Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii ya kuweza kuchangia katika mjadala unaoendelea. Pengine nitajikita zaidi kwenye hoja ile ambayo inazungumzwa ya ongezeko la gharama kwenye lot 3 na lot 4 na nafasi ikitosha, basi nitaendelea na mengine.
Mheshimiwa Spika, moja ya hoja ambayo imezungumzwa ni kwamba, tulipotumia single source, taarifa yetu ya uchukuzi, tulipotumia single source gharama zilizongezeka by 1.3 million na 1.6 million per kilometer. Kabla sijaanza hata kujibu au kuingia kwenye kuchambua, logic pia nyepesi kabisa, unapojenga mradi mbali kutoka Dar es Salaam, unapoenda mbali zaidi gharama za usafiri na vitu vingine zinaongezeka. Hiyo ni kwa lugha nyepesi kabisa, lakini kwa kuwa imezungumziwa hoja ya kwamba ni kinyume na sheria za manunuzi, napenda pia kuzungumzia kwenye sheria yetu ya manunuzi Na. 7 ya mwaka 2011 na kanuni zake ambayo imetoa fursa na mazingira gani unayoweza kutumia single source.
Mheshimiwa Spika, ukienda Kifungu cha 161 (c), imeeleza kwa kirefu sana, lakini mojawapo ni kwamba, pengine kama mtu huyo yupo site au mmeona kuna faida kubwa ya kufanya hivyo. Tayari mkandarasi aliyekuwa anajenga lot 1 na 2 moja alikuwa site, pili alikuwa na mitambo, tatu Mradi wa lot 3 na 2 alikuwa ameshafika asilimia 97 na 95 respectively. Kwa hiyo, kwa wakati huo ilikuwa ni muhimu pengine kumtumia.
Mheshimiwa Spika, pengine wakati naendelea na hilo, kabla hatujachambua lot No. 3 na No. 4, hebu tuchambue gharama za lot No. 1 na No. 2 zimefanana ili tuweze kujenga hoja kumbe gharama za Na. 3 na Na. 4 kwa nini ziliongezeka? Ukienda kwenye Na. 1 na Na. 2 zilitofautiana kwa karibu dola 500,000 na sababu zilikuwa ni nyingi. Lot No. 1 inatoka Dar es Salaam mpaka Morogoro, ya pili inatoka Morogoro mpaka Makutupora. Na. 1 haikuwa na mahandaki, lot No. 2 ilikuwa na mahandaki karibu kilometa tatu. Hivyo usingetegemea zifanane. Pia, lot No. 2 vis-a-vis No. 1 ilikuwa inapita kwenye Mto Kondoa, kwa ambao ni wenyeji, pembezoni, jambo ambalo litakutaka katika eneo kubwa sana ujenge madaraja. Sasa katika hali hiyo, kama namba I na II hazikufanana, kwa nini tuseme Na. 3 na Na. 4 zifanane?
Mheshimiwa Spika, Na. 3 na Na. 4, tofauti za bei, it is very obvious, yako mambo kama 11, lakini kwa sababu muda leo ni mdogo naomba nitaje machache:-
Mheshimiwa Spika, nilisema na jana lot No. 3 na No. 4 inategemea kupita kwenye rift valley karibu kilometa 50 wakati lot No. 1 na 2 haina bonde la ufa. Gharama zitatofautiana. Lot No. 3 na No. 4 zina junction kubwa ambapo pale tunajenga karakana yetu, lakini pia tunakwenda kujenga Chuo cha Reli Tabora, center ya excellence ya Reli itakayohudumia karibu nchi zote za Afrika. Katika hali ya kawaida haiwezi kufanana na Lot No. 1 na No. 2 ambako kitu hicho hatuna.
Mheshimiwa Spika, ukiacha hilo, tunakwenda kujenga kituo kikubwa cha mizigo ambacho kinaunganisha karibu pande tatu. Kinaunganisha upande wa Dar es Salaam, reli inayokuja Dar es Salaam, inayokwenda Kigoma na inayokwenda Mwanza. Hii kwenye lot No. 1 na No. 2 hazipo. Ni vizuri Watanzania wakafahamu katika mazingira hayo haziwezi kuwa sawa.
Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi, eneo la Malongwe na Nyahua, wenyeji wa hapa wapo watanisaidia, karibu kilometa 40 inapita kwenye swamp. Huwezi kufananisha reli unayoijenga kutoka Dar es Salaam kupitia Pwani na ambayo inapita kwenye swamp. Kule kwenye swamp utajenga madaraja, utajenga makalavati, utainua matuta, kwa nini tunafikiri kwamba gharama zitakuwa sawa sawa? Ni vyema Watanzania wakalifahamu hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, kati ya Salanda na Manyoni kuna miinuko miwili…
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa David Kihenzile, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mpina.
Mheshimiwa Naibu Waziri, kaa kidogo.
TAARIFA
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, la kwanza, haya yote anayoyaongea Naibu Waziri, Mheshimiwa Mkaguzi wetu aliyakataa.
Mheshimiwa Spika, la pili, anachozungumzia kuhusu suala la mazingira ya mradi wa kutoka Morogoro kuja Makutupora…
SPIKA: Mheshimiwa Mpina, Taarifa ni moja.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, basi niiweke hiyo moja.
SPIKA: Haya, ahsante.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, hiyo moja …
SPIKA: Aah, umeshasema ya kwanza.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Aah, ahsante.
SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa David Kihenzile unaipokea Taarifa hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, namwomba tu aendelee kunisikiliza kama nilivyokuwa namsikiliza huko nyuma. Taarifa yake naikataa, kuweka record vizuri. (Makofi/Kicheko)
SPIKA: Sawa. Sasa ngoja niweke sawa.
