Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na niweke tu sawa hapo ni Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini pia nimpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya na mabadiliko makubwa mno kwenye kila sekta ya Wizara zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Waziri wa Elimu, Profesa lakini nimpongeze pia Kaka yangu Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo na timu yote. Nimpongeze Mwenyekiti wangu wa Kamati, ametuongoza vizuri lakini pia niwapongeze Wajumbe wa Kamati, kwa kweli wamekuwa na imani nasi na tumefanya kazi vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka nijikite sana kwenye Wizara ya Michezo, Sanaa na Utamaduni na sababu ya msingi ndiyo Wizara pekee ambayo ina ukomo mdogo wa bajeti. Mwaka 2023 tumepitisha hapa bajeti ya bilioni 35. Katika bilioni 35, fedha za maendeleo ni bilioni 11.8. Katika miradi 14 ni miradi minne tu imepokea fedha mpaka sasa hivi tunavyozungumza. Vile vile, hii miradi minne ni kama bilioni mbili tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najaribu kutazama. Mpaka tunafika Juni mana yake sisi mliotupatia kazi ya kusimamia Wizara hii ya Michezo, tutashindwa kwenda tukasimamie nini, tukaangalie mradi gani wakati hawana fedha? Sasa, jambo hili linatupatia wakati mgumu sana. Kamati tumeeleza Vizuri na mimi nataka niweke msisitizo. Hatuwezi kuendelea kwa utaratibu huu wa Wizara kutokupewa fedha wakati tumepitisha bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo hii tunapozungumza, 2027 sisi ndiyo wenyeji wa AFCON Mungu akitujalia uhai, lakini mwakani 2025 hii timu ya AFCON (ambao wanaandaa AFCON) watakuja kukagua viwanja. Viwanja ambavyo tunatarajia sasa hivi tuwe tunazungumza kwamba Wizara imeanza kujenga ama kukarabati viwanja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanja cha Arusha pekee kinahitaji zaidi ya bilioni 187.5. Dodoma kinahitaji zaidi ya bilioni 187.5. Hapo sijazungumza recreation center, Dodoma tu inataka bilioni 32, kule Arusha inataka bilioni 21 kwa ujumla wake unazungumzia kama bilioni 492. Hizi fedha zinatakiwa ziwe zimekwishatengwa kwenye bajeti. Bajeti ambayo tunaizunguzmia sasa tunazunguzmia bilioni 35 na hiyo bilioni 35 fedha haijatoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napata mashaka watakapokuja kutukagua sisi mwakani, je, haya maandalizi tutakuwa tumekwishafanya ya kutosha? Maana yake ni kwamba, kama tusipokimbia kwa sasa AFCON 2027 tutaikosa na kwa nini tuikose? Tutaikosa kwa sababu Serikali haijaamua kwa dhati kuweka fedha kwenye maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaombe ndugu zangu wanaohusika kwenye eneo hili, huu ndio wakati sahihi wa kupeleka fedha kwenye Wizara ya Michezo ili tuweze ku-meet yale mahitaji ambayo yanatakiwa na AFCON. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetembelea kiwanja cha Benjamini Mkapa, hali ni mbaya sana. Tumetenga zaidi ya bilioni 31 kwenye bajeti na zimetoka bilioni saba. Katika zile bilioni saba juzi tumetembea uwanja umekarabatiwa kwa asilimia 24 tu, shilingi bilioni saba kwa hesabu yao ulitakiwa ufikie asilimia 40, sasa asilimia 24 unazungumza leo, mkataba unaisha tarehe 24 Agosti, 2024. Tumebakisha miezi sita tu, hata leo Wizara ya Fedha wakisema watupatie fedha yote twende tukamalize ukarabati, nina uhakika hatuwezi tukamaliza ule ukarabati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka muone hali ilivyo mbaya, kama una uwanja wa Taifa leo uko asilimia 24 na Serikali imetenga fedha lakini bado hakuna kazi inayofanyika ya kuturidhisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema nini hapa? Mshauri mwelekezi ambaye tumempa kazi sisi ambaye ni TBA ndiyo jicho letu, nina mashaka kama ana uwezo wa kusimamia miradi mikubwa kama hii. Yeye ndiye alitakiwa atuambie anakwama wapi ili turudi kwenye mikataba yetu tuone huyu Mkandarasi tuliyempa kazi, hana uwezo wa kufanya kazi yetu. Sasa sisi mmetuambia tukasimamie na sisi tuwe sehemu ya kulaumiwa. Hatutakuwa tayari kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba Serikali, leo hii kama unafikia asilimia 24 na imebaki miezi sita mkataba uishe, wanataka kutupeleka wapi na uwanja huu ndiyo unaotegemewa? Napata mashaka huko tunakoelekea kwenye kuandaa mashindano ya AFCON. Tunaweza tusifikie malengo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine muhimu sana nataka nilielezeeā€¦

