Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na mimi kuniruhusu nichangie hii hoja ya Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii. Mimi nitaongelea mambo matatu, jambo la kwanza ni Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, pili ni programu ya kukuza ujuzi na Sheria ya Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Mfuko huu wa Maendelo ya Vijana. Mfuko huu ulianzishwa mwaka 1993 na mpaka mwaka 2023 ulikuwa umekopesha vijana wetu jumla ya shilingi bilioni 8.9 hongera sana Serikali. Mfuko huu una mapungufu makubwa mawili, kwanza Serikali imekuwa ikitenga shilingi bilioni moja kila mwaka tangu mwaka ule wa 1993 lakini hasa hasa kuanzia mwaka 2015 mpaka 2022. Kwa hiyo ukipiga hesabu jumla ya hela zote ilikuwa bilioni tisa lakini mpaka 2020/2021, 2021/2022 ilikuwa imekusanya bilioni moja tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Serikali imeufelisha Mfuko huu kwa sababu mwaka 2022/2023 kulikuwa na maombi ya shilingi bilioni 6.7 ya mikopo lakini mfuko ulikuwa na shiling bilioni tatu tu, kwa hiyo ukashindwa kabisa kufanya wajibu wake. Mfuko pia umekuwa na utata wa pili wa kukusanya madeni ambapo mwaka 2022/2023 Mfuko ulipata marejeshio ya shilingi bilioni 2.6 lakini ulikuwa unadai jumla ya shilingi bilioni 4.6, kwa hiyo hela nyingi haijakusanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi inayochangiwa na theluthi moja ya Tozo ya CBL kutoka kwa waajiri wote Tanzania, Kamati ilibaini kuwa mgao huo umekuwa ukipungua kila mwaka. Mfano, kutoka bilioni 18 mwaka 2019/2020 mpaka bilioni tisa tu mwaka 2023/2024, upungufu huo umefanya idadi ya vijana waliotakiwa kuwasomesha kupata ujuzi kupungua kutoka 42,000 kwa mwaka mpaka 12,000. Jambo hili limeangusha programu nzima. Kwa hiyo, Serikali imepunguza idadi ya wanaotakiwa kupokea mafunzo hayo kutoka wale watu iliyokusidia kuwafundisha kwa mwaka 136,000 mpaka 12,000 haya ni mapungufu makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la tatu nataka niongelee mahusiano yetu waajiri, Serikali na wafanyakazi, utatu ambao unasimamiwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO). Tunaunganishwa na Sheria ya Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini, Sheria hii imepitwa na wakati, inashindwa kufanya kazi ya kutibu kasoro ya ajira na kazi na mahusiano kazini kama ilivyokusudiwa. Mfano mzuri tulipatwa na COVID hapa, COVID-19 matokeo yake nchi ilipokuwamba na COVID wafanyakazi fulani walizuiwa majumbani, wengine waliwekwa karantini hospitali lakini waajiri wengine walifunga, lakini muda wote huu waajiri walitakiwa kuwalipa wafanyakazi mishahara yao, hii haikuwa sahihi kwa sababu waajiri hawakuleta COVID hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wao kuendelea kuwalipa wakati hawazalishiwi mali yoyote na wafanyakazi ambao walikuwa wanafanya kazi kwa muda wa kulipwa kila siku wakang’ang’ania kwenda kazini ambako hakuna kazi na mwajiri amefunga mlango. Kwa hiyo, wafanyakazi waliokuwa wanapata hela kwa wiki hawakupata hela, waajiri mali haikuzalishwa lakini vilevile waliofungiwa ndani kwa sababu ya COVID hawakufanya kazi, lakini waajiri walitakiwa kuendelea kuwalipa. Tuona kwamba sheria hii sasa Serikali iilete kupia Baraza la Sheria za Kazi (LESCO) ili iweze kurekebishwa iweze kutibu kasoro au mapungufu haya ambayo tumeyaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia pia sekta ya ulinzi binafsi ambayo inafanya kazi kwa kutumia sheria hii ya kiraia ipo katika matatizo makubwa sana na haitendewi haki. Moja, hawa wa sekta ya ulinzi binafsi wanabeba silaha, wanavaa sare, wanafanya kazi kama askari lakini wanatumia Sheria hii ya Kiraia na sheria hii itakuwa sawa tu kama sheria hii ya Labour Relations Act ya mwaka 2004 itarekebishwa. Sasa hivi wafanyakazi hawa askari, walinzi wanalazimishwa kufanya kazi masaa mengi zaidi kuliko saa ambazo zimetajwa katika Sheria hii ya Labor ya sasa. Kwa hiyo, tungependekeza sheria mpya itakayokuja itibu pia tatizo la askari binafsi wa ulinzi ambao wanafanya kazi kama askari lakini wanatumia Sheria ya Kiraia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake ni nini? Wakati huo wote ambao askari hawa, walinzi hawa binafsi wanafanya kazi wanasukumwa na sheria hii ya sekta ya ulinzi binafsi ambayo haipo, lakini wanasukumwa sasa na sheria hii ya kiraia, matokeo yake waajiri wengi wako mahakamani - CMA kwa ajili ya kudai overtime au kwa ajili ya kutumikishwa masaa ya ziada kuliko ambavyo sheria inataka. Dawa yake ni kuleta Sheria mpya ya Ajira, Kazi na Maelewano kazini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa ruhusa, ahsante sana. (Makofi)