Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Kamati hizi tatu. Kwanza, nianze kwa kuunga mkono kazi kubwa ambayo imefanywa na Kamati hizi tatu kwa niaba ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa na hoja ndogo yenye masilahi kwa Taifa letu. Nilikuwa nataka niseme jambo moja, kazi ya Bunge ni kuisimamia Serikali, lazima sisi kama wawakilishi wa wananchi tulinde haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nataka nitangulize hivyo kwa sababu gani; nchi hii imekuwa inaibiwa siyo kwa mitutu ya bunduki. Nataka Mheshimiwa Waziri wa Fedha (Mchumi aliyebobea), juzi alisema, namnukuu “Fedha hazipotei, kwa sababu Serikali inalinda mianya ya fedha kupotea”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie kwamba, hatuibiwi kwa kwenda kuvunja nyumba, tunaibiwa kwa kutumia akili, tunaibiwa kwa kuingia mikataba mibovu. Lile suala la kuingia mikataba ndilo limeingiza Taifa letu hasara na tusipokuwa makini tutaendelea kuwa na hasara. Hapa ndio nashindwa kuelewa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu inafanya kazi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ndiyo maana Mheshimiwa Rais siku moja alisema, sijui hicho cheo cha Mheshimiwa Kabudi (Mzee wa mikataba) kipo? Kwa sababu, tumekuwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ambayo inakwenda inakula huku na huku. Kwa sababu gani, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu inatakiwa isaidie Serikali katika kuingia mikataba mbalimbali. Sijawahi kuona Serikali inakwenda kushinda kesi, Serikali inakwenda kutetea mkataba ulioingia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakutolea mfano mwaka 2013/2014 ilikuja hoja hapa ya Tegeta Escrow mnaikumbuka. Mwanasheria Mkuu aliyekuwepo wakati ule alisema zile fedha siyo za Serikali. Wakasema fedha ni za watu binafsi. Kwa kuwa siku hazigandi, hilo jambo limerudi tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme jambo moja ndiyo useme Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na yenyewe inatakiwa iendewe na CAG huko. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliingia mkataba na APTL, tukatengeneza akaunti ya pamoja, tukasema fedha zetu tuziweke mahala fulani, Serikali ikatimiza wajibu wake ikaweka fedha. Wakatokea wajanja wakaenda kuzipakua. Tukaanza kuuliza humu za umma au siyo za umma si za umma? Mwanasheria Mkuu akasema siyo za umma, leo anaumbuka huku zile fedha zilikuwa za Serikali. (Makofi na Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna mashtaka yamekwishakuja tunadaiwa zaidi ya dola za kimarekani bilioni 148. Tunatakiwa tulipe dola za kimarekani milioni 148 sawa sawa na bilioni mia tatu na ushee. Sasa, huyu Mwanasheria Mkuu hakuliona hili toka zamani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo hapo nakuja kusema kwamba, kwa nini Ofisi ya Mwanasheria Mkuu haitusaidii? Cha ajabu, yule APTL wakati wanakwenda kutoa hizi fedha wakisema za kwao akasema, likitokea lolote linalohusu Serikali, Serikali haitohusika nitahusika mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo inakwenda kudaiwa Serikali na Serikali imekwishajiandaa kuanza kulipa. Mimi ninawambia msilipe, kalipeni hela zenu huko. Mwaka 2018 Mwanasheria Mkuu akapeleka kesi mahakamni kumshtaki huyu IPTL kwa nini ametutelekeza, sijui imekuwaje, mbona tulikuwa wote pamoja, ameingilia wapi? (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama Kuu ikatoa uamuzi wa kwamba, IPTL iilipe Serikali hizo fedha ili likitokea la kutokea iweze kuwalipa wale wanaodai ambao waliikopesha IPTL. Lakini mpaka kufikia tarehe 1 Machi, 2021 ilitakiwa zile fedha ziwe zimwkeishalipwa lakini hadi kufikia Desemba 2022 fedha hizo bado hazijalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Serikali inaanza kuandaa eti kwa sababu tutakamatiwa ndege, image ya nchi itaharibika. Mimi niwambie hivi, kwa kulinda wezi, wabadhilifu, mlikuja hapa na hoja ya kusema fedha siyo za Serikali kumbe ni za Serikali. Mlikuwa mnajizunguka wenyewe leo mnaumbuka. Mimi niwambie na Kamati imependekeza fedha hiyo isilipwe, watakwenda kuchukua fedha za walipa kodi wa Tanzania kwenda kuhalalisha hela walizokuwa wamezitoa wakati ule kwenda kugawana kwenye viroba na leo hii hatuwajui waliogawana wako wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ulikubaliana na IPTL fedha ilipwe, nenda ukasimamie hilo jambo. Bunge hili hatutapitisha fedha kwenda kulipwa kwa sababu ya uzembe wa watu. Kwa hiyo, nilikuwa nataka niikumbushe Serikali kwamba, hatuibiwi kwa mitutu ya bunduki kwa sababu hata hao wenyewe wenye mitutu ya bunduki na wenyewe wameshaibiana huko tozo unatozwa polisi wenyewe wameibiana. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii nchi kila mtu ni mpiga deal. Mlinzi wa amani mpiga deal, ukienda TAKUKURU unakwenda kupumzishwa na hakuna kitu kinachoendelea. Kwa hiyo, haya mambo yaweze kusaidika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni la kusikitisha, Serikali imekwenda kuanzisha vitaasisi vya kufanya biashara halafu hamuwezi kufanya biashara. Leo TANOIL imeleta hasara duniani sijawahi kuona, Serikali ilipeleka bilioni 128 kuusaidia mfuko wa TANOIL ili ifanye biashara ya mafuta. Leo hata bilioni 20 haifiki, hela zote wamekula, tunaanza hapa kuzungushana, tumewafukuza. Umewafukuza wamekwedna wapi? Au ninyi wenyewe mlijitangulizia pasi ili mwende mkafunge? (Makofi/Kicheko)

