Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. George Natany Malima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia hoja iliyopo mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha nia ya dhati kabisa ya kufanya uwekezaji katika nchi yetu. Shilingi trilioni 73 ambayo yote imeenda kwa ajili ya uwekezaji si fedha kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji Mitaji ya Umma, nimepata nafasi ya kupitia mashirika mbalimbali. Zipo changamoto nyingi. Changamoto moja wapo ambayo ningependa kuizungumzia hapa ni mzigo mkubwa wa madeni ambayo taasisi hizi zinayo. Taasisi nyingi zinaendeshwa kwa hasara kwa sababu zina madeni mengi sana, lakini pia hata unapokutana nazo huwezi kuona mikakati ya dhati kabisa ya kulipa hayo madeni. Kwa hiyo taasisi kama hizi zinazoendeshwa kwa madeni huwezi kutegemea utapata tija ile iliyokusudiwa wakati wazo la uwekezaji lilipoanzishwa. Kwa hiyo ndiyo maana unaona Mashirika haya yanashindwa hata kutoa gawio katika Mfuko Mkuu wa Serikali kwa sababu wanadaiwa lakini pia hawana mikakati ya kulipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetoa mifano tu kidogo ya Mashirika kama mawili au matatu, kwa mfano Taasisi ya NSSSF mwaka 2019/2020 ilikuwa inadaiwa shilingi bilioni 239.58 lakini mwaka 2020/2021 ikawa inadaiwa shilingi bilioni 256.43 na 2021/2022 inadaiwa shilingi bilioni 306.29. Sasa taasisi kama hii inahusika na kulipa mafao ya watumishi wale wanaostaafu. Nataka kujiuliza taasisi yenye madeni kama haya inaweza kuendelea kuwa na uwezo wa kulipa michango ya wastaafu, au ndiyo kama zile tunazoona mtaani kila siku wastaafu wanazunguka mtaani Kwenda na kurudi kwa sababu mashirika haya hayafanyi vizuri? Mimi ningeshauri sana Serikali lazima tujikite kutafuta sababu kubwa ambayo inasababisha mashirika haya yasifanye vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni hili la uendeshaji mbovu. Wale wanoendesha, kama ambavyo wamesema wengine, kuna wafanyakazi ambao siyo waaminifu, hawatumii vizuri michango hii ya watumishi; kwa hiyo lazima tuwamulike na tuwachukulie hatua. Nimeona baadhi ya Mawaziri wameonyesha commitment kwamba Serikali itaendelea kuchunguza wale wote ambao hawafanyi vizuri kwenye mashirika ya umma wachukuliwe hatua. Mimi ningependa sana kusikia siku moja watendaji wabovu wanachukuliwa hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye Shirika la Michezo ya Kubahatisha nalo kwa miaka mitatu mfululizo limeendelea kupata madeni huku madeni yakiendelea kukua. Kwa mfano, mwaka 2019/2020 lilikuwa na deni ya shilingi milioni 742.5, lakini mwaka 2020/2021 likawa linadaiwa shilingi bilioni 2.8. Hata wao tulipokutana nao hawaonyeshi nia ya dhati kwamba wana mikakati gani ya kuhakikisha kwamba deni hili linalipika na linapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi nyingine ni Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), nalo pia ni Shrika ambalo lina mzigo mkubwa sana wa madeni. Mwaka 2019/2020 lilikuwa linadaiwa shilingi bilioni 1.36, lakini hadi 2021/2022 likawa linadaiwa shilingi bilioni 5.9. Mashirika haya yote usitegemee kwamba yanaweza kutoa mchango katika Mfuko Mkuu wa Serikali, lengo ambalo kwa kweli ndilo kubwa. Unapowekeza hata kwenye biashara yako binafsi unategemea upate faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unawekeza halafu hupati faida kila mwaka, na kila unapokwenda kuangalia hesabu zake hazionyeshi matumaini maana yake huwezi kupata faida; na ndiyo maana tunashauri kwamba Serikali ijaribu kupita upya mashirika haya; hebu tuone yale ambayo yako kabisa yana dhamira ya kufanya biashara na kuleta tija iliyokusudiwa yaendelee na yapewe uwezo; lakini yale ambayo hayafanyi vizuri ama menejimenti zibadilishwe na bodi ama mashirika hayo yaunganishwe na mashirika mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo ningependa kulizungumzia kidogo hapa ni utegemezi wa ruzuku. Yapo mashirika mengi yanategemea sana ruzuku; na ukishangaa shirika ambalo linapewa ruzuku ya Serikali bado linaendeshwa kwa hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningeomba hapa kwamba Serikali iangalie vizuri, kwamba, kama shirika halifanyi vizuri hakuna sababu ya kupeleka fedha pale, ni afadhali tuwapeleke wale wanaofanya vizuri. Mashirika mengi yanategemea ruzuku, ni pamoja na NEMC pia. Mwaka 2022 ilipata shilingi bilioni nne zilikopwa kutoka Serikalini. Sasa ukiangalia bado halifanyi vizuri, bado lina mzigo wa madeni na bado Serikali inapeleka fedha nyingi mahali pale; nadhani tuangalie vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia shirika lingine ni Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA), pia linapata ruzuku nyingi sana. Na hata ile ziada ambayo wana-register kila mwaka inatokana na fedha kutoka ruzuku ya Serikali sisi tungetegemea tuone ziada inayozalishwa na wao wenyewe na kwa ruzuku hii kwa