Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru na mimi kunipatia nafasi ili niweze kutoa mchango wangu wa hizi taarifa zetu za Kamati za Bunge tatu.
Mheshimiwa Spika, pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na uhai na tatu niwapongeze Kamati hizi tatu kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kwa maslahi mapana ya Taifa letu na Watanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, hii ripoti wakati inasomwa mbele ya Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Rais alikasirika na alichukia sana kitendo hiki cha ubadhirifu ndani ya Taifa letu. Lakini kinachonisikitisha ni Mawaziri wetu ambao ni wasaidizi wa Mheshimiwa Rais kutetea ubadhirifu ambao umefanyika huko chini kwa watendaji wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuko hapa si kwa maslahi ya mtu mmoja mmoja anayesimama kuchangia hoja hizi, tuko hapa kwa maslahi ya Taifa letu; na hiki tunachokisema Waheshimiwa Wabunge si kwamba tunawachukia Waheshimiwa Mawaziri bali tunataka Waheshimiwa Mawaziri watimize na wao wajibu na majukumu yao ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kwenye nafasi walizonazo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapa leo miradi ya maendeleo huko chini iliyopo asilimia kubwa Watanzania wanachangishwa na kwenda kujitolea nguvu kazi kwenye maeneo yao. Na Wakurugenzi wetu wanapoambiwa kwenda kumalizia kazi zile ama miradi ile ya maendeleo kwenye maeneo yetu Wakurugenzi wamekuwa wakisema hawana fedha za kwenda kumalizia miradi ya maendeleo ambayo wananchi wetu wamejitolea.
Mheshimiwa Spika, lakini kwenye taarifa ya CAG hapa nianze kuzungumzia halmashauri tu kushindwa kukusanya shilingi bilioni 37 kwenye vyanzo ambavyo vipo. Shilingi bilioni 37 halmashauri zimeshindwa kukusanya, Serikali inajua, Mawaziri wenye dhamana mpo na mnajua hamjachukua hatua. Tukisema mnakinga kifua hamtaki tuyaseme haya, mnachotaka tufanye ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, halmashauri zinajulikana zimetajwa tangu mwezi wa nne wamesema halmashauri zimeorodheshwa hapa zimeshindwa kukusanya hiyo fedha bado Mkurugenzi yuko ofisini, bado watendaji wako ofisini, wanalipwa mshahara, miradi ya maendeleo Watanzania wajitolee, Watanzania wachange na kodi wamelipa, hiki kitu hakiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ambazo zimeshindwa kukusanya fedha hii, hao wakurugenzi na watumishi waliopo hawafai, wameshindwa kazi, wakapumzike tutafute watumishi na watendaji wengine waweze kwenda kutimiza huu wajibu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala hili leo Watanzania vijana wako wengi huko mtaani, wamebeba mabegi yana vyeti wanahangaika kutafuta kazi; ni kwa nini tunaendelea kuwakumbatia watu ambao hawako tayari kufanya kazi ya kuwatumikia Watanzania? Isitoshe Watanzania hawa ambao wanafanya ubadhirifu wamesoma na kodi za Watanzania. Mama zetu huko vijijini ndio wametengeneza pombe, wamelima kwa shida bila pembejeo, bila mbegu bora, bila usimamizi mzuri, mvua za shida, kilimo duni wamelipa kodi hatimaye leo watu wachache ambao wamepewa dhamana na Watanzania wenzao wakasimamie rasilimali zao wanakwenda kufanya haya wanayoyafanya. Kama Taifa hatujitendei haki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la Halmashauri kufanya malipo ya shilingi bilioni 11.78 bila viambatanisho, hivi hata haya nayo Waheshimiwa Waziri mnataka nako mkinge kifua? Kanuni na sheria zinaelekeza kila Afisa Masuuli anapolipa chochote ni lazima alipe kwa kutumia viambatanisho aoneshe kalipa kitu gani; hawafanyi hivyo. Shilingi bilioni 11, washikaji wamelamba wametulia wanakula bata na wanasema hata wakipeleka huko wataenda watapiga kelele watatuacha maisha yataendelea; na ndivyo ilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaletewa taarifa hizi hapa tunazijadili, tukimaliza hakuna hatua yoyote inayochukuliwa; hatujitendei haki na mnavyofanya hivyo hamumkomoi mtu yeyote, tunalikomoa Taifa letu la Tanzania na kizazi chetu kinachokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika malipo au madeni ya watumishi wetu wanaodai. Watanzania wenzetu ambao tumewapa majukumu ya kutusaidia huko chini wanadai shilingi bilioni 119. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninajiuliza, hivi humu ndani leo ni Mbunge gani anayeidai Serikali hata shilingi mia? Nani Mbunge humu ndani asimame anyooshe kidole kwamba mimi naidai Serikali? Lakini hawa watumishi wana madai miaka mitano, miaka kumi, miaka ishirini na ni haki yao hawaombi wamefanya kazi, wanadai stahiki yao miaka na miaka bilioni 119, watumishi wanaofanya kazi; Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamesema; mtu huyu unataka awe na morali ya kwenda kufanya kazi? Umempelekea shilingi 2,000 ataenda kuitumia kwenye kazi uliyomtuma? Lazima aichukue.
Mheshimiwa Spika, haya madeni ni ya miaka mingi, Halmashauri ya Chemba kuna watumishi 79 wanaodai madeni yao tangu wakiwa wako Kondoa mpaka leo Halmashauri ya Chemba iko pale hawajalipwa hela zao za likizo, hawajalipwa malimbikizo yao ya mshahara, hawajalipwa hela zao za uhamisho, hawajalipwa madeni mbalimbali, kwa nini hatuwalipi?
