najishangaa. Kuna ubadhirifu mkubwa unafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii utaona kuna fedha za miradi ya CSR iko kule inatafunwa, kuna fedha zinapelekwa kule hazikamilishi miradi. Tumesema kwamba fedha zinakuja ziende zikakamilishe miradi, tumepewa fedha za kujenga shule, shule hajakamilika mpaka leo, matokeo yake ni nini? Matokeo yake wanaanza kutafuta fedha (cash) kwenye mapato ya vyanzo vingine wanaenda kuziba mapengo kwenye fedha ambazo zimeletwa na Mheshimiwa Rais zikamilishe miradi. Miradi haiendelei, fedha ile ambayo ingeenda kutumika kujenga darasa lingine inatumika kuziba mwanya wa wizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu unafanya kazi kubwa mno. Mimi wakati mwingine huwa nakuonea huruma, unazungumza mpaka sauti inakwama, majambazi haya hayakomi. Nikuombe utembelee pia Wilaya ya Kahama uangalie uone ni nini, inawezekana Halmashauri ya Ushetu kupata hati chafu ni kwa sababu kipindi hicho Mkurugenzi hakuwepo, hawa pia huwa na wenyewe…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, Taarifa

SPIKA: Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi muda wako umekwisha.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana ninaunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)