Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Aloyce Andrew Kwezi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, umenichekesha, ahsante na naomba nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kutupa wasaa huu wa jioni, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoendelea nayo ya kujenga Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana Mawaziri hawa wawili. Mwigulu Nchemba pamoja na Profesa pale. Niwapongeze kwa kazi nzuri walizonazo ambazo sisi Watanzania tunaziona kwa macho na hatuna haja ya kusimuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu kuhusiana na Mpango wa 2024/2025, napenda niishauri Serikali yangu mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu wengi sana Waheshimiwa Wabunge wameongelea sana mambo ya Barabara, lakini walipokuwa wanaendelea nilikuwa najiuliza mambo ya msingi kwamba hivi kweli tunapanga Mpango wa Maendeleo wa 2024/2025, lakini yapo mambo ya msingi, sisi kama Wabunge tumekuja Bungeni tunashauri mambo mengi sana kuhusiana na barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote tunawaambia jamani tunahitaji barabara hizi kwa kuinua mishipa ya kiuchumi ya wananchi wetu. Barabara hizo ambazo tumewaomba zitawasaidia wananchi wetu kwa mfano tuliomba Barabara ya kutokea Mpanda - Kaliua mpaka Kahama. Barabara ambayo ina-cut across mikoa mitatu ina umuhimu gani, kwa sababu maeneo yetu sisi kwanza tunazalisha sana tumbaku, tunalima sana mpunga, lakini bado tunalima mazao ya mahindi na mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo wa barabara kama hii kiuchumi tafsiri yake ni kwamba sisi tutaweza kuuza mazao yetu kwa bei kubwa sana, lakini tafsiri yetu ya pili tutakuwa na uwezo wa kusafirisha mazao yetu mfano mchele tunauza sasa hivi Uganda, tunauza Rwanda, lakini ule mzunguko uitafute Nzega tofauti na barabara tunayowashauri unakuwa umekwenda nje ya kilomita 250. Sasa ushauri kama huu mkiwa mnauzingatia tutakuwa na mipango ambayo ni endelevu na mipango mizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii nimeanza nayo kwa sababu gani? Barabara hii kwenye Ilani ya Chama ipo, 2010 - 2015 ipo 2015 - 2020 ipo sasa tuna 2020 - 2025 ipo. Nashauri tuwe na utashi wa mambo ya msingi kwa sababu tunaweza tukawa tumeweka Mipango ambayo haitekelezeki hapa ikaishia kwenye maneno na siyo kwenye vitendo tutapata shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwashauri haya mambo ambayo tunawashauri sisi Waheshimiwa Wabunge ndio tunajua njia sahihi na ndio tunaishi kwenye yale mazingira tunaona hali halisi ya nchi yetu inakwendaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kweli wapo wasomi wa kutosha humu lakini usomi peke yake hautoshi kwa sababu usomi ni issue nyigine na utendaji ni issue nyingine. Kwa hiyo niwaombe ndugu zangu hawa wahakikishe yale ambayo sisi tunayashauri ya Mipango ya Maendeleo wanayaingiza kwenye Mpango huo wa 2024/2025 ikiwemo hii Barabara ya Mpanda - Kaliua mpaka Kahama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ambalo naweza kushauri, nimejiuliza hii Mipango naomba muipitie vizuri sehemu moja. Tunapopanga Mipango yetu nadhani sasa hivi tunazingatia population. Sasa inawezekana hatuzingatii vizuri population kwa sababu yapo maeneo yenye idadi kubwa sana ya watu, hatujaangalia ni miradi gani mikubwa ya kitaifa tupeleke kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni nini maana yake sasa? Utakuta maeneo yenye population ndogo yatapelekewa miradi mikubwa, yatapelekewa miradiya masoko na mambo mengine, wakati kuna population kubwa ambayo ingeweza kuzungusha fedha, ingeweza kufanya biashara, tunaacha. Kwa hiyo nashauri, jambo hili ni la msingi kulizingatia kwamba maaamuzi yenu pamoja na takwimu na sasa hivi Serikai imepata idadi ya watu, basi naomba mipango iendane na maeneo husika na historia za maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilianza kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa sababu ya miradi mikubwa inayoendelea nchini. Jambo kubwa la SGR jamani ninaomba kabisa tusilipige vita. Tuliunge mkono kwa sababu njia nyepesi ya usafirishaji itakazoziokoa Barabara zetu nchini ni pamoja na reli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukaangalia gari la mizigo moja kwa maana ya reli linabeba behewa 40 na utumiaji wa mafuti hauwezi ukawa sawa na malori ambayo yatafuatana njia nzima huku yakiharibu na mizani na kila kitu. Kwa hiyo maamuzi yake ya kujenga reli ya SGR hususani ya Tabora – Kigoma hususani ya Kaliua - Mpanda. Ni jambo ambalo sisi tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu linakwenda kuinua mishipa yetu ya kiuchumi na wananchi wataweza kupata pato na pato na Taifa litaweza kupanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie kwenye Sekta ya Utalii. Hapa naona kama vile mipango yetu mingi haijawekeza nguvu ya kutosha. Tunazo National Parks nyingi sana karibu 22 hivi. Sasa National Park zote hizi tujiulize hivi wakati wa masika zote zinafikika? Je, tutakuwa na seasonal utalii? Tena utalii wa kiangazi tu unasubiri mvua ikiwa imekata. Maana yake ninyi mmesoma, Maprofesa mmejaa, Ma-doctor mmejaa. kweli tunashindwa ku-cover kipindi cha mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tupeleke fedha nyingi sana kwenye ujenzi wa hoteli za kutosha, camp za kutosha barabara za kutosha, mawasiliano ya kutosha. Sisi kule tuna National Park moja nzuri sana, sisi tunaona ni kama Eden village, Ugalla National Park, lakini ukiangalia hata advertisement ukiangalia TV mipango ya kutangaza michache, sasa unajiuliza hivi hawa watu wataifahamu vipi? Hata upite barabarani kabango kake unakuta ukubwa huu hapa. Kwa nini tunashindwa kuwa wa kisasa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri ili tuendane na usasa, ni lazima tuhakikishe vivutio vyote kama Mheshimiwa Rais alivyokuwa frontline kutangaza utalii hebu na sisi tusimame naye. Bahati nzuri vivutio Mungu ametubariki jamani ni kila sehemu vipo. Ukienda Kigoma kuna Gombe, Tabora kuna Ugalla, ukienda sijui Katavi National Park ipo ukienda maeneo yote Nyanda za Juu Kusini zimejaa Ruaha na kila kitu mpaka kaskazini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tufungue fursa hizi siyo kwa kuangalia njia moja tu kwamba huku ndio kunawezekana watalii wengi, kumbe na kule tunaweza hata utalii wa ndani tunaweza. Sisi Kaliua idadi yetu ni 768,000, hata tukifanya utalii wa ndani tu unatutosha. Tumeuza zetu mazao vizuri, miradi imefunguka, tunatakiwa tukapumzike, sasa kipindi kama hiki huwezi ukapumzika, Christmas unaishia nyumbani tu. Kwa hiyo Serikali tukiishauri haya iyazingatie kwa faida ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naweza kushauri, maeneo yetu mengi naomba tuelekeze nguvu kwenye ujenzi wa maghala. Wakulima wengi wanashindwa ku-store na wanaibiwa sana mazao yetu nchini. Anashindwa ku-store mazao yake, ku-upgrade mazao yake ili ikifikia msimu fulani sasa nakwenda Uganda kuuza mchele wangu utakwenda, nakwenda kuuza sehemu fulani mazao yangu yatakwenda, wana-store wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, naomba kabisa Serikali itoe msukumo uhifadhi wa maghala. Zamani nakumbuka tulikuwa tunahifadhi kienyeji wakati wa Mwalimu Nyerere, tulipewa vile vihenge vile, lakini sasa hivi hata hawaji kushauri, tujenge hivyo vitu vya msingi ili tuhakikishe wananchi wetu wanakaa vizuri na mazao yao yale na niombe kwa hapo hata Kaliua kuna maghala yanaendelea pale, tayari maeneo yako wazi Ndugu yangu Bashe anafanya kazi nzuri sana, nimwombe atoe msukumo tukamilishe pale maghala matatu, la Zuginole, Igwisi, Ughansa kule kuna wakulima wakubwa na wa kutosha. Kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri tuendelee na hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napata wakati mgumu wakati tunapanga hii mipango yetu. Hivi tunapanga hii mipango yetu ni kutokea Wilayani kwenye Taifani au mpaka kijijini? Kama tunapanga mpaka kijijini waelewe kwamba vipo vijiji ambavyo kipindi cha masika huwezi kufika Makao Makuu ya Kijiji kwa shida ya miundombinu. Matokeo yake ni nini? Kama ni debe la mahindi lilikuwa liuzwe Sh.2,000 matokeo yake litauzwa Sh.500.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, wao wanajua jiografia yetu na wanajua watu wanavyojituma, tuangalie hii mishipa ya kiuchumi tuweze kuifungua vizuri. Nimshukuru Waziri na hili moja naleta kwake ni ombi maalum pamoja na Mheshimiwa Naibu Spika kusema, lakini hili ni ombi maalum mezani kwake kuna ombi la wananchi wa Kaliua. Tuna shida ya miundombinu, tulishaleta mezani kwake lina muda mrefu kama miezi sita na Kamishna anafahamu na Waziri anafahamu, wananchi kule wanateseka barabara zilikatika awamu iliyopita, tumeomba emergence na special fund, mpaka sasa sijui wanakwenda kulimaje? Kwa hiyo, niombe Waziri atusaidie ili tuweze kwenda pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii mipango tunayopanga lazima tuangalie afya za wananchi wetu, ni lazima tuhakikishe uzalishaji ni pamoja na kuwa na afya bora, wakiwa na afya mbovu, hatutarajii kabisa uzalishaji utakuwa mzuri. Sasa wakiugua kama Kituo cha Afya hakiko karibu, kama zahanati haiko karibu uzalishaji unakuwaje? Anatumia muda mwingi kusafiri kwenda kufuata kituo cha afya au zahanati. Naomba haya yote tuyaingize kwenye Mpango wetu wa 2024/2025 ili Mheshimiwa Rais kuhakikisha mambo yake yanakwenda vizuri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)