Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge kuhusu Wakala wa Kimataifa wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (International Renewable Energy Agency - IRENA) na Azimio la Bunge kuhusu mapendekezo ya kuridhia Mkataba wa Kuanzisha Taasisi ya Dawa ya Afrika wa Mwaka 2019 (Treaty for the Establishment of the African Medicine Agency - AMA)

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge kuhusu Wakala wa Kimataifa wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (International Renewable Energy Agency - IRENA) na Azimio la Bunge kuhusu mapendekezo ya kuridhia Mkataba wa Kuanzisha Taasisi ya Dawa ya Afrika wa Mwaka 2019 (Treaty for the Establishment of the African Medicine Agency - AMA)

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuweza kuchangia Azimio la Bunge la kuunga mkono Mkataba wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea na mchango wangu naomba nitumie angalau sekunde chache kuweza kumshukuru Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye mara baada ya kuteuliwa alifika Ngara na kuzindua miradi ya umeme kwenye vijiji vya Ntanga na Kaburanzwili na kwa kweli ziara ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kule Ngara imekuwa na matunda makubwa. Mbali na kuzindua umeme Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, aliwasiliana na Waziri wa Maji Aweso, ili aweze kufika Ngara kutatua changamoto ya maji kule Murusagamba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli naomba Waziri Aweso na Naibu Waziri Mkuu wachukue maua yao, kwa sababu kazi nzuri waliyoifanya kule Ngara imeleta matunda makubwa na wananchi wa Murusagamba sasa wanapata maji ambayo walikuwa hawana kwa muda mrefu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli huyu ndugu yangu Aweso ni mzee wa kutolaza zege alivyopokea simu ya Naibu Waziri Mkuu alifika Ngara ndani ya sku mbili, Mheshimiwa Aweso pokea maua yako. Sisi Wabunge tunajua namna unavyotuhudumia na namna unavyohudumia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nielekeze mchango wangu kwenye eneo hili la Mkataba wa IRENA. Nishati Jadidifu imeanza kutumika miaka 2000 iliyopita. Wenzetu huko Ulaya walianza kuzungusha magurudumu kwenye mito na yale magurudumu yakawa yanazalisha umeme wakagundua kwamba kumbe maji yanaweza yakazalisha umeme. Wakati huo sisi Afrika tulikuwa tunayatumia maji kwa ajili ya shughuli za kawaida, kuoga, kuogelea humo humo kwenye maji, kuyanywa, kufua nguo na kipindi kingine kuendesha mitubwi kwenye maji. Lakini wenzetu Ulaya miaka 2000 iliyopita walikuwa wameshaendelea na wameshaanza kuyatumia maji kwa ajili ya kuzalisha umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na kuanza kwao kutumia maji kuzalisha umeme wenzetu mwaka 1590 waligundua kwamba upepo unaweza ukatumika kuzalishia umeme na wakaanza kuzalisha umeme kwa kutumia upepo. Hawakuishia hapo mpaka mwaka 1800 wenzetu huko Ulaya waligundua kwamba jua na lenyewe linaweza likatumika kuzalisha umeme na wakaanza kupata umeme kutokana na nguvu ya jua. Mpaka wanakaa kwenye mkutano wa kugawana Bara la Afrika mwaka 1885 wenzetu walikuwa walishapiga hatua na walipokuja Afrika kuanza kugawana wenzetu walikuwa tayari wana hiyo teknolojia ya kuweza kuzalisha umeme kutokana na upepo maji pamoja na jua.

Mheshimiwa Naibu Spika, na sisi wakoloni walivyofika hapa tulibahatika kuridhi teknolojia hizo za kuzalisha umeme jadidifu mathalani kwa upande wa maji. Wote ni mashuhuda kwamba wakoloni ndio ambao wamefika Tanzania na kuanza kujenga mabwawa ya maji ambayo mengine tunayatumia mpaka sasa na kwa minadili hiyo Tanzania imepiga hatua kwenye eneo hilo la nishati jadidifu na mpaka sasa Tanzania inazalisha asilimia 31.5 ya umeme unaotokana na nishati jadidifu kwa maana ya renewable energy. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni sawa uzalishaji wa megawati 5704.60. Mataifa ambayo ni wanachama wa Umoja wa Mataifa, baada ya kuona kwamba matumizi ya nishati jadidifu ndio mwelekeo na njia sahihi ya kuepukana na mabadiliko ya tabia ya nchi, ambayo mabadiliko ya tabia ya nchi yanasababishwa na matumizi ya nishati zisizo jadidifu wenzetu wakaamua kutengeneza Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu kwa maana ya IRENA.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2009 wenzetu waliunda hiki chombo na Tanzania ikabahatika kusaini mkataba huu mwaka 2009 lakini kwa bahati mbaya watanzania tumeendelea kujivuta kwa miaka 14. Tumekuwa tukishiriki kwenye vikao vya IRENA kama watazamaji tu kama Observer na matokeo yake wenzetu wamekuwa wakikutana wana-share ujuzi, wanafundishaji mambo ya nishati jadidifu, wanapeana fursa mbalimbali za uwekezaji kwenye nishati jadidifu, sisi Tanzania tukiwa tunashuhudia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni sawasawa na kule vijijini unakwenda kwa majirani unakuta wanachinja ng’ombe wewe unatazama watu wanachinja ng’ombe wanagawana minofu, wewe unaondoka bila kuwa hata na unyoya. Ndicho ambacho Tanzania kwa miaka 14 imekuwa ikikifanya. Tunakwenda kwenye mikutano ya IRENA sisi tunabaki kuwa Observer, wenzetu wanagawana minofu tunaondoka tunarudi kama tulivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna kipindi watanzania tumejichelewesha ni sasa na kama kuna kipindi kama Taifa tunatakiwa haraka sana iwezekanavyo turidhie na tujiunge na IRENA ni sasa. Huu ndio mwelekeo sahihi wa kuepukana na athari za mabadiliko ya tabia nchi zinazotokana na matumizi ya nishati chafu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania ni mashuhuda kwamba maeneo ambayo mvua zilikuwa zinanyesha mwezi wa nane, mwezi wa tisa, sasa hivi zinachelewa kunyesha. Watanzania ni mashuhuda kwamba kuna kipindi unaweza ukapanda mbegu, baada ya kupanda mbegu mvua ikanyesha mara moja na baada ya hapo ikapotea, yote hayo yanatokana na mabadiliko ya tabia ya nchi yanayoletwa na kutumia nishati zisizo jadidifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania ni mashahidi kwamba kipindi hiki jua limeongezeka, kuna kipindi jua linawaka utadhania limetumwa au utafikiria linawaka kwenye kichwa chako peke yako. Unajiuliza hivi hili jua limekuwa namna gani? Lakini yote haya ni kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi yanayotokana na matumizi ya nishati zisizo jadidifu. Muda sasa umewadia watanzania kuweza kuridhia na kujiunga moja kwa moja tuwe wanachama tuanze kushiriki na tufanye maamuzi na tunufaike na fursa kedekede zilizopo kwenye IRENA.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ndaisaba kengele ya pili ilishalia ahsante kwa mchango mzuri.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)