Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu kama ilivyoelezwa kwenye Taarifa ya Kamati yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninapenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika kuhakikisha kuwa wananchi wake wa Tanzania tunaweza kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Taarifa ya PAC Mwenyekiti wangu ameongelea kuhusiana na DAWASA. DAWASA kumekuwa kuna Taasisi nyingi za Serikali ambazo zinadaiwa na DAWASA. Kama unavyojua, kuna sehemu nyingi kwenye majimbo mengi bado watu hawajaunganishiwa maji kutokana na uchache wa fedha. Hizi fedha shilingi bilioni 13.5 zipo katika Taasisi za Serikali, kwa hiyo, nilikuwa ninaomba nichukue nafasi hii kuziomba hizi taasisi ziweze kuwalipa DAWASA ili wananchi waweze kuunganishiwa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua, mwananchi wa kawaida asipolipa maji tu kwa miezi miwili anakatiwa maji lakini hizi taasisi zimekaa muda mrefu sana hazijawahi kulipa bili zao wala hazijawahi kukatiwa. Tunajua kwamba hizi ni taasisi muhimu na tunajua hawapati asilimia 100 ya bajeti lakini wajaribu kuangalia. Katika bajeti ambayo wanaipata waweze kuwalipa DAWASA ili na wao waweze kufanya shughuli zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilikuwa ninataka kuliongelea ni jambo la kumuomba Mheshimiwa Waziri wa Maji aweze kuangalia bili. Bili zetu ambazo tunazipata au wananchi wanazozipata hazina uwiano na matumizi ya maji. Unakuta mwananchi ambaye ana familia ya watu watatu anapata bili sawa na mwenye familia ya watu 10 na hizi bili zinakuja, kila bili zinapokuja unaweza ukuta kwa muda wa miezi mitatu iliyoongozana mtu anapata bili ambazo, mfano kama alipata shilingi 220,000 mwezi uliopita basi atapata shilingi 220,000 kwa muda wa miezi mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuangalie ni jinsi gani usomaji wa bili unaonekana kuna tatizo kidogo. Waangalie ni jinsi gani wanaweza kutofautisha familia ya watu wengi na familia ya watu wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na miundombinu mibovu ya maji. Maji ambayo yanatoka DAWASA ambayo tayari yameshatengenezwa asilimia 37 maji yote yanapotelea njiani na ni kwa sababu ya miundombinu mibovu. Kingine, mfano bomba limepasuka, unaweza ukawaita watu wa DAWASA waje kutengeneza lile bomba kwa sababu bomba linapopasuka maji yanatoka inawezekana hata kwa siku tano mfululizo lakini hawa watu hawaji na ndiyo maana hawa watu wa DAWASA wanaendelea kupata hasara kwa sababu miundombinu yao mingi ni mibovu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana wananchi wengi mfano Mkoa wa Dar es Salaam, Jimbo la Segerea kuna kata zangu, Kata ya Kinyerezi, Kata ya Bunyokwa, lakini pia na Kata ya Segerea, maji yanatoka kwa mgao kwa sababu maji mengi ambayo yanakuja ili yaende kwa wananchi yanaishia njiani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tulikuwa tunawaomba. Pamoja na kazi kubwa ambayo anaifanya Mheshimiwa Rais, pamoja na kazi kubwa anayoifanya Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri lakini kama huku chini kutakuwa hakuna watu ambao wanaweza kufanya kazi kuziba haya mapengo basi wananchi wataendelea kukosa maji muda wote kwa sababu maji ambayo yanakuja yanaishia njiani. Na haya maji yamekuwa yakileta hasara kubwa kwenye barabara, watu wametengeneza barabara, bomba likipasuka barabara yote inaharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyoy, tulikuwa tunaomba watu wa DAWASA, kwa kweli watu wa DAWASA wamekuwa ni wavivu sana hawa watu wa chini kuja kushughulikia haya mabomba machakavu. Na haya mabomba kama ninavyosema yanaleta usumbufu katika barabara lakini pia kwa wananchi. Unaweza ukakuta bomba limepasuka maji yanaingia kwa wananchi. Nilikuwa ninaomba haya mambo yaweze kufuatiliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nililokuwa ninataka kumuomba Mheshimiwa Waziri ni kuhusiana na jumuiya ya watumia maji. Tulikuwa na visima ambavyo vilikuwa vinaendeshwa na jumuiya ya watumia maji, DAWASA wakavichukua hivi visima, lakini sasa hivi hawavihudumii. Visima vyenyewe pampu zilishakufa siku nyingi. Kwa hiyo, nilikuwa ninaomba kama wenyewe wameshindwa kuviendeleza au kuvifanyia service ili viendelee kutoa maji, basi wawarudishie watumia maji kwa sababu kwa muda mrefu hivi visima vimekuwa vikiangaliwa na jumuiya ya watumia maji na vilikuwa vizuri tu. Tangu walivyovichukua DAWASA, visima vimekuwa havitoi maji, vingine vimekufa, vingine havifanyi kazi. Yaani tuna shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi kata zangu ambazo nimekuambia kata tatu au tano zina visima vya watumia maji lakini kwa sababu pampu zake zimekufa na DAWASA hawajaenda kutengeneza, inabidi wanunue maji na wakati vile visima vipo pale. Kwa hiyo, tunamuomba sana Mhehimiwa Waziri aangalie ni jinsi gani anaweza akavirudisha hivi visima kwa wananchi ili waweze kufanya kazi ya kuviendeleza na wananchi waweze kupata maji. Kwa sababu, kwa kawaida sisi tunapata maji ya mgao, Bonyokwa, Segerea, Kimanga pamoja na Kinyerezi wanapata maji ya mgao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama wanapata maji ya mgao, hivi visima ndiyo vingekuwa vinatusaidia lakini DAWASA visima wanavyo, lakini pia maji hayatoki. Waturudishie hivi visima vya watumia maji ili wananchi waweze kutumia hivi visima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nililokuwa ninataka kuongelea ni kuhusiana na vyanzo vya maji. Vyanzo vya maji vimekuwa ni tatizo kubwa kwa sababu kwenye vyanzo vya maji kumekuwa kuna shughuli za kibinadamu na ndiyo maana sisi tunapata maji ya mgao. Pamoja na kwamba, Mheshimiwa Rais anaanzisha miradi mingi na tunamshukuru pamoja na Mheshimiwa waziri, tunamshukuru hasa kwa miradi hii ya kimkakati ambayo imeanzishwa katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa jina la Dar es Salaam ya Kusini, tunashukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana sana viangaliwe hivi vyanzo vya maji. Kwa sababu, kwenye hivi vyanzo vya maji kama kutaendelea kuwa na shughuli za kibinadamu maji hayatakuwa yanatoka. Tutaendelea kupata mgao wa maji na tutaendelea kupata mgao wa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwapunguzie wananchi wetu ili waweze kupata mgao mmoja, wapate tu hata huo mgao wa maji, lakini visima hivi ambavyo tulikuwa tunaviendesha wenyewe tuweze kuvitumia. Visima hivyo wanavyo, pamoja na maji yao yanatoka kwa mgao. Tunaomba sana, tunajua Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri wanafanya kazi kubwa sana, Mkurugenzi wangu wa DAWASA Dar es Salaam, anafanya kazi kubwa sana lakini wasipoangalia huku chini maji yanakopotea itakuwa ni shida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetoka Mwaka 2015 mpaka Mwaka 2020, tulikuwa hatuna tatizo la maji mpaka Mwaka 2021, lakini sasa hivi linaanza kurudi tatizo la maji. Ukiangalia tatizo kubwa la maji linasababishwa na miundombinu. Mabomba yanapasuka. Hata hapa hapa Dodoma ukiangalia mabomba yanapasuka lakini ukiwapigia simu wahusika hawaji kwa wakati. Maji yanaendelea kupotea na wakija kwenye taarifa wanasema kwamba wana hasara, upotevu wa maji asilimia 37 na haya maji yanayopotea tayari yameshawekewa dawa kwa hiyo, wanaendelea kupata hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba hawa watu wanatakiwa wawalipe, DAWASA kutokana na hizi kazi zao pamoja na changamoto zao lakini pia waweze kurekebisha miundombinu yao ya maji. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Bonnah Kamoli.

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)