Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Momba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Kwanza nianze kabisa kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa nchi hii kwa namna ambavyo anafanya kazi vizuri na kwa namna ambavyo anaendelea kupambana kuhakikisha hata sisi ambao tunatoka Majimbo ya Vijijini tunapata pesa. Tunapata pesa kwenye miradi ya maendeleo, tunapata pesa ambazo zinaendelea kuwasaidia wananchi kwenye shughuli mbalimbali, hata wananchi wa Momba nitumie fursa hii kusema tulivyokuwa jana si ndivyo tulivyo leo.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC ambayo kwenye kitabu hiki kimesheheni mambo mengi sana. Katika kipindi ambapo nilipata nafasi ya kusikiliza uwasilishaji wa CAG katika Taasisi mbalimbali ambazo zilikuja kututembelea kuna baadhi ya mambo nikajifunza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimegundua kwamba Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa sana kwa kujitoa kwa huruma, kwa weledi na kutamani kuisaidia jamii yake na kama Mama amedhamiria kuona ule uchungu wa Mama kwa ajili ya kuwasidia Watanzania, lakini kuna baadhi ya mambo nikaona kwamba mimi ni Mbunge natokana na Chama cha Mapinduzi, Serikali ya Chama cha Mapinduzi haina wapinzani, wapinzani ni baadhi ya watendaji wa Serikali ambao siyo waaminifu kwa dhamana ambayo wamepewa ndani ya Serikali, wao ndiyo wanawaumiza Watanzania wenzao kwa nafasi ambazo wamepewa lakini wao ndiyo wanamfanya Mheshimiwa Rais apate do ana Watanzania wakati mwingine wamlaumu ilihali walipaswa kulaumiwa wao.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia ripoti ya Kamati yangu ya PAC nikaangalia kwenye ripoti ya Kamati ya watu wa LAAC, asilimia 10 ya Halmashauri, Serikali ilidhamiria kuwasaidia wananchi wa kawaida vijana ambao hawawezi wakakopesheka, wakina mama na maskini watu wenye ulemavu ili waweze kusaidika, lakini angalia shilingi bilioni 5.6 hazikuweza kupelekwa kwenye huo Mfuko, shilingi bilioni 1.7 hazikuweza kupelekwa kwenye huo Mfuko kwenye baadhi ya Halmashauri. Jambo la kusikitisha shilingi bilioni 88.42 hazikuweza kurejeshwa kwenye huo Mfuko! Bilioni 88 hivi kwanini hizi pesa hata zisingepelekwa hata kwenye zahanati? Watanzania wanakufa huko vijijini, kuna vijiji havina zahanati, hakuna vituo vya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemsikia jana Waziri wa Afya akiwa anaongelea vyanzo vya kupata pesa kwa ajili ya kuwezesha Mfuko wa Bima kwa Wote, hizo pesa si zingeweza kuwasaidia Watanzania. Kwa hiyo, nikagundua Serikali ya Chama cha Mapinduzi haina mpinzani wapinzani ni baadhi ya watu waliopo ndani ya Serikali wameshindwa kutumia nafasi zao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wakati anapokea hotuba ya CAG kama ambavyo ameongea Mjumbe mwenzangu wa Kamati, aliongea kwa uchungu sana. Nae kama Kiongozi wa State na yeye kama Mheshimiwa Rais wetu yeye mwenyewe alionyesha kuchukizwa na baadhi ya mikataba ambayo inafanywa na watu wasiokuwa waaminifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye shirika moja hapa la TRC kwenye SGR, naomba nisome kidogo tu. Kwenye SGR kwenye kipengele kidogo ambacho kinasema dosari mbalimbali zilizobainishwa katika ununuzi wa vichwa na mabehewa ya treni. TRC ilikataa zabuni mara mbili kwa ajili ya manunuzi ya vichwa vya treni ya umeme na mabehewa ya abiria ambapo mzabuni aliye na bei ya dola za Kimarekani 263,460,514 alikataliwa kufanya manunuzi yasiyo na ushindani kwa dola za kimarekani ikapelekea kufika dola za Kimarekani 478,507,468 iliyosababisha ongezeko la gharama dola za Kimarekani 215,046 ambapo ni sawa na pesa za Kitanzania bilioni 550.