Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Bakar Hamad Bakar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili kuweza kuchangia ripoti hizi za Kamati tatu ambazo zimewasilishwa ndani ya Bunge letu leo asubuhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma; ambaye ametuwezesha kuwa wazima na afya njema na kuweza kukutana hapa katika kutekeleza majukumu yetu mbali mbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti hizi ambazo zinasomwa na hoja hizi ambazo tangu asubuhi leo zinaendelea kutolewa hapa zinaonyesha mapungufu mbalimbali yaliyomo ndani ya Serikali yetu. Si kwamba Serikali yetu haifanyi kazi, tunaamini kwamba Serikali yetu inafanya kazi nzuri na mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anafanya kazi nzuri sana. Tunaendelea kumpongeza na kumtakia afya njema ili anendelee kuwatumika Watanzania kwa umakini sana na kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia dosari hizi ili Serikali yetu iendelee kufanya kazi vizuri zaidi; iendelee ku-perform na iendelee kukusanya fedha za umma na kusimamia fedha za umma ili kuweza kutekeleza miradi kwa kasi na pia, kuwatumikia Watanzania kwa weledi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mapungufu mbalimbali ambayo yamebainishwa na ripoti za CAG; nami nitazungumzia machache. Kwanza nitaanza kwenye bohari ya dawa (MSD). Tarehe 12 Oktoba, ya mwaka 2021 MSD iliingia mkataba na kampuni ya Misri ya Alhandasya. Mkataba na kampuni hii ulikuwa ni kwa ajili ya kusambaza dawa na vifaa tiba kwa items 75.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkataba uliingiwa tarehe 12 mwezi wa kumi, lakini malipo kwa ajili ya kazi hiyo yalifanyika siku moja kabla ya mkataba kuingiwa. Kwa maana tarehe 11 Oktoba MSD walimlipa Alhandasya bilioni 3.4 advance payment kwa ajili ya kazi hiyo. Tunaona hapa kwanza tu kuna jambo huko mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Alhandasya Kampuni ya Misri, kampuni hii ilishindwa kutekeleza jukumu lake wakati tayari imeshalipwa 3.4 bilioni, na ikatoweka na fedha hizo mpaka leo fedha hizi hazijulikani ziko wapi na hawa Alhandasya hawajulikani hata walipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, MSD walipofuatilia, Alhandasya kule Misri kupitia mabalozi wetu kule walishindwa kuipata kampuni hii. Kwa maneno mengine ni kusema kwamba kampuni hii ilikuwa ni kampuni hewa; kwa maana haipo na fedha hizi za umma zaidi ya bilioni 3.4 zimelipwa na zimepigwa, hazipo tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchato huo na Alhandasya kushindwa kutekeleza majukumu yake MSD walimpata mkandarasi mwingine; kampuni nyingine ambayo inaitwa EIPICO ambapo yeye alikubali kuweza kusambaza vifaa tiba na kupewa mkataba mwingine wa kuweza kufanya kazi na MSD. Hapo ndipo na yeye alipopewa mkataba wa bilioni 10.8 kuweza kusambaza vifaa mbalimbali kwa makubaliano kwamba ataanza kusambaza vifaa ambavyo alipewa Alhandasya; ambazo zilikuwa ni item 75. Ndani ya item hizo 75 kwa mkataba huo, pia na yeye huyo EIPICO alisambaza item 12 kwa fedha ileile ya 3.4 bilioni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona haya ni mapungufu makubwa na madhaifu makubwa ndani ya Serikali yetu. Tunaiomba sana Serikali iweze kusimamia mikataba hii na iweze kufanya kazi hizi kwa ufanisi mkubwa. Hizi fedha ni nyingi sana kwa ajili ya kuweza kuwatumikia Watanzania. Tunazo shida na changamoto nyingi sana, sasa unapoona mambo haya yanatokea ndani ya Serikali, ni kuitia doa Serikali yetu na ni kumtia doa Mheshimiwa Rais wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu ana nia ya dhati ya kuwatumikia Watanzania lakini mambo haya ambayo yanatokea ni mambo ambayo yanendelea kumtia doa Mheshimiwa Rais wetu. Tunaiomba sana Serikali isimamie mikataba, isimamie fedha za umma kama vile Bunge linavyotaka, kama vile Bunge lilivyoidhinisha fedha hizi ndani ya bajeti ambayo inaendelea na tumeipitisha hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi ambazo zililipwa, zililipwa kinyume na taratibu. Kwanza, hakukuwa na dhamana kutoka kwa benki ambayo ililipwa lakini pia, hakukuwa na dhamana ya utendaji kazi wa hizo kampuni ambazo zimelipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo yanatokea hapa hapa Tanzania na hawa hawa Watanzania ambao wanalalamika ndio hao hao ambao wanamkwamisha Mheshimiwa Rais wetu. Kwa hiyo, tunaomba sana kuweza kufanyika marekebisho makubwa ndani na kusimamia fedha hizi za umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye jambo lingine. Kuna nakisi ya ukusanyaji wa kodi wa zaidi ya bilioni 887 ambazo hazikukusanywa kutokana na mambo mbalimbali na changamoto mbalimbali zilizoko pale TRA na kila siku tunakuwa tunapiga kelele kuhusiana na mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa fedha za umma zilizopo pale TRA…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba sana Serikali, fedha hizi ni nyingi sana. Kwa mfano kuna mafuta ambayo yaliingizwa nchini kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nchi nyingine lakini mafuta hayo hayakusafirishwa kwenda nchi nyingine na badala yake yalitumika ndani ya nchi na kuisababishia Serikali kukosa kodi stahiki kwenye mafuta hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo yanatokea hapa na sisi tupo na wasimamizi wa mambo haya Maafisa Masuuli wapo. Kwa hiyo tunaiomba sana Serikali iweze kurekebisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kuweza kusimamia zaidi ukusanyaji wa mapato ndani ya nchi yetu ili kuweza kufanikiwa zaidi kwenye utekelezaji wa majukumu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mchakato wa ajira BOT. Pia ni moja kati ya mambo ambayo CAG alibainisha, BOT walitangaza ajira kwa utaratibu wa kawaida na Watanzania walio wengi ambao wana sifa ya kuomba ajira zile, waliomba, lakini cha kushangaza ni kwamba baadaye katika mchakato baada ya Watanzania kuomba, katikati ya mchakato walibadilisha sifa huko ndani kinyume na utaratibu, kinyume na sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu na sheria inasema kwamba, ajira kwa maana ya Watanzania wanatakiwa kuajiriwa chini ya miaka 45, lakini BOT walikwenda kubadilisha hiki kipengele cha umri kutoka miaka 45 wakasema mwisho miaka 30. Tunajiuliza ni kwa nini kipengele hiki cha umri kisiingizwe kabla ya mchakato wa ajira kuanza, kwa nini hakikuwemo ndani ya zile sifa ambazo zilibainishwa pale awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye hili tunaona kulikuwa na mkakati makusudi wa kuwakosesha baadhi ya Watanzania fursa hizi za ajira na kuweza kuwanufaisha baadhi ya watu ambao inawezekana wanajulikana. Haya ni malalamiko na changamoto hizi zipo kwa muda mrefu kwamba BOT na taasisi zinazofanana na hizi kuwa watu wanaoajiriwa ni watu ni wa wakubwa ambao wanajulikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapungufu haya ni makubwa ambayo yanaisababishia Serikali yetu doa kubwa na tunaiomba sana Serikali iweze kujirekebisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naunga mkono mapendekezo yote ambayo yametolewa na Wenyeviti wetu hapa kwenye Kamati zetu tatu. Nashukuru sana. (Makofi)