Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie taarifa ya Kamati zetu zote tatu. Kitu ambacho nimejifunza kwa Serikali kwa wakati huu, kidogo sana, uandaaji wa hesabu ufanisi umeongezeka. Kwa kweli tunawapongeza Serikali kwa kuongeza ufanisi katika suala zima la uandaji wa hesabu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, kuna changamoto ambazo zimeonekana na bahati nzuri Kamati zetu zimetoa hapa. Nitachangia maeneo matatu. Eneo la kwanza, ni eneo la Mfuko wa Pembejeo; limesemwa na Kamati ya PAC lakini pia limesemwa na Kamati ya PIC. Haiwezekani kwa akili ya kawaida. Haiwezekani kabisa mnakopesha shilingi bilioni 26, halafu katika zile shilingi bilioni 26, shilingi bilioni 21 zinakuwa na indication ya kutokukusanyika. Hii haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi naona hapa ufanisi wakati wa utoaji wa mikopo hii haukuwa vizuri, kwa sababu kama tungefanya due diligence vizuri katika utoaji wa mikopo hii isingewezekana leo tunazungumza shilingi bilioni 21 ni mikopo chechefu yaani NPL, tunaweza kuzungumza mikopo mmetoa shilingi bilioni 26 katika zile shilingi bilioni 26, shilingi bilioni 21 hazikusanyiki hii haiwezekani! Nimeona Kamati ya PIC wametoa pendekezo la kufuta mikopo hii, mimi nitakuwa wa mwisho kukubaliana na hili, watu hawawezi kukopeshwa shilingi bilioni 21halafu leo tupitishe tufute eti tu-write off kwenye vitabu vya hesabu, fedha za Serikali ziwe zimekufa kiasi hicho, haiwezekani tufanye suala kama hilo. Watu waliokopeshwa wafuatiliwe, fedha zetu za Serikali zirudi tukopeshe watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano 2003 mpaka 2017 kuna bank zilikopeshwa zaidi ya shilingi milioni 800 zikafungwa na mikopo hii ikafia huko. Mfano, kulikuwa na Benki inaitwa Kagera Cooperative Bank, ilikopeshwa shilingi milioni 294, kulikuwa na Benki inaitwa Mbinga Community Bank ilikopeshwa shilingi milioni 286. Kulikuwa na Benki inaitwa Meru Community Bank ilikopeshwa shilingi milioni 150, kulikuwa na Benki inaitwa Njombe Community Bank ilikopeshwa shilingi bilioni 76. Hawa wote hawakurejesha fedha hizi! Pamoja na hayo nini kifanyike? Leo hatuwezi kupitisha eti tufute madeni haya Hapana! Maafisa Masuuli wahakikishe fedha hizi za walipa kodi, fedha hizi za nchi yetu ya Tanzania zinarejeshwa ili watu wengine waweze kukopeshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, benchmark ya mikopo inasema “mikopo chechefu walau iwe asilimia tano” yaani mikopo ambayo inaweza isikusanyike walau iwe asilimia tano. Kwa Mfuko wa Pembejeo ni asilimia 81, sasa asilimia 81 na sisi tuunge mkono eti tu-write off kwenye vitabu vyao vya hesabu, haiwezekani! Tunaomba sasa Wizara pamoja na Mfuko wetu wa Pembejeo, wahakikishe fedha hizi zinarejeshwa. Pia wafanye due diligence wakati wanatoa mikopo kwa Watanzania, inawezekana wanatoa mikopo halafu wanaenda kuzichukua zile fedha, halafu waliopewa wanashindwa kurejesha na tunafika kwenye hali ambayo leo tumefika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia lazima tuimarishe mfumo wa ndani wa ukusanyaji. Tulipowahoji hao watu walisema mfumo wa ndani wa ukusanyaji wa hizi fedha siyo mzuri, pia wanasema staff ni watu wachache. Sasa kama staff ni watu wachache inakuwaje tunakopesha? Kwa hiyo, tanakopesha halafu tunakuja kusakizia eti hatuna watu wa kufuatilia hiyo mikopo, kweli? Haiwezekani ni lazima tuhurumie fedha za walipa kodi, ni lazima tuhurumie fedha anazotupatia Mama yetu kipenzi Mama Samia Suluhu Hassan, analeta fedha nyingi lazima sisi tuwe mfano wa watu ambao tunakusanya fedha hizi ili kusudi ziweze kuzunguka kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni eneo la TANOIL, Shirika letu la Mafuta. Hapa sasa ndiyo kuna issue, kilichofanyika nini hapa? Tumepata hasara ya shilingi bilioni saba na milioni mia nane. Hasara hii imetokana na nini, hasara hii imetokana na watendaji kujichukulia uamuzi ambao haupo katika kanuni ambazo zinawaongoza. Kanuni zinataka uuze kwa bei hii, lakini wao wanajichukulia maamuzi yao binafsi kupunguza bei ya mafuta kwa lita ambayo haipo kwenye kanuni. Pale TANOIL wanakanuni kwamba, ile margin wanaweza kupunguza kwa asilimia 30, lakini imefika sehemu mpaka wanapunguza zaidi kwa shilingi 78 mpaka kupelekea kupata hasara ya shilingi bilioni 7.8.
