Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nimepitia vyema taarifa ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2024/2025. Vilevile nimepitia vyema Taarifa iliyosomwa na Waziri wa Fedha, Taarifa ya Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali 2024/2025; na vilevile nimeshiriki katika maandalizi ya Taarifa yetu ya Kamati ambayo imewasilishwa na Makamu Mwenyekiti kwa niaba ya Mwenyekiti wetu, na nimemsikiliza vyema pia alipokuwa anaisoma hapa mbele ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri sana tunapojadili mapendekezo ya mpango, tukaifahamu historia kidogo ya chombo ambacho kimekuwa kikipanga mipango toka tumepata uhuru. Ni muhimu kujua historia hii kwa sababu lipo jambo ambalo mimi nafikiri na ninaamini hatulifanyi kwa usahihi, tunalikosea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1961 mpaka 1964 mipango yetu imekuwa ikipangwa na Tume ya Maendeleo ya Uchumi, tukaona haifai, tukabadilisha. Mwaka 1965, mwaka mmoja tu mipango yetu tukaipeleka Ofisi ya Rais, Idara ya Mipango na Maendeleo; tukaona haifai tukahama. Mwaka 1965 mpaka 1975, miaka 10 hapo tukakaa, mipango yetu ikawa inapangwa na Wizara ya Uchumi na Mipango ya Maendeleo; tukaona haifai tukahama. Mwaka 1975 mpaka 1980, miaka mitano mipango yetu ikawa inapangwa na Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango; tukaona haifai, tukahama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, 1980 mpaka 1985, 1985 mpaka 1989 tukarudi kwenye Wizara ya Fedha, Mipango na Uchumi, tukaona haifai tukahama. Mwaka 1989 mpaka 2000 mipango yetu ikawa inapangwa na Tume ya Mipango, tukaona haifai tukahama tena. Mwaka 2000 mpaka 2005 tukaenda Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji, haikutosha, tukaona haifai tukahama. Mwaka 2008 mpaka 2016 mipango yetu ikawa inapangwa na Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, tukaona haifai, tukahama. Mwaka 2016 mpaka 2023 mipango yetu ikawa inapangwa na Wizara ya Fedha na Mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwa historia hiyo ya kuonesha namna ambavyo Taifa limehangaika kupata wapi mipango ipangwe, nani asimamie mipango; nimesimama hapa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Maeneo yote haya ambayo nimeyataja na kuhamishwa kwa Idara hii ya Mipango imekuwa ikifanyika tu kwa Presidential Decree. Rais anakuja anatoa tamko, mipango ihamie sehemu fulani kama ambavyo nimeonesha. (Makofi)

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kakunda, taarifa.

TAARIFA

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa mzungumzaji kwamba confusion kubwa ilitokea mwaka 2001 wakati ambapo Idara ya Kuondoa Umaskini ilipelekwa katika Ofisi ya Makamu wa Rais nayo ikawa inapanga mipango. Hiyo ni taarifa. (Kicheko/Makofi)

