Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, asiyeshukuru watu hata Mwenyezi Mungu hawezi kumshukuru. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa dhati ya moyo wangu nakushukuru sana Spika wangu. Moja, kwa kutuongoza vizuri lakini la pili, kwa kuaminiwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge yote Duniani. Nataka nikutie moyo, unatosha mpaka chenji inabaki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee nilishukuru sana Bunge lako Tukufu, kwa namna nyingine ninashukuru sana Kamati zako. Moja, kwa michango yao ambayo imewasilisha, hasa juu ya taarifa za CAG katika Wizara zetu.

Mheshimiwa Spika, taarifa hizi kwa Wizara yetu ya Maji, imetupa tathmini na kuongeza utendaji na uwajibikaji hasa katika kwenda kuchukua hatua. Hoja ya Kamati iliyoeleza dhidi ya Wizara yetu ya Maji, imezungumza suala la udhibiti wa upotevu wa maji yaliyotibiwa, sitaki nipingane na Kamati, naomba nikubaliane na Kamati, hili tumelipokea na tunaenda kulifanyia kazi zaidi na zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kiwango cha upotevu wa maji kinachokubalika Kitaifa na Kimataifa, Kitaifa ni asilimia 25 na Kimataifa ni asilimia 20. Mpaka Septemba kwa maana ya mwaka huu, Wizara ya Maji eneo la upotevu wa maji kiwango tulichofikia ni asilimia 36.5. Hiki bado ni kiwango kikubwa, maana yake kuna haja ya kuendelea kupambana na suala zima la upotevu wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kazi za utendaji ambazo nimefanya katika Wizara yetu ya Maji, moja, katika hili eneo la upotevu wa maji, kama Wizara ya Maji lazima tukubali kubadilika. Wakati mwingine unaweza ukakuta mwananchi kule chini ama mtaani, bomba linavuja lakini anatoa taarifa, hakuna response ya haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili tumeliona na sisi kama Wizara kupitia mamlaka zetu za maji, tumetengeneza task force ambapo inapotokea taarifa basi hili jambo lifanyike kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili, jamii ipo na viongozi wapo tu. Ukiwashirikisha utafanikiwa, usipowashirikisha utakwama. Tunajua huko chini kuna viongozi mbalimbali wa Serikali za Mitaa na viongozi wengine, kupitia mamlaka zetu za maji, maelekezo ambayo tumeyatoa ni kuendelea kushirikiana nao.

Mheshimiwa Spika, pia eneo lingine ni suala zima la taarifa zinazotolewa na Mamlaka zetu za Maji. Kwa mfano, unaweza ukafanya ziara katika Mamlaka ya Maji, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji anakwambia hapa upotevu ni asilimia 46. Unaweza ukamhoji, hebu tupite mtaani tuone asilimia hiyo 46 inayopotea. Kwa sababu unapozungumza asilimia 46 ya maji yapotee, maana yake sisi tunategemea kuwe na mabwawa makubwa kwa ajili ya kufugia samaki, lakini ukipita hauoni, maana yake nini, moja kuna uunganishaji wa kiholela. Kwa mfano, inawezekana kuna baadhi ya viwanda ama hoteli kubwa zimeunganishwa lakini hawasomeki kama wateja ambao wanatumia maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni eneo la wizi wa maji. Tumeendelea kutengeneza uboreshaji kwa maana ya operation mbalimbali tunazozifanya na niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, hili ni jukumu letu sote, tushirikiane kwa ajili ya kupambana na eneo hili.

Mheshimiwa Spika, kubwa ni kwamba, dunia imebadilika na sisi lazima twende huko. Lazima teknolojia zitumike kwa ajili ya kufanya mageuzi na mapinduzi hasa katika eneo la upotevu wa maji. Kwa hiyo, sasa hivi tunajiwekeza katika suala zima la TEHAMA ili tuwe na mitandao ambayo ita-detect kwa haraka sehemu ambako kunapotea maji na sisi kama Wizara ya Maji tunakwenda kudhibiti kwa haraka ili Watanzania waweze kupata maji safi na salama. Eneo lingine, …

MHE. PHILLIPO A. MULLUGO: Mheshimiwa Spika, taarifa, taarifa, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mbarawa, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mulugo.