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Sima, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Bashungwa.

TAARIFA

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Sima anachangia vizuri lakini nilitaka nimpe Taarifa kwamba, TBA inafanya kazi nzuri na ina uwezo mzuri. Kwa hiyo, nilitaka nimpe hiyo Taarifa kwamba tuko vizuri. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Sima, taarifa hiyo unaipokea?

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamheshimu sana Kaka yangu, mimi ni mwanamichezo, nazungumza kitu ambacho nimekiona, ataniwia radhi. Kwenye eneo hili niko very serious, tunazungumza 24 percent, tulitakiwa tufikie asilimia 40. Mimi mashaka yangu, kama kweli TBA wana uwezo huo, inawezekana wanao lakini mimi nimejionea. Nimeonesha mashaka, kwenye hili naomba waniwie radhi sana. Tunatakiwa tufanye kazi kwa uhalisia, Serikali inatakiwa iwe serious kwenye mambo ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kueleza eneo hili la sport betting. Mwaka 2020 tulifanya amendment hapa (Miscellaneous Amendment) kwenye Wizara ya Fedha. Tukasema kuwe na asilimia tano iende kwenye maendeleo ya michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza miaka mitatu sasa, tukiomba taarifa ya kile kilichopatikana, hatuwezi kupata taarifa iliyokamili. Mpaka sasa hatuna taarifa kwamba, imekusanywa nini kwa mwaka ili tuweze kupata hiyo asilimia tano. Hakuna anayeweza kuelewa jambo hili. Pia, ndiyo maana Mheshimiwa Taletale amesema sanana kwenye Kamati amesema sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema nini? Huko tunakoelekea kama hatuwezi kuwa na taarifa kamili ya fedha inayokusanywa halafu ukapewa asilimia tano, itakuwa tunafanya hisani wakati sisi tumetunga sheria ambayo inatakiwa Sheria hii tuitekeleze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo ningependa kuishauri Serikali. Kuna haja ya makusudi kabisa, fedha hii ambayo inakusnywa na TRA sina mashaka na Mamlaka ya Mapato. Fedha hii ikitoka TRA inakwenda kwa watu wa Hazina, mambo haya yawekwe wazi, tumekusanya nini na asilimia tano yenu ni hii. Hilo ni jambo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili. Sisi tunapaswa fedha ambayo inatengwa kwa asilimia tano wapewe, wapewe kwa wakati. Leo unaona hizi timu za Taifa zote zinategemea Baraza la Michezo la Taifa kuziwezesha kuweza kuendelea na mashindano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa juzi umeona wamefanya harambee. Sasa kama Wizara imeanza kutembeza bakuli maana yake inatupeleka wapi? Unatembeza bakuli wakati hela unayo na Serikali inajua hela yao ipo. Kwa nini wasipewe hela yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi mmetupatia kazi ya kusimamia Wizara kwenye suala la maendeleo, hamuwapi fedha na fedha yao wanayo ipo, wananchi tayari kwenye Sport Betting tayari fedha imekwishapatikana. Nataka niiombe Serikali, ni muhimu mno na ni jambo la msingi tunahitaji maendeleo ya michezo tuweze kuyasimamia na tuyasimamie kwa dhati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi kwa kweli nakushukuru sana. nakushukuru na ninajua kwenye Kamati yako ya Bajeti wewe ndiye Mwenyekiti. Haya tunayoyasema kwa uchungu utarudi kule kwenda kuangalia lile kapu la Wizara ya Fedha kuwawezesha wenzetu hawa kupata fedha ili tuweze kuendelea. Ahsante sana. (Makofi)