Waheshimiwa Wabunge, hoja hii ni ya Kamati zetu tatu. Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwenye hoja hii ni wachangiaji kama mchangiaji mwingine. Kwa hiyo, inaruhusiwa kutoa Taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa David Kihenzile.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, kwa sababu muda ni mdogo, naomba niseme jambo moja muhimu sana kwa kuhitimisha kabla sijaendelea pengine.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, engineering estimate ambazo zinatumika kwenye mradi huu zilifanywa kati ya 2012 na 2016.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Ngoja. Mheshimiwa Halima, sasa hapo utakuwa unanipa mimi Taarifa kwa sababu, ndiye niliyetoka kuzungumza.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, alikuwa ameshaanza.
SPIKA: Ngoja achangie halafu utapewa, maana la sivyo, utakuwa unanipa mimi Taarifa.
Mheshimiwa Kihenzile.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nilitaka niwarejeshe Waheshimiwa Wabunge…
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: …kwenye Ripoti ya International Union of Railways, yaani Taarifa ya Reli Duniani. Ni vizuri tukaelewana hapa, tukasikilizana kwa faida yetu sisi kama Wabunge pamoja na Waheshimiwa wananchi.
MHE. HALIMA J. MDEE: Kumbe inauma!
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, katika ripoti hiyo, imeainisha na ninaomba tutembee kifua mbele Watanzania; imeainisha Barani Afrika zimejengwa kilometa 7,200 katika hizo, 2000 ni za Tanzania. Katika mchanganuo…
SPIKA: Haya, Mheshimiwa Kihenzile kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Halima Mdee.
TAARIFA
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kuhusiana na SGR na kwa mujibu wa mahojiano ambayo Kamati ya PAC imefanya kuhusiana na SGR, tumeambiwa wazi kwamba, mlilazimika kumpa mkandarasi Yapi Markezi, huyo Mturuki kwa sababu ya masharti ya Benki ya Standard Chartered. Masharti ya mikopo ndiyo yamewalazimisha mfanye maamuzi ambayo hayana maslahi. (Makofi)
SPIKA: Taarifa ni moja Mheshimiwa.
Mheshimiwa David Kihenzile, unaipokea Taarifa hiyo.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, Taarifa hiyo ninaikataa kwa sababu, haipo sehemu ya mjadala wangu. Tulimpa huyo baada ya kujiridhisha na vigezo vya Kitaifa. (Kicheko/Makofi)
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ninaendelea kwa sababu, nimekuwa Mwenyekiti, huwa ninafahamu taratibu na Kanuni.
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kuweza kuniruhusu. Nataka nitoe taarifa ya hali ya ujenzi wa reli Barani Afrika.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri ngoja.
Mheshimiwa Anatropia, unatakiwa usubiri kidogo kwa sababu, sasa utakuwa unampa Taarifa juu ya nini? Maana la sivyo, utakuwa unampa Taarifa Mbunge mwenzio. Kwa hiyo, unamwacha achangie kidogo ndiyo umpe Taarifa kwenye hiyo hoja yake.
Mheshimiwa David Kihenzile.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nilitaka kuzungumza kwamba, katika kilometa 7,200 karibu kilometa 2,000 zimejengwa Tanzania. Mataifa mengine wanakuja kujifunza tumefanyaje Watanzania?
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, katika gharama, Tanzania tumejenga kwa gharama ndogo ya shilingi 4.3 million per kilometer. Nchi nyingine ni kama ifuatavyo: Nigeria 6.1 million, Kenya milioni 7.3, Ethiopia milioni 5.9, Morocco 6.5 million, sisi ni 4.3. Tutembee kifua mbele tujisifu, Mheshimiwa Rais Samia anatuongoza vizuri. Huko tunakoenda ni kuzuri zaidi. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Kihenzile kwa sentensi yako naona hujamaliza, nataka kukuongeza dakika moja ili umalizie mchango.
Mheshimiwa Anatropia, Taarifa gani?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa Taarifa, hoja ya CAG ni ku-award kandarasi bila kufanya ushindanishi, single source. Single source ambayo angepaswa kuifanya ingekuwa na economic value. Mkaguzi amejiridhisha kwamba, ame-award bila kuwa na economic value. Hiyo ndiyo hoja yetu.
SPIKA: Haya, ahsante sana. Mheshimiwa Kihenzile, dakika mbili, malizia mchango wako na kama unaikubali hii Taarifa au hapana.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Taarifa ninaikataa kwa sababu nimeshasema mwanzoni kwamba sheria inaruhusu. Tunaongelea sheria ya nchi. Kama nchi saba zimejengwa kilometa 7,200 na zinakuja Tanzania kujifunza tumejengaje kwa 4.3 dola kwa kilometa moja, kwa nini Watanzania tusijivunie mambo mazuri?
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Kwa nini msiyafurahie?
Mheshimiwa Spika, tutembee kifua mbele kwa sababu tumejenga reli kwa gharama ambazo ni nafuu ukifananisha na wengine. Hilo ni moja. Pili, engineering estimate ambayo tumejengea reli zetu iko chini. Kwa mfano, wakati engineering estimate ya lot No. 3 ilikuwa ni 4.9, tumejenga kwa 4.05 wakati ile ya lot No. 4 ilikuwa ni 4.8 tumejenga kwa 4.3. Kwa hiyo, tuko vizuri, tutembee kifua mbele, tujidai, miradi iko kimikakati, wengi wangetamani kuwa kama sisi, tujivune, tuchape kazi. Tumuunge mkono Rais wetu. (Makofi)