Mheshimiwa Spika, hela za kuiba zipo, hela za kulipa watumishi wetu hazipo. Hiki kitu hakiwezekani, hawa watu ni lazima Waziri mwenye dhamana kwa kuwa kuna hela ambazo zinachezewa huko chini tunaomba watumishi wetu wanaodai hizi shilingi bilioni 119 waende wakalipwe fedha hizi.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, taarifa.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, kwa sababu Halmashauri zina uwezo wa kulipa ndio maana zinaiba.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, taarifa.
TAARIFA
SPIKA: Mheshimiwa Kunti Majala kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jesca Msambatavangu.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, naungana na Mheshimiwa Kunti nataka nimpe taarifa pia; katika madeni ya watumishi kuna wazee ambao wamestaafu milioni 309 ambao hawajalipwa hela zao za kurudi vijijini sasa sijui wako wapi?
SPIKA: Mheshimiwa Kunti Majala unaipokea taarifa hiyo.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na unacheka si kwa sababu una furahi bali unaumia ndani ya moyo hivi vitu vinakwaza vinaumiza. Sisi kama wawakilishi, sisi kama watumishi wa umma tunaowahangaikia Watanzania, hivi ni kwa nini mzee aliyezeeka shilingi milioni 300 ya mzee aliyelitumikia Taifa hili kweli Serikali inashindwa kulipa?
Mheshimiwa Spika, mimi nikuombe, kama sio kikao hiki basi kikao kijacho, hebu usitulipe Wabunge na sisi tuonje uchungu wa kutokulipwa, usitulipe. Mwezi huu usitulipe mshahara na posho zile zingine Bunge lijalo usitulipe ili tuonje uchungu huu ambao wanakumbana nao Watanzania wenzetu waliolitumikia Taifa hili pamoja na wazee wastaafu waliostaafu ambao mmeshindwa kuwalipa fedha zao. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Ngoja kwanza, subiri kwanza Mheshimiwa. Waheshimiwa Wabunge kuna hoja imetolewa hapa wanaounga mkono hoja, hakuna, haya ahsante sana. (Kicheko)
Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Kunti Majala kuna mmoja ameunga mkono kwa hiyo ni wachache, Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nilitaka kumpa taarifa mchangiaji anayechangia vizuri kwamba jukumu la kuwalipa hawa ambao hawajalipwa ni la Serikali, kwa hiyo ambao mishahara yao izuiliwe ni ya Mawaziri wote. (Kicheko)
SPIKA: Haya ahsante sana. Naona hoja nyingine imetolewa sasa hiyo sitaitoa ili nione nani anaunga mkono. (Kicheko)
Mheshimiwa Kunti Majala malizia mchango wako. (Kicheko)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nilikuwa nimesema hii nilikuwa nataka nione ni kwa namna gani Mawaziri wanauwezo wa kunyoosha mikono kwa makosa yao wenyewe ya kutokusimamia watumishi wetu kule chini ili watendaji wengine waweze kulipwa haki zao watanyoosha mikono.
Umeona uzalendo wa Mawaziri wetu, kosa wanafanya wao, wameshindwa kuwasimamia watu kule chini wameshindwa kunyoosha mikono wasipate mishahara; ubinafsi uliopitiliza na unafiki uliokithiri. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
Timizeni wajibu wenu na majukumu yenu wasaidieni Watanzania walioko kule chini, acheni kula nyinyi raha wenzeu wanateseka.
SPIKA: Mheshimiwa Kunti Majala.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, Waziri una gari, mtumishi anatembea kijiji kilometa 20, 30 hana gari, hana mafuta anatembea kwa miguu.
SPIKA: Mheshimiwa Kunti muda wako umeshaisha. Mheshimiwa Waziri amesimama; Mheshimiwa Waziri.
TAARIFA
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, ninaheshimu sana mchango wake; lakini kwa kweli kwa sababu tu muda wake umeisha. Kanuni zetu haziruhusu kutumia lugha za kuudhi na lugha zinazodhalilisha watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba hili nizungumze kwa muktadha wa Bunge lako, ninaamini kabisa hakuna Waziri yeyote ambaye amesimama hapa akajipiga kifua mbele anatetea ubadhirifu wa fedha hizo ambao umekuwa ukifanywa na Watumishi wa Serikali; hayupo. Tunachokisema; na tutapata muda hapa; tunachokisema hapa ni kwamba ziko hatua zilizochukuliwa labda kwa mfumo, utamaduni wa kuendesha mijadala hapa Bungeni tutakapopata fursa ya kueleza mafanikio ya kazi nzuri ya Serikali hii inatokana na kazi nzuri iliyofanywa pia na Mawaziri katika udhibiti kama mnavyotuagiza Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa kweli hizo lugha hata sisi zinatusikitisha hatuwezi kuambiwa lugha hizo ambazo kwa kweli siyo za kistaarabu.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri nisaidie ili niweze kufanya maamuzi, ni maneno gani ya kuudhi ili nataka niyafute.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, ninaomba sana kiti chako ikiwezekana na ikikupendeza lugha ya kwamba Mawaziri ni wanafiki siyo kweli. Hatukai hapa na hatujakaa hapa tukiwa wanafiki katika kuisaidia hii Serikali yetu. (Makofi)
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kama nilivyokuwa nimesema muda wa Mheshimiwa Kunti ulikuwa umeshakwisha na hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi inahusu utaratibu kwa maana ya matumizi ya lugha ambayo kanuni zetu zinakataza. Kwa hivyo katika mchango wa Mheshimiwa Kunti Majala maneno ambayo yametokeza kwa namna ya kuashiria Mawaziri ni wanafiki yanaondoka kwenye Taarifa Rasmi za Bunge. (Makofi)