Mheshimiwa Spika, tulipowauliza walipata wapi kibali, hawana kibali. Waziri wa Nishati, hakuwapa kibali, TPDC hakuwapa kibali. Wakajichukulia tu wenyewe, Bodi haikuruhusu lakini wao wakaamua tu kupunguza bei ya mafuta, haiwezekani, implication yake ni nini? Implication yake hii kwa wale ambao sasa wanawauzia mafuta, wanawauzia kwa kuwapunguzia kwa sababu wao wameamua halafu wanatuzunguka wanaenda kuchukua cha juu, business as usual. Lazima tuangalie hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri, Waziri wa Nishati yupo hapa, naomba akaanze na hili, ni lazima tukubaliane na pendekezo la Kamati, Mkaguzi Mkuu akafanye ukaguzi wa kiuchunguzi yaani Forensic Audit kuona wale wote waliosababisha hasara kwa Taifa ya shilingi bilioni 7.8 wachukuliwe hatua za kinidhamu, bila hivyo tutakuwa tunapeleka fedha, tunafanya biashara lakini hatupati faida, tunafanyeje sasa, tunakuwaje na kampuni ambayo leo imetuingiza hasara ya shilingi bilioni 7.8 halafu bado ipo. Haiwezekani lazima tuchukuwe maamuzi ya kuwasaidia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la tatu na la mwisho. Kampuni ya Mbolea, yaani hawa watu wanafanya biashara ya mbolea katika mwaka ambao tunauzungumza 2021/2022, Serikali ilipeleka ruzuku kwa kampuni ya mbolea ya shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kulipa mishahara pamoja na operating expenses. Katika biashara waliyofanya, hawakufanaya biashara yoyote wakapata sales sifuri. Yaani tumepeleka fedha watu wamekaa ofisini, wamelipwa mishahara shilingi bilioni 10.2, mishahara imelipwa kwa watu, matumizi ya mafuta tumewapa, sasa walikuwa wanafanya nini? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, yaani sales ni sifuri, wanafanya nini, si tuwapeleke wakafanye kazi zingine? Tuwapeleke hata huko Busega wakatusaidie kazi zingine? Kwa hiyo tuyaangalie maeneo haya. Hatuwezi tukawa tunapeleka fedha za Serikali, tunalipa watu mishahara halafu wanasoma magazeti, haiwezekani ni lazima mishahara ilete tija kwa Taifa. Sisi Wahasibu tunaita this is nugatory expenditure, you incur some expenditure that cannot generate any benefit! Ndiyo hawa wa mbolea, tumegharamika shilingi bilioni 10 hakuna walichotuingizia Serikalini. Yupo Mkurugenzi Mkuu, yupo sijui Afisa nini wanaitwa, yupo Afisa Masoko, Afisa sijui nani, sasa hawa wanafanya nini huko? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kampuni ambazo tunazianzisha ni lazima zilete tija, zilete matokeo kwa Watanzania. Kama kuna kampuni, kama kuna Mfuko hauleti matokeo chanya kwa Watanzania, kama hauleti matokeo chanya kwa Taifa ni heri ufutwe kuliko kuendelea kutuingizia hasara bila sababu za msingi. Mfuko wa Mbolea umetuingizia hasara bila sababu za msingi, futeni pelekeni Wizarani watagawa mbolea, kuliko kupeleka fedha shilingi bilioni 10.2 halafu mwisho wa siku hamna mapato ambayo tunapata kama nchi, hamna biashara wanayofanya, tumewapa mafuta, tumewalipa posho halafu kwenye hizi kuna posho nyingi, karibu shilingi milioni 800, tulipowauliza za nini sijui walikuwa wanafuatilia! Sasa unafuatilia nini wakati hakuna ulichouza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasikia kengele ya pili naomba kuunga mkono hoja mapendekezo yote ya Kamati yachukuliwe kama yalivyo, Forensic Audit kwa TANOIL lazima ifanyike. Ahsante sana. (Makofi)