TAARIFA

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, toka nimeanza kusikia…

SPIKA: Samahani kidogo. Mheshimiwa Aweso, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mulugo.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, toka asubuhi hapa nimeanza kusikia response za Mawaziri, ndiyo Waziri pekee ambaye nimeanza kumwelewa. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Aweso.

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza niendelee kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri kwa kazi kubwa ambazo wanazifanya, lakini kubwa nataka nieleze kwa eneo hili la upotevu wa maji kwamba hili ni jukumu letu sote, tuendelee kushikamana, kuhakikisha kwamba tunapigana katika hili eneo na kuhakikisha kwamba tunaenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni suala zima la miundombinu chakavu. Hapa naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais, miradi mingi ilikuwa na miundombinu chakavu, lakini kwa kipindi hiki tu kwa mwaka huu vijijini tunatekeleza miradi zaidi ya 1,546; mjini tunatekeleza miradi 2,244. Nini maana yake? Ujenzi wa miundombinu hii itakwenda kupunguza kwa kiwango kikubwa suala zima la upotevu wa maji.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo nataka kuzungumza na kwa dhati ya moyo wangu naomba nimpongeze CAG kwa kazi kubwa ambayo ameifanya. Moja ya maelekezo niliyopewa Waziri wa Maji, tarehe 22 Aprili, 2021 ambapo Mheshimiwa Rais alihutubia katika Bunge lako tukufu, Wizara ya Mji tulipewa maelekezo mahususi. Pamoja na kazi nyingine tulizopewa, lakini kuna kazi ile mahususi. Moja, ni juu ya kukamilisha mradi wa Same – Mwanga. Kwa hiyo, kipaumbele cha Wizara ya Maji pamoja na kazi nyingine, moja, ni Same – Mwanga; pili, ni Same – Mwanga, na tatu ni Same – Mwanga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, anayelala na mgonjwa ndiye anayejua mihemo ya mgonjwa. Waheshimiwa Wabunge, kaka yangu Mheshimiwa Tadayo na Mheshimiwa Mathayo, wamekuwa wasumbufu juu ya utekelezaji wa mradi huu. Kwa nini nasema nitumie nafasi hii kumshukuru CAG, ni kwa sababu huu ni mradi ambao ni wa muda mrefu, takribani sasa ni miaka 10. Mwaka 2021, CAG alifanya special audit kupitia taarifa yake hii, ndiyo imetuwezesha kutoka mradi asilimia 60, leo hii tuna asilimia 83.

Mheshimiwa Spika, nataka nikuhakikishie, sisi kama Wizara ya Maji, hatutakuwa kikwazo kuhakikisha mradi huu unakamilika ndani ya mwezi wa Sita na wananchi wa Same – Mwanga waweze kupata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, hoja ya Kamati ambayo imekuja mbele dhidi ya Wizara yetu ni kuhakikisha kwamba inaenda kufanya audit tena katika mradi ule. Nataka niwaambie Kamati pamoja na hoja hii, sisi hatutakuwa kikwazo, tutampa ushirikiano CAG, kwa sababu nia ni njema katika kuhakikisha kwamba…

SPIKA: Sekunde 30.

WAZIRI WA MAJI: …mradi huu unakamilika na Watanzania wa Same – Mwanga waweze kupata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, mwisho hii Tanzania ni nchi yetu na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni Rais wetu. Pamoja na mafanikio mengi ambayo tunayapata, lakini popote kwenye mafanikio hapakosi changamoto.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Muda wake umeisha.

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, tuendelee kushirikiana, maoni ambayo mmeyatoa, sisi kama viongozi tutaendelea kuyachukulia hatua ili kuhakikisha Watanzania wanapata majisafi, ahsante sana. (Makofi)