mfano VETA mwaka 2020/2021 walipata ruzuku ya shilingi bilioni 62 kutoka Serikalini. Na ndiyo maana ukiangalia kwenye hesabu zao kuna ziada kwa miaka mitatu mfululizo, ni kwa sababu fedha nyingi inatoka Serikalini lakini wao wenyewe hatujaona kama kuna kitu wanajaribu kufanya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuzungumza ni uzingatiaji wa vigezo vya Msajili wa Hazina; vigezo vinavyohusu utendaji wa kifedha na utendaji wa ujumla. Msajili wa Hazina amepewa mamlaka ya kuweka vigezo (KPIs) kwa ajili ya kuendesha mashirika, lakini yako mashirika ambayo hayafuati hata kimoja, je mfano tu Bodi ya Chai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Chai ni kati ya mashirika ambayo hayafuati vigezo vya Msajili wa Hazina. Kwa mfano ukiangalia kwenye gharama za watumishi kwa matumizi ukomo wa TR ni asilimia 40 lakini wao wanaendesha kwa asilimia 64. Kwa utegemezi wa ruzuku TR anazungumzia hoja ya kupunguza kutegemea ruzuku lakini wao wanategemea ruzuku kwa asilimia 86. Uwiano wa matumizi kwa mapato, ukomo wa TR ni asilimia 50 lakini Bodi ya Chai wao wanaendesha kwa asilimia 116 lakini unaona kwamba hawaendi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na yapo mashirika mengine, kwa mfano Mfuko wa Pembejeo wa Taifa na NHIF; yote haya hayafuati vigezo vile ambavyo vimewekwa na Msajili wa Hazina lakini unaangalia unaona kwamba Msajili wa Hazina hana meno, hana namna ya kuwachukulia hatua watu kama hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nashauri muswada uletwe turekebishe sheria. Msajili wa Hazina awe na Sheria, awe na nguvu ya kuyawajibisha Mashirika kama haya ambayo hayafuati taratibu hizi. Taratibu hizi zimewekwa maalum kwa ajili ya kusaidia mashirika yetu yaweze kufanya vizuri. Sasa kama hakuna kitu cha kuwasukuma wafanye hivyo ndiyo maana tunaona mashirika mengi sana hapa hayafuati na yanafanya yanavyotaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni tatizo la kuchelewesha kuwalipa wakandarasi na wale watoa huduma. Tatizo hili limeleta hasara kubwa sana serikalini. Unapochelewesha kumlipa mkandarasi au mtoa huduma maana yake kunakuwa na penalty, kunakuwa riba, baadaye unapokuja kulipa lazima ulipe na riba. Tumeona kwenye ripoti kwamba kwenye mashirika 12 ambayo yalichelewesha kuwalipa wakandarasi na watoa huduma, walilazilika kulipa zaidi shilingi bilioni 63. Hizi fedha ni nyingi sana na zingeweza kufanya kazi nyingine ya kuwaletea wananchi Watanzania maendeleo lakini zinalipwa kwa ajili ya riba na wale waliofanya hivyo, waliochelewesha kuwalipa wakandarasi au watoa huduma wanaendelea kuwa ofisini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, jambo hili ni jambo ambalo linatia aibu, kwa nini tucheleweshe kuwalipa halafu tuingie kwenye penalty kubwa kama hii, shilingi bilioni 63.7. Mimi nadhani watu kama hawa Serikali lazima iwachukulie hatua, kwa sababu wanatuingiza kwenye hasara kubwa na fedha hizi ni za walipakodi na wakati mwingine walipakodi wa chini kabisa ndio wanaolipa hizi fedha. Sasa zinatumika vibaya na bado tunaendelea kusema waendelee kuwa ofisini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hatua lazima zichukuliwe, tumpe meno Msajili wa Hazina, anaposimamia mashirika haya awe na nguvu ya kumwajibisha Mtendaji au kuiwajibisha Bodi ya hiyo taasisi. Hii itatusaidia kupunguza gharama kama hizi ambazo zimekuwa zikitokea, ni kama hakuna mtu wa kuangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuchelewa kukamilika kwa miradi ya maendeleo na hii imetuletea shida pia. Unapochelewa kukamilisha mradi gharama zinapanda kwa sababu bei za vifaa zinabadilika, lakini pia kuna zile gharama za kimkataba. Mkandarasi mlikubaliana ujenzi kwa miaka mitatu, inafika miaka saba, lazima kuwe na penalty, ndio haya mambo ambayo tunayasema. Kwa nini tunachelewesha miradi ya maendeleo? Kwa nini haikamiliki kwa wakati?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna watu wanahusika, Serikali ichukue hatua kuliko kusubiri mpaka tulipe gharama hizi, tunasubiri mpaka vifaa vinapanda bei. Kwa hiyo, gharama iliyokuwa imekusudiwa kulipwa kwa huo mradi mmoja, unapokuja kukamilika tunalipa mara tatu zaidi, pamoja na penalty, pamoja na gharama za kimkataba. Kwa hiyo nafikiri na hili jambo ni muhimu sana, ningependa pia nilizungumzie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nikubaliane na wenzangu wote kuunga mkono hoja. Tuendelee kum-support Mheshimiwa Rais kwa kumsaidia katika maeneo kama haya ambayo yameonekana yanaleta shida katika uwekezaji. Fedha hizi amezitoa kwa wingi, shilingi trillioni 73, sisi kumuonesha kwamba tunamuunga mkono lazima tusimamie haya mashirika kwa uhakika na kwa usahihi mkubwa sana. Bila hivyo hizo fedha zitakuwa zinatolewa, tija haipatikani na tunaendelea kusema tuna uwekezaji hapa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nakushukuru. (Makofi)