Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii nami niweze kuchangia. Kwanza kabisa kabla sijasahau, niseme naunga mkono hoja za taarifa za Kamati zote tatu.
Mheshimiwa Spika, kwanza nami napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi ambazo ametuletea katika Halmashauri yetu ya Mji wa Ifakara na Jimbo la Kilombero. Sasa hapa lazima tutofautishe kuletewa fedha na matunda ya zile fedha katika miradi ile.
Mheshimiwa Spika, ukienda huko kwenye kuona miradi kutokana na fedha ambazo Wizara ya TAMISEMI imetuletea na Mheshimiwa Rais ametuletea ni vitu viwili tofauti na ni vitu viwili mbalimbali. Napenda sana kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea Mkuu wa Mkoa wetu, Dkt. Malima na Mkuu wetu wa Wilaya, Dunstan Kiwobya. Waziri wa TAMISEMI na viongozi nataka niwaambie, kama sio huyu DC mpya aliyekuja, Wakili Dunstan Kiwobya, basi miradi yetu ingekuwa mibaya mara tatu. Huyu Mkuu wa Wilaya aliyekuja naye ameshaanza kuletewa chuki na hao ma-tycoon wa Halmashauri kwamba anaingilia mpaka kwenye kusimamia, mpaka kwenye kufunga taa usiku ili miradi iende. Kwa hiyo, pamoja na hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kweli, kwa mabadiliko haya ya kutuletea Mkuu wa Wilaya, yamesababisha angalau kidogo miradi ya Halmashauri tunaanza kuiona.
Mheshimiwa Spika, nitagusia upande wa TAMISEMI. Najua maeneo mengi sana yamesemwa kuhusu wizi na ubadhirifu, lakini nataka kusema kwenye TAMISEMI na Halmashauri kwa sababu nilikuwa Mjumbe kwenye Kamati ya LAAC, na tuliyaona mengi sana na mengine leo yanajirudia yale yale. Tulikuwa na Mwenyekiti wetu, mama pale katika Kamati ya LAAC.
Mheshimiwa Spika, nina imani sana na Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Mchengerwa. Kwa kweli, kwa dhati ya moyo wangu nina imani naye sana kwamba atafanya mabadiliko. Kwa nini nina imani na Mheshimiwa Mchengerwa? Kwa sababu, ameteuliwa tu, ameenda kule Lindi na Mtwara akazitaja Halmashauri ambazo miradi mibovu na miradi haiendi. Hata sijamlalamikia, hata sijamwambia, kataja huko kwenye vyombo vya habari, nikasema eh, Waziri ndio huyu sasa tumempata. Basi hatua zitachukuliwa na tutaona mabadiliko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kule kwangu, Mheshimiwa Waziri Mkuu, wameiba mpaka vile vifaa vya maafa ya mafuriko ulivyonipa. Mimi nimepata mafuriko Ifakara, nimekuja kwa Waziri Mkuu nimelia, naomba magodoro, naomba sufuria, naomba mablanketi. Mheshimiwa Jenista Mhagama akaniambia nakusaidia, Waziri Mkuu kaniambia nikusaidie. Nimeenda bohari, nimepakia vifaa, magodoro, blanketi, sufuria, na kadhalika, nimeendanavyo mpaka Ifakara. Namwambia Mkurugenzi, tugawie watu waliopata mafuriko vifaa hivi. Wameiba katika stoo ya Halmashauri bila kuvunjwa kwa stoo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nimemwambia DC wetu Dunstan Kiwobya akahakikisha, akathibitisha. Watu wameandikiwa barua rudisheni kimya kimya. Vingine Naibu Waziri wa Uchukuzi pale, Rais wa RedCross, Mheshimiwa David Kihenzile, RedCross nao walinipa, wameiba. Vifaa vya maafa wameiba Ifakara.
Mheshimiwa Spika, ukisema, chuki, na Wakurugenzi wengine wanaingia kwenye siasa wanasema huyu tunamsubiria 2025 tutashughulika naye. Wameiba. Hakuna mtu yeyote ameenda Polisi, magodoro yale na mablanketi yale yana ubora wa namna yake, wanaambiwa warudishe yale ya dukani hayaeleweki. Fuatilieni mtaona, hakuna hatua iliyochukuliwa. Kwa hiyo, nasema kwa dhati kwamba, nina imani na Mheshimiwa Mchengerwa kwa sababu bila kukwambia uliitaja Halmashauri yangu kuzembea katika miradi, kukamilika katika miradi nikajua utachukua hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili nikwambie, Mheshimiwa Rais na Wizara mmetuletea shilingi milioni 528 za kujenga sekondari. Mmeleta tarehe 25 mwezi wa Sita, juzi ndiyo ujenzi umeanza. Hakuna hata wiki. Ukifuatilia unaambiwa wanabishana wampe mkandarasi huyu, wampe mkandarasi huyu, mradi haujakamilika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nafikiri …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Asenga, ngoja nielewe vizuri hapo. Hizo ni hoja zako ambazo unataka Serikali isikie ama ziko kwenye taarifa ya CAG?
