Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia kwenye Taarifa yetu ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii. Napenda kuanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa anazozifanya za kuimarisha haki za wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi hizi zinaenda sambamba kabisa na namna ambavyo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Katiba na Sheria wameanzisha Samia Legal Aid Campaign ambayo inalenga kwenda kutatua maeneo mbalimbali ya changamoto za wanawake kupata haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika, namshukuru sana Mheshimiwa Spika na Wabunge wenzangu wote ambao tulichangia katika Miswada ya Sheria ambazo zinahusu masuala ya siasa na uchaguzi, na kwa namna ambavyo tuliibeba agenda ya wanawake na hadi kupelekea kuweza kuongeza vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kama moja ya kosa la uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huo, mchango wangu utajielekeza katika maeneo manne yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni Sheria ya Ukatili wa Kijinsia kwa maana ya GBV; tukirejea wakati tunajadili hapa Bungeni kwenye kupitisha Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama alielezea namna ambavyo Serikali imetambua ukubwa wa tatizo la ukatili wa kijinsia na kwamba sasa Serikali iko mbioni kuleta Bungeni Muswada wa Sheria ya Ukatili wa Kijinsia kwa maana ya GBV.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nijielekeze katika eneo hili. Serikali ifanye jitihada ya haraka ituletee huu Muswada Bungeni kwa maana ya Muswada wa Sheria ya GBV na Sheria hii itakayokuja hapa Bungeni isijielekeze tu katika kuweka makosa na adhabu zake yaani offences na penalties, lakini pia ijielekeze katika kutoa elimu ya namna ya kupambana na kuthibiti vitendo vya GBV na vilevile ijielekeze katika namna ya kutoa compensation kwa wale wahanga ikiwemo na adhabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo napenda kusisitiza kwamba Sheria hii ya GBV isiyajumuishe makosa yote kwenye kundi moja, badala yake iainishe makosa kwenye makundi tofauti kulingana na jinsi yalivyo. Kwa mfano, ukatili wa kijinsia mitandaoni, kwenye ndoa, nyumbani, watoto na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni kuhusiana na umiliki wa ardhi kwa wanawake. Kumekuwa na changamoto kubwa sana ya umiliki wa ardhi kwa wanawake japokuwa Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1995 inazingatia kwamba umiliki wa ardhi kwa wanawake na inaainisha iwe vipi, lakini kuna Sheria mbalimbali ambazo zinakinzana na jambo hili. Kwa hiyo, hapa napenda kupendekeza kwa Serikali kwamba lazima ije na mfumo wa kisheria na kikanuni ambao utaweza kurahisisha namna ya kuhakikisha wanawake wanamiliki ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kipekee nampongeza Mheshimiwa Jerry Silaa, Waziri wa Ardhi pamoja na Mama yangu Mheshimiwa Waziri Dkt. Dorothy Gwajima kwa namna ambavyo wanashirikiana kwa ukaribu kutatua changamoto za umiliki wa ardhi kwa wanawake likiwemo eneo la mirathi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili halipaswi kuwa kwa utashi wa viongozi, kwa hiyo, ni vyema sasa Serikali ione namna ambavyo itaweka mfumo rafiki kuhakikisha masuala ya wanawake ya umiliki wa ardhi yanaratibiwa ipasavyo. Kwa mfano, kunaweza kukawa na dawati la umiliki ardhi kwa wanawake na watoto wa kike ndani ya Wizara hii inayosimamia masuala ya Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, halikadhalika hivyo hivyo kwenye Wizara ya Ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ni kuhusu MTAKUWA. Wote tunafahamu kwamba Serikali iko mbioni kukamilisha Mpango wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto Awamu ya Pili. Sasa katika maeneo haya, yako maeneo mawili ambayo napenda kusisitiza kwa Mheshimiwa Waziri Dkt. Dorothy Gwajima kuhakikisha kwamba MTAKUWA unayazingatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari hapa Bungeni tumeshatambua kisheria kwamba vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia katika uchaguzi ni kosa la uchaguzi. Vivyo hivyo basi na kwenye MTAKUWA itakuwa ni vyema pia kutambua unyanyasaji na ukatili wa kijinsia katika uchaguzi kama moja ya maeneo ambayo MTAKUWA lazima iangazie. Jambo la pili, ni ukatili wa kijinsia mtandaoni kwa wanawake, mabinti, watoto na jinsia zote. Ni muhimu sana jambo hili nalo likazingatiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la nne ni unyanyasaji katika maeneo ya kazi. Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kidunia pamoja na ya kikanda. Mathalan, kwa haraka haraka Tanzania imeridhia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Binadamu, Article 2 na 21 ambayo inaangalia haki za kisiasa bila ubaguzi, pia imeridhia Mkataba wa Haki za Kisiasa kwa Wanawake wa1952, pia imeridhia Beijing Declaration and Platform for Action ya Mwaka 1995; pia tumeridhia Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu Juu ya Haki za Wanawake ambayo hii ni Itifaki ya Maputo 2003; vilevile tumeridhia Itifaki ya SADC ya Usawa wa Kijinsia 2008 pamoja na Mkataba wa Kuondoa Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW) 1979, lakini Tanzania tuliridhia 1985.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia upo Mkataba mmoja wa Kimataifa ambao bado Tanzania hatujaridhia. Tanzania bado hatujaridhia Mkataba wa C190 ambayo inahusu sexual harassments at work. Yaani kwa maana kwamba bado hatujaridhia Mkataba wa Kimataifa…

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.


TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Neema, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jacqueline Msongozi.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Neema Lugangira kwa namna ambavyo anachangia hasa kwenye hili eneo la ukatili wa kijinsia makazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka tu niongezee kwake kwa maana ya taarifa, kwamba siyo tu makazini kwa maana ya maofisini kama alivyosema, lakini pia kumekuwa na ukatili wa kijinsia kwenye maeneo ya kazi ambayo kwa wafanyakazi wa majumbani. Kwa lugha nyingine ni ma-house girl na ma-house boy. Kumekuwa na ukatili mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, anapozungumza, basi aongeze na hilo ili sasa Muswada utakapokuwa unaletwa hapa Bungeni, basi uzingatie pia kwenye maeneo haya kwa sababu kwenye maeneo haya ni waathirika wakubwa pia, ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Neema, taarifa unaipokea?

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea hiyo taarifa na huko ndiko ambako nilikuwa naelekea, kwa sababu tunapoongelea huu Mkataba wa Kimataifa wa C190 wa Sexual Harassment, maeneo ya kazi ni maeneo yote yakiwemo majumbani. Pia uko Mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambao una vipengele mbalimbali. Katika itifaki hizi za mikataba ya kimataifa na kikanda, siyo lazima nchi iridhie vipengele vyote. Kwa hiyo, sisi kama Tanzania tunaweza tukachambua tukachagua maeneo ambayo yanaweza yakaendana na tamaduni, desturi na namna ambavyo Tanzania tunaendesha masuala yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea ukatili huu wa kijinsia na unyanyasaji kwenye maeneo ya kazi ni pamoja…
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Neema, taarifa kutoka kwa Naibu Waziri Mheshimiwa Patrobass.

TAARIFA

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Nampongeza sana Mheshimiwa Neema, ana ujuzi na ubobevu mzuri kwenye hayo maeneo, lakini ni muhimu wakati anachangia mchango wake mzuri akumbuke pia tayari kwa Tanzania tumeshazingatia maeneo mengi. Tunayo Sheria yetu ya penal code ambayo ilifanyiwa maboresho baada ya kuwa na Sexual Offences Special Provincial Act ya Mwaka 1998.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria hii ilikuwa inahusiana na masuala ya makosa yote yanayofanana na masuala yanayohusiana na unyanyasaji wa kijinsia. Utakumbuka kuna kipindi ilikuwa hata kukonyeza ni kosa, kwa hiyo, ikawekwa kwenye Sheria yetu ya Penal Code. Sheria Penal code iko extensive sana kwa maana kwanza ina-establish offence na pili inaeleza adhabu na utendekaji wa kosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ili aweze kuendelea na mchango wake, kwenye Sheria yetu ya Rushwa na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, zimetambua makosa hayo specific, masuala ya sexual harassments kuwa ni makosa. Kwa hiyo, hatuko nyuma, tusiseme kama vile Tanzania iko nyuma sana.

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Neema malizia mchango wako, muda umeisha.

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naomba unilinde, nataka tu kumsahihisha kidogo kaka yangu Wakili mbobezi kabisa, hakuna ambapo nilisema kwamba Tanzania haijafanya vizuri, na ndiyo maana nilianza kwa kutambua mikataba yote ambayo Tanzania imeridhia Kimataifa na Kikanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nikasisitiza na nikatambua kauli ya Serikali wakati tunajadiliana hapa kwenye Miswada ya Sheria za Uchaguzi na masuala ya siasa kwamba Serikali yenyewe imetambua kwamba kwa ukubwa wa changamoto ya masuala ya ukatili wa kijinsia, ije na sheria mahususi ya GBV. Hata mwaka 2022, SADC tayari wametoa SADC GBV Model Law. Kwa hiyo, ni kwa muktadha huo huo najaribu kuainisha kwamba, ni lazima sasa ile ahadi ya Serikali iliyoitoa ndani ya Bunge hili siku ya Ijumaa wiki iliyopita, sheria ile ije kwa haraka ili maeneo haya yote ya GBV kwa umahususi wake yaweze kuzingatiwa badala ya ilivyo hivi sasa. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Neema.

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)