Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika hoja mbili ambazo ziko mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuwapongeza Wenyeviti wote wawili wa Kamati ambao wamewasilisha vizuri sana lakini nipongeze pia Kamati zetu ambazo zimejadili vizuri na hatimaye kuja na taarifa hizi ambazo tutazitolea maazimio. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesikia kuna mapungufu yamezungumzwa lakini niseme tu kwamba mapungufu yote ambayo yanazungumzwa haina maana kwamba Serikali haijafanya kazi. Serikali imefanya kazi sana, kazi nzuri katika sekta zote ambazo zimewasilishwa hapa, na kwa namna ya pekee nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais wetu Mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wasaidizi wake ambao ni Mawaziri wa Wizara ambazo zinahusika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye Wizara ya Elimu. Mimi nitazungumzia kidogo mapungufu ambayo tumekuwa tukiyaona pamoja na kazi nzuri nyingi sana ambazo zimefanyika katika Wizara ya Elimu, ikiwa ni pamoja na ujenzi na miradi ya HEET pamoja na ujenzi wa vyuo vya VETA na vyuo vingine lakini kuna tatizo kubwa sana la ajira katika Wizara hii, tatizo kubwa sana la ajira za Walimu. Tumekuta katika mijadala yetu kuna upungufu mkubwa wa walimu katika shule zetu hususani Walimu wa Sayansi na Hesabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Kamati kuwa upande huu kuomba nguvu zaidi iongezwe katika kuajiri walimu. Kwa maana hiyo basi, uwepo mkakati madhubuti ili kuweza kuhakikisha kwamba ujenzi wa shule au uboreshaji wa miundombinu unakwenda sambamba na ajira za walimu ili tuweze kuimarisha elimu na kutoa elimu iliyo bora kwa watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la elimu ya watu wazima limeshazungumzwa pia. Katika ziara zetu tulikuta kule kuna changamoto ambayo walimu wanajitolea sana na wanafundisha. Hii elimu ni ya lazima sana kwa wale ambao wameacha shule kwa sababu mbalimbali, lakini utaona kwamba ukilinganisha elimu iliyo rasmi na elimu ya watu wazima, utaona Serikali imeelekea upande mmoja kwamba inatoa elimu bure kwa elimu rasmi, lakini hakuna fungu katika hii elimu ya watu wazima. Hivyo niungane na Kamati kuishauri Serikali itoe fungu la elimu bure ili kuwawezesha wale ambao wanawasaidia vijana wetu ambao wameacha shule katikati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mwingine nizungumzie wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwemo watoto wenye ulemavu. Kazi inayofanyika kule kwenye idara hii ni kubwa sana, lakini utashangaa fungu ambalo linatoka, kwa mfano kama kipindi hiki zimetoka shilingi milioni 300 tu, na ukilinganisha idadi, ni kubwa mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme tu kwa mfano kuna kazi ambayo inabidi walimu waende moja kwa moja katika majumba ya hawa watoto wenye ulemavu ambao hawawezi kufika shule, watahitaji nauli. Naiomba sana Serikali iongeze fungu katika upande huu ili kuwawezesha walimu kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mikopo ya elimu ya juu, ushauri wangu ni kwamba Serikali iruhusu sasa Wizara au Bodi ya Mikopo iweze ku-retain zile fedha zinazorejeshwa. Naambiwa ni zaidi ya shilingi trilioni moja. Sasa kama shilingi trilioni moja imekuwa retained, ina maana itasadia wanafunzi walio wengi ambao hawapati mikopo na inawezekana pia watoto wote wakapata mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Utamaduni inahusika sana na Sekta ya Burudani na Sanaa. Sekta ya Burudani na Sanaa ina sifa kuu mbili; ya kwanza, hii ni software au ni nguvu laini ya Taifa; pili, sekta hii inakua kwa kasi kubwa sana kuliko sekta zote. Kwa mfano, mwaka 2022 imekua kwa asilimia 19. Kuna changamoto kubwa hapa, budget sealing. Samahani nakwenda kwenye maeneo haya kwa sababu ni mahitaji muhimu sana katika maendeleo ya sekta hizi. Budget sealing ni ndogo na ukiangalia vipaumbele vingi katika Wizara hii vimeshindwa kutekelezwa kwa mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona hata yale maeneo ambayo yamepangiwa budget kwa mfano shilingi milioni 60, kwenye ujenzi wa Kiwanja cha kisasa hapa Dodoma na hiki ni kipaumbele kwa sababu utakikuta kwenye kifungu cha 243 (a) cha Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi. Imetengwa shilingi milioni 60, lakini hakuna hata shilingi moja ambayo imetolewa. Sasa unajiuliza, watu hawa watafanyaje kazi? Kwa sababu inakuja kutokea kwamba kila wanapokuja kwenye Kamati wanazungumzia mambo yale yale ambayo pesa yake inatolewa kidogo kidogo au wakati mwingine haitolewi. Ni kwa sababu utekelezaji haupo kutokana na kutokupata mafungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana sana Serikali iangalie Wizara hii kwa jicho la kipekee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)