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Venant, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mwigulu.

TAARIFA

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mchangiaji. Pamoja na mchango mzuri anaochangia naomba nimpe taarifa kwamba, hizi taarifa tunazojadiliana ni moja ya sehemu ya kazi nzuri zinazofanywa na taasisi zetu ikiwepo TAKUKURU pamoja na CAG. Inawezekana katika utendaji wa kazi na taasisi akawepo mtu mmoja mmoja. Hata hivyo, ningeomba hiki chombo chako ambacho ndiyo mtungaji wa Sheria, kiepuke ku-generalize taasisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inaheshimika kwa taasisi. Inaweza ikawa na mtu mmoja mmoja akafanya hivyo lakini taasisi zetu ni moja ya nchi ambayo inaheshimika sana. Pia, TAKUKURU ni moja ya taasisi yetu ambayo inaheshimika kama taasisi. Kwa hiyo, nilitaka nikubaliane na michango yake na hisia aliyonayo lakini nimuombe asi-generalize taasisi kama taasisi, bali twende kwenye maeneo moja moja ambalo tunaona mapungufu. Pia, Serikali iko kwa ajili hiyo na huo ndio utawala wa Sheria unavyotaka. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Venant, unapokea hiyo taarifa?

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza amekula dakika zangu tatu, zilindwe. CAG alisema, Jeshi la polisi fedha zilizopotea za tuzo na tozo na hajamtaja mtu mmoja mmoja. Sasa, kama kuna mtu mmoja mmoja mtuletee tuwashughulikie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, CAG yeye alifanya Jeshi la polisi, sasa kumbe mnawafahamu mtu mmoja mmoja. Mtusaidie hilo jambo...

MHE. CHISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, Taarifa.