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, zipo kwenye taarifa. Nataka kusema kuhusu ubadhirifu katika Halmashauri ambazo Taarifa ya Kamati ya LAAC imesema hapa kuhusu kuchelewa kwa miradi na ubadhirifu katika Halmashauri. Ndiyo ninachokisema.
SPIKA: Haya.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Kwa hiyo, hiyo ni mifano nimetoa kwenye jimbo langu Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, nimetoa mifano ili kuthibitisha ukweli wa Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, mifano ndiyo hiyo. Miradi inachelewa. Kamati imesema, nami natoa mfano Ifakara mradi hela zimepelekwa tarehe 25 mwezi wa Sita, mradi umekuja kuanza tarehe 15 mwezi wa Kumi ambapo ndiyo tarehe ya mwisho kwa mradi kukamilika. Kwa namna hii hatuwezi kufika, hatuwezi kuendelea.
Mheshimiwa Spika, nataka kusema suala la vikao na sisi kuwa Wajumbe wa Kamati za Fedha na Mabaraza ya Madiwani. Waziri Ummy akiwa Waziri wa TAMISEMI hapa, hii hoja imetolewa hapa, alitoa maelekezo kwamba ni vizuri Wakurugenzi wakaongea na Wabunge wao namna ya kuandaa vikao hivi. Jambo hilo halijafanyika, lakini leo tunaweza tukawajibishwa sisi kwamba ni Wajumbe wa Kamati za Fedha, Wajumbe wa Mabaraza ya Madiwani, lakini wewe unatupangia hapa ziara za Kamati, unatupangia Bunge lako, kwa nini vikao hivi visifanyike hata weekend kwa umuhimu wa sisi kushiriki ili tuseme?
Mheshimiwa Spika, vinginevyo nataka nikwambie, kama hatuingii kwenye Kamati za Fedha hizi, na watu wanapanga ratiba tofauti na Bunge, wana malengo yao. Siyo kwamba watu hawajui kwamba kuna siku moja inaweza ikapatikana Mbunge akapata nafasi akashiriki Kamati ya Fedha, akashiriki Baraza la Madiwani, wanapanga wanajua, Mbunge akiwa hapa hili hatakubali. Hilo la kwanza. (Makofi)
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Taarifa inatoka wapi? Mheshimiwa Mtaturu.
TAARIFA
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba, sehemu pekee ambayo tunashirikishwa Wabunge ni kipindi ambacho Halmashauri zinaitwa kwenye Kamati ya LAAC na PAC. Hapo ndiyo tunashirikishwa vizuri sana na tunaweza kushiriki ili kwenda kuchangia mawazi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Kicheko)
SPIKA: Mheshimiwa Abubakari Asenga, unapokea Taarifa hiyo?
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa mikono miwili. Pia, hata vile vikao kimoja kimoja unachovizia ama Katibu wako anaenda kwenye Baraza la Madiwani, maana Kamati ya Fedha hata Katibu wako haruhusiwi kwenda. Wanasema Mbunge mwenyewe uwepo. Sasa wakichengesha ile tarehe huwezi kushiriki, watu wameshapitisha mambo kule. Unakumbuka Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Comred Abdulrahman Kinana, katika semina alituambia, katika mambo muhimu ya Mbunge kufanya ni kutokupoteza hii Kamati ya Fedha.
Mheshimiwa Spika, haya la pili, makabrasha hayo yanakuja lini? Kabrasha unaletewa kama nyumba hivi, siku moja, labda saa sita, kesho kikao. Utapitia nini, utaacha nini?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunachoomba ni kwamba, wanapoandaa hivi vikao washirikiane nasi, tupate makabrasha kwa wakati, tujue tukienda kwenye Kamati ya Fedha tunapitia nini na tukienda kwenye Baraza tunapitia nini? Wako Madiwani wazuri sana. Sio Madiwani wote wanahusishwa ama wanatuhumiwa na kadhalika, lakini wako Madiwani ambao ni wazuri, wanasimamia, lakini baadaye wanaitwa wanaambiwa mradi wako utahamishwa, sijui nini, wanatishiwa na hatimaye unakuta, ile kauli ya Mheshimiwa Rais kwamba Madiwani chukueni hatua, fanyeni kazi yenu, inakuwa inakwama.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)