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na-convert hapa kwenye vituo vya afya ni vituo vya afya 1,100 maana yake Jimbo langu lote la Momba lingekuwa limeshapata vituo vyote vya afya, Mkoa mzima wa Songwe na Mikoa mingine yote ambayo ipo hapa Tanzania ingekuwa imepata kwa sababu tu kuna mtu hakufuata utaratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najiuliza swali huu utaratibu je, ni Mheshimiwa Rais ndiyo anawatuma wafanye hivi? hawa ni watu wasio waaminifu ambao wamepewa dhamana, wameaminiwa na wanajificha kwenye kichaka cha dhamana ambazo wamepewa wanasahau kwamba wanaumiza Watanzania wenzao. Kwa nini wasifuate utaratibu, Kanuni na Miongozo kama ambavyo CAG mwenyewe anasema kwamba yapo baadhi ya mambo ambayo tunayapata ni watu kwa kutokufuata utaratibu, Kanuni na maagizo ndiyo yanatupelekea hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea hapo hapo kwa SGR, katika mkataba wa manunuzi wa locomotive na mabehewa ya abiria yaliyotumika, TRC ilitelekeza mkataba wa bila dhamana ya tendaji kazi hali iliyosababisha hasara ya Euro 5,520,400 ambayo ni sawa sawa na bilioni 13.7 za Kitanzania, nikaweka kwenye vituo vya afya ni vituo vya afya 28.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ilitokana na Mkandarasi kushindwa kutekeleza mkataba na TRC kushindwa kutoza gharama zilizotokana na uvunjifu wa masharti ya mkataba. Anaendelea anasema Mkandarasi alidai sababu hizo zilikiuka kanuni hivyo vitu kama hivyo. Mheshimiwa Rais siku anapokea hotuba yake ya CAG aliongelea mambo kama haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea tena…
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. CONDESTER MICHAEL SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Reli TRC, Mheshimiwa Waziri utapewa nafasi ya kujibu, shirika la Reli la Tanzania …..
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Condester naomba usubiri kuna taarifa usuburi, Mheshimiwa Naibu Waziri.
TAARIFA
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka tu kumkumbusha msemaji Dada yangu ambae anaongea vizuri sana, kwanza kwa hoja ya kwanza aliyoizungumza na cancellation kwamba unapobadilisha Mkandarasi wa kwanza na wa pili na bei ikitofautiana kuna factor nyingi. Moja kuna teknolojia, mbili kuna wakati ulipofikia awamu ya kwanza na awamu ya pili. Pia kwenye hoja yake hii ya pili anayoizungumza sasa hivi ambayo kimsingi alikuwa ameshaanza kuizungumza vizuri, tunazungumza hapa tulikuwa tumeshazunzumza haikufanyika ni kwa sababu hakukuwa na performance iliyo-guarantee ndiyo maana hakupewa, kwa hiyo hakukuwa na hasara iliyotokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Taifa likafahamu kwa sababu isije ikajengeka hoja kwamba ilifanyika manunuzi tukapata hasara bilioni 13, haikufanyika na sababu mojawapo kwa nini haikufanyika na haikufika mwishoni ni kwa sababu hapakuwa na hiyo performance guarantee, kwa hiyo nilitaka kuiweka vizuri hiyo statement. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Condester unaipokea hiyo taarifa?
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei. Mimi ni Mjumbe wa Kamati na Management ya TRC ilikuja ikahojiwa nilikuwepo kwenye Kamati na Hansard zipo, kwa hiyo najua ninachokifanya na hiki ninachokisoma mimi ni taarifa ya CAG siyo mimi, siyo taarifa yangu kutoka Momba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea. Shirika la Reli Tanzania - TRC lilimwomba Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Uturuki kufanya uchunguzi wa kina due diligence kuhusiana na kampuni ya Eurowagon juu ya ununuzi wa vichwa viwili na mabehewa 30 ya abiria ili waendelee kufanya hii shughuli. Jambo la kusikitisha ni TRC waliendelea na shughuli hii pamoja na Mheshimiwa Balozi kuwafanyia due diligence kuwaambia kwamba kampuni hii haifai lakini wakaendelea kufanya. Sasa swali tunajiuliza Mheshimiwa Balozi yupo nchini kule, anatumia pesa zetu za kodi na yupo kwa ajili ya hiyo kazi, anataka kulisadia Taifa lakini bado waliokuwa wamemwomba wakakataa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imagine tunaenda wapi, imagine yaani mtu kateuliwa na Mheshimiwa Rais, halafu hawataki, hawa ndiyo wapinzani wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Ninaendelea anasema kampuni hao Eurowagon haikuwasilisha dhamana ya utendaji kazi (performance security) licha ya kukumbushwa mara kadhaa na Shirika la Reli Tanzania (TRC), Shirika la Reli Tanzania liliendelea kutekeleza mkataba huo pasipokuwa na dhamana ya utendaji imagine na hivyo kupelekea hasara, anasema Shirika la Reli Tanzania TRC haikutoza Euro 2,260,000 hivyo kupelekea hasara ya Euro 5,520,400 hapa nime-convert ni bilioni 14 za kitanzania sawa na vituo 24 ya afya Watanzania wangekuwa wamevipata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema nini, wapo viongozi wa juu ambao nia yao ni njema wanataka kulisaidia Taifa, mpango wao ni mzuri ndiyo huo ambao Mheshimiwa Rais alionao mzuri. Lakini wapo wachache ambao wameaminiwa ni wataalam Mheshimiwa Rais amewaamini, ni wabobezi wa kufanya hayo mambo, badala watumie utaalam wao kulisaidia Taifa, kutusaidia Watanzania ambao labda sisi hatujui, wanatumia dhamana yao na utaalam wao vibaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana hawa watu pia wamesomeshwa kwa mkopo wa Serikali, hawa nikuambie ni wahujumu uchumi kama wahujumu wengine tu ambapo zipo sheria ambazo watu wakikosa makosa kidogo tu wanachukuliwa hatua, kwanini hawa hawachukuliwi hatua, kwa nini? CAG kwa nini kaandika hiki? Kwa nini alileta kwenye Kamati jambo kama hili? Walikuja kwenye Kamati kwanza taarifa yao yenyewe ambayo ilikuwa imeletwa na CAG walikuwa wanaikataa, na GAG mwenyewe alikuwa anawashangaa, as if hawakuwa na exit meeting walipokutana na CAG! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo inatosha kwamba watu wasiendelee kumwangusha Mheshimiwa Rais anapowaamini kwenye mikataba na wasifikirie Watanzania ni wajinga sana, wasiendelee kutuhujumu sana maana wanalitesa sana Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kwamba Taifa hili halina fedha, hicho kidogo tunachopata tungeweza kuki-utilize vizuri, tukakifanyia kazi vizuri, tungefika mbali, lakini watu wachache wasiokuwa na nia njema na mapenzi ya Taifa hili wanaendelea kulihujumu Taifa hili, kujinufaisha peke yao, kwa manufaa yao peke yao na kuendelea kututesa jambo ambalo siyo sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ana nia njema ya kutumikia Taifa hili. Yule mama ni mtu mzima, anapambana na hata unaiona sura yake ya kusaidia watu. Hata siku moja mwanamke hajawahi kuwa tapeli, mwanamke hajawahi kuacha kuwasaidia watu kwenye nyumba yake, lakini hawa aliowaamini ndio wanaomfanya Mheshimiwa Rais apate doa na Mheshimiwa Rais ana…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Condester, ahsante sana, kengele ya pili imelia.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu umeisha?
MWENYEKITI: Ndiyo, ni kengele ya pili.
MHE.CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia tu hoja moja, kuhusiana na suala la BoT, kama ambavyo wameongea wenzangu; aliongea Mjumbe mwenzangu wa Kamati. BoT ni taasisi kubwa, sisi wote ni Watanzania, na kila mtoto wa kawaida wa Tanzania anatamani afanye kazi kwenye sehemu nzuri. BoT wanapaswa kurejea ile procedure yote ambayo walipatikana wale watu, kwa sababu kila mtoto aliyepo Tanzania ana haki ya kupata kazi kwenye taasisi kubwa kama zile. BoT wamevunja sheria, wao kwa ajili ya kujinufaisha wenyewe, baadhi ya watu wameona watoto wao ndio wanaofaa sana kwenye hii nchi na ndiyo maana wakavunja utaratibu na wakaenda ndivyo sivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba Watanzania watendewe haki sawa na Watanzania wote. Sisi fahari yetu ni Utanzania wetu. Babu zetu waliokufa kwenye ardhi hii, sisi wote lazima tunufaike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)