TAARIFA

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji makini anayezungumza jambo hili kwa uchungu unaostahili. Jambo la msingi na namna bora ya Bunge hili kujiheshimisha kwa wale waliotuleta hapa, kuhitimisha hoja hizi kubwa tatu, ni kwa Bunge hili kuweka Azimio madhubuti na kuhakikisha kwamba Wizara zote ambazo ufisadi umetokea wa matrilioni ya fedha hizi, Mawaziri wanaohusika, narudia kusema Mawaziri walioshindwa kusimamia taasisi zilizoko chini ya Wizara zao wawajibike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hawatowajibika hakuna namna nyingine. Kama hawatowajibika wao, twende na shingo ya yule ambaye tuna mamlaka naye ili boti letu lililotobolewa leo na mafisadi wasiendelee kwenda kushangilia kula hela ya umma huko halafu tunalijadili jina la jambo hili kwa wepesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima Bunge hili lilinde heshima ya Bunge kwa kuwachukulia Mafisadi hatua na kuwachukulia wale walioshindwa kuwawajibisha. Nataka kumuunga mkono kwa kusema hivyo, acheni masihara. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Venant, unapokea taarifa ya Mheshimiwa Olesendeka?

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea. Kwa kuongezea kuweka msisitizo wa mtoa taarifa, nilikuwa nagusia Taasisi ya TANOIL ambayo imetupotezea zaidi ya bilioni mia moja na kidogo. Yaani hatua, Serikali inasema tumewaweka pembeni. Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na pia ni Waziri wa Nishati, ninakuheshimu sana. Nikuombe, nenda pale TANOIL na Kalandinga, ukamuache mhudumu tu. Wengine wote kamata mwende mkawaweke huko. Aliyehusika akae huko, hajahusika mumtoe kwa utaratibu uliopo. Lakini pale TANOIL kuna uozo mkubwa na sisi huku tumetoa mapendekezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kupitia Bunge lako, tunapigwa ndani na nje, tusipodhibiti sisi wenyewe, hakuna baba ambaye atakuja kutuokoana haya yatakuwa watendaji wa Serikali...

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jenista.



TAARIFA

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza kabisa naomba niendelee kumpongeza mchangiaji kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuendelea kutoa ushauri na kuungana na ripoti ya CAG kupitia kwenye Kamati husika. Lakini naomba tu nikumbushe maneno mengine ambayo mchangiaji amekuwa akiyatumia mara kadhaa leo kwamba, tunapigwa, tunapigwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunapigwa, naomba tu nikumbushe Bunge lako Tukufu kwamba, yako makosa na baadhi ya watumishi kweli wanatukosea na wanafanya isivyo haki. Lakini bado Serikali yetu ya Awamu ya Sita imeendelea kufanya kazi nzuri katika miradi mingi na maeneo mengi. Kwa hiyo, ninachotaka kutoa taarifa, makosa haya yatachukuliwa na kufanyiwa kazi kwa uzito wake kwa idadi ya makosa yaliyopo. Lakini hayatochukua nafasi ya kazi nzuri sana ambayo imefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwahudumia wananchi.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Venant, malizia.

MHE, VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inafanya kazi vizuri, hatujakataa. Hao mnaowasema mmoja mmoja kwa nini mnawachelewesha huku mtaani wanaendelea kutusumbua? Wachukulieni hatua mapema. Hapa mnapokuja, hapa CAG mlikwishashindana huko ndiyo maana mmekuja humu Bungeni. Tunachokisema, tumekwishawaita kwenye Kamati wamejitetea na hakuna utetezi zaidi ya kuchukua hatua… (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wake umekwisha nilimpa dakika moja tu amalizie.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi.

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, wamenilia dakika zangu lakini yote kwa yote, Bunge hili tusilete ushabiki. Ni lazima tuisaidie nchi, lazima tumsaidie Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais amesema tumsaidie. Inaweza kuwa ninyi Mawaziri hamjui huko ni nini kinachoendelea. Sisi tukijua mkayafanyie kazi, msianze kukinga kinga hapa mtakuwa hamtusaidii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)