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo, na pana story ndefu sana kwenye hili ambalo amelisema Mheshimiwa Kakunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu mwaka 2023 amerejesha Tume ya Mipango chini ya Ofisi ya Rais na siyo tu by Presidential Decree, ameirejesha kwa sheria. Kwa hiyo, hivi sasa tunayo Sheria ya Bunge tuliyoitunga hapa juzi ya kuanzishwa Tume ya Mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ya sheria ile inasema, Tume ya Mipango, Kuanzishwa kwa Tume; kipengele cha 4(1) na (2) kinasema; “inaanzishwa Tume itakayojulikana kama Tume ya Mipango. Tume itakuwa Idara itakayojitegemea chini ya Ofisi ya Rais.” Sasa nimepongeza hatua hii ya kurejeshwa Tume ya Mipango na kutungiwa sheria ya uwepo wake, lakini kuna jambo moja ambalo nataka nilishauri na Serikali mlichukue. Hili litatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, usipokuwa na chombo imara cha kupanga mipango, definitely huwezi ukaisimamia mipango hiyo. Huwezi kuifanyia tathmini mipango hiyo. Kwenye hili siyo, tu kwamba nashauri kama Mbunge wa Handeni Mjini, lakini nashauri kama mtu aliyesoma Mipango. Hapa tuliposema tume itakuwa Idara itakayojitegemea chini ya Ofisi ya Rais, natamani sana Serikali na Bunge tukafanya marekebisho. Tume hii ili tuwe na mipango mizuri na tuweze kuisimamia, twendeni tukaifanye kuwa taasisi (an institution). Ikiwa ni taasisi itatusaidia mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, itatusaidia kuandaa wataalamu watakaopata uzoefu wa muda mrefu, lakini kutakuwa na urahisi wa kufanya transitions kutoka kizazi na kizazi, pia kutakuwa na mwendelezo hata wa mipango yenyewe kwa sababu ni taasisi. Hivi sasa kwenye hii Tume ambayo ipo chini ya Mheshimiwa Prof. Kitila kwenye Wizara yake, hii Tume inayojitegemea, ukiuliza leo wafanyakazi wa Tume hii, atakwambia anaokotaokota kutoka idara nyingine za Serikali. Haipaswi kuwa hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalieni maeneo ambayo tumetumia taasisi kufanya jambo na mwone ambavyo tumefanikiwa. Angalia leo TRA kama taasisi, angalia leo NBS kama taasisi. Ni muhimu Tume hii ya Mipango ikawa ni taasisi wala siyo Idara chini ya Ofisi ya Rais. Ikiwa taasisi, hatuiondoi pale kwa Rais. Inakuwa ni taasisi inayojitegemea ambayo iko chini ya Rais kwa sababu mipango ni instrument ya Rais katika kuleta maendeleo kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitawapeni mfano wa wenzetu ambao wamefanikiwa sana. Mfano nchi ya India, Mheshimiwa Rais alikwenda kule na bahati nzuri niliona Mheshimiwa Prof. Kitila aliambatana na Mheshimiwa Rais kule. Nina imani kwamba yapo ambayo mmejifunza. Pale India wana Tume ya Mipango (Planning Commissioner) ambaye leo hivi nilivyosimama imetimiza miaka 73. Ipo toka mwaka 1950 ipo pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi miaka yote 62 ambayo nimeitaja kwenye ule mlolongo toka mwaka 1961 mpaka leo tunatangatanga wapi pa kuiweka Tume ya Mipango, halafu wakati mwingine inakuwepo, wakati mwingine haipo. Sasa unaandaa vision ya miaka zaidi ya 20 halafu msimamizi ndani ya miaka mitano amefutwa! Unaandaa Mpango wa miaka mitano mitano ili kutekeleza vision ndefu ya miaka mingi, halafu Tume ya Mipango haipo, imefutwa. Definitely mpango wako huwezi kuusimamia. Ninatoa mifano michache hapa kuonesha namna gani tumeshindwa kuusimamia mpango kwa sababu ya structure yenyewe ya wapi chombo cha mipango kikae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna madini. Ameongea Mheshimiwa Mzee Njeza, tuna madini tusiyoweza kuyachimba miaka 62. Hii ni mifano michache sana natoa ili tuone kwamba tusipokuwa na chombo madhubuti, taasisi ya kusimamia na kuandaa mipango tutakuwa tuna-miss target na indicators nyingi ambazo tunakuwa tumejiwekea wenyewe. Tuna madini tusiyoweza kuyachimba, tuna samaki tusioweza kuwavua. Kwenye hili nimpongeze Mheshimiwa Rais. Just imagine kwa mara ya kwanza ndiyo Serikali imenunua vyombo vya uvuvi na kuvigawa nchi nzima. Yaani Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kana kwamba tumetoka msituni au tumepata uhuru leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aliongea Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwenye ziara ya Mheshimiwa Rais kule Singida, hata yale yanayofanyika kwenye Afya, yote yanafanyika kana kwamba tumetoka msituni na tumepta uhuru leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa ambavyo Mheshimiwa Rais anapeleka, zahanati na vituo vya afya vinavyojengwa, lakini vyote hivi tungekuwa na Tume ya Mipango ambayo ni taasisi tungekuwa tumeshajenga uwezo wa kusimamia na kuyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalieni mambo ambayo tume-miss target. Tuna hekta milioni 29.4 ambazo zinafaa kwa umwagiliaji, lakini muulize Waziri wa Kilimo tumeweza kumwagilia ngapi kwenye hizo hekta milioni 29? Tumeweza kumwagilia hekta 822,000. Tuna-miss target kwa sababu ya kukosa mipango mizuri na taasisi ya kusimamia mipango hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna vivutio vya utalii vingi sana, na tumshukuru Mheshimiwa Rais kwa ile Royal Tour ambayo imetusaidia kuongeza watalii, lakini angalia; tuna vivutio vya utalii vingi sana ambavyo malengo yetu tulitaka tufikie watalii milioni tano na tupate fedha za kigeni six billion USD na tutengeneze ajira 1,750,000. Fanya tathmini leo, tuko mbali mno ya malengo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa mwisho, tuna Gridi ya Taifa ambayo haijakamilisha urefu wa 9,351 kilometa na tuna uzalishaji wa umeme ambao haujafika megawati 4,915. Tusipokuwa na taasisi na tusipoifanya Tume hii kuwa taasisi tutaendelea kuya-miss malengo na tutashindwa kuyasimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo ningependa kwenye mpango huu lijitokeze ukiacha huu ushauri wa kuifanya Tume kuwa taasisi huru, taasisi inayojitegemea, taasisi inayoripoti kwa Mheshimiwa Rais, taasisi ambayo ni instrument ya Mheshimiwa Rais, jambo lingine kwenye mpango huu ambao tulitaraji kuliona lakini halija-surface ni tathmini ya mpango wenyewe. Tunafunga vision 2025 na ni miaka miwili tu baadaye, ni mwaka mmoja baada ya mpango huu kupita mwezi wa tatu, lakini hatujapata kufanya tathmini ya ule mpango. Kwa kweli siyo tu tathmini ya miaka mitano hii ya mwisho, tunataka tuone tathmini ya jumla ya miaka yote hii ambayo tumei-practice vision 2025. Hii tathmini inatakiwa ifanyike mapema ili ituwezeshe kuandaa vision nyingine ya mbele. (Makofi)

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Taarifa.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nimpe taarifa mzungumzaji kwamba tunashindwa kufanya tathmini hiyo Mheshimiwa Kwagilwa kwa sababu hatuna taasisi inayojitegemea. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa taarifa hiyo unaipokea?

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hii. Unajua ukiwa unaongea hapa Bungeni, unamuambukiza mwenzako umeme hapa. Kwa hiyo, ameelewa kabisa nilichokuwa nakisema kwamba ni muhimu tukawa na taasisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosekana kwa taasisi kumefanya hata mpango wetu tukiuandaa, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, Ilani ya chama changu mimi ndiyo imekuwa kiongozi wa mipango ya nchi hii. Ndiyo Ilani ya Chama, wakati kumbe it was supposed to be the opposite. Inatakiwa Ilani zote za vyama zi-refer kwenye mpango, yaani chama A kituambie tu wanafanyaje kufikia mpango wetu wa Taifa kuukamilisha, chama B watuambie hivyo. Hata ukisoma mpango leo watakwambia rejea yao walitumia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Vyama vingine ndiyo kabisa hata rejea hazipo, maana ni vyama hata